Media » News and Events

Dk.Shein afungua barabara ya Jendele-Cheju- Unguja Ukuu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiondoa kipazia kuashiria kuweka jiwe la msingi la Uzinduzi wa Baraza ya Jendele hadi Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja, kulia Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe na kushoto Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Hassan Khatib, hafla hiyo imefanyika katika barabara hiyo jendele ikiwa ni shamrashamra za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 54.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya juhudi katika kuhakikisha inatumia wataalamu wake wazalendo katika kujenga barabara za hapa Zanzibar kwani hatua hiyo tayari imeanza kuzaa matunda.Dk. Shein alisema hayo leo mara baada ya ufunguzi wa barabara ya Jendele-Cheju- Unguja Ukuu ikiwa ni muiongoni mwa shamrashamra za miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964.

Dk. Shein alieleza kuwa vijana wa Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara (UUB) wana utaalamu mkubwa lakini kinachowakwaza ni ukosefu wa vifaa pekee na kueleza kuwa ujenzi unaofanywa na mafundi wazalendo hupelekea kujenga barabara imara kwa fedha kidogo ikifananishwa na Kampuni za kutoka nje ya Zanzibar.Alisisitiza haja ya kujitegemea katika kujenga barabara za hapa nchini na ndipo Serikali imeamua kutoa fedha kwa ajili ya kununua vifaa ili kuandeleza shughuli hizo kwa ufanisi mzuri zaidi huku akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kufanya mambo yake.

Dk. Shein aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni mpango wa Serikali wa kujenga barabara hiyo na wala Serikali haijakurupuka kwani barabara hiyo itasaida katika usafirishaji wa mazao mbali mbali yakiwemo mpunga pamoja na bidhaa nyengine na wananchi.Alisema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yameleta umoja na usawa miongoni mwa wananchi wa Zanzibar na wala hayajambagua mtu kwa rangi yake, dini yake, kabila lake na yote yanayofanywa Unguja yanafanywa na Pemba, na yanayofanywa mjini hufanywa na vijijini.

Download File: