Media » News and Events

Dk.Shein aliwaongoza Waumini wa dini ya Kiislamu katika Maulidi ya Mtume Muhammad (SAW)

Sherehe hizo za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo hufanyika kila mwaka Kitaifa hapa Zanzibar ni miongoni mwa kawaida na mila ya Waislamu wa Zanzibar.

Alhaj Dk. Shein aliungana na Waislamu na wananchi hao wakiwemo viongozi mbali mbali wa Dini na Serikali pamoja na wananchi ambapo pia,Mama Mwanamwema Shein nae alihudhuria Maulid hayo akiwa pamoja na viongozi wengine wanawake wa Kitaifa.

Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji alitumia fursa hiyo kuwakaribishwa wananchi wote pamoja na viongozi mbali mbali akiwemo Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein katika sherehe hizo za Maulid.

Katika Sherehe hizo, Waislamu walisisitizwa suala zima la amani, umoja na mshikamano miongoni mwao na kutakiwa kufuata nyayo za Mtume Muhammad (S.A.W) ili wapate kuongoka hapa duniani na kesho akhera.

Akisoma khutba Sheikh Muhammed Kassim Said kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana aliwataka Waislamu kuwa kitu kimoja huku akiwasisitiza umuhimu wa kusaidiana na kuhurumiana kwa lengo la kupata rehema za Allah.

Sheikh Muhammed pia, alitumia fursa hiyo kukemea mambo maovu katika jamii hasa suala la unyanyasaji wa wanawake na watoto ikiwa ni pamoja na suala zima la ubakaji jambo ambalo limeanza kushamiri hivi sasa katika jamii na kueleza athari zake na kutaka mashirikiano ya pamoja katika kulipiga vita.

Aidha, alieleza kuwa ni jukumu la Waislamu kusherehekea siku hii adhimu pamoja na kufuata mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W) aliyokuja nayo.

Sherehe hizo za Maulid ambazo husherehekewa duniani kote, zilianza kufunguliwa na Qur-an tukufu iliyosomwa na Ustadhi Hamdan Juma Hamdan kutoka
Magogoni Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo tafsiri yake ilitolewa na Sheikh Ali Muobwa Hassan kutoka Chuo cha Kislamu Zanzibar.

Milango ya Maulid Barzanji iliyoenda sambamba na Qasweeda ilisomwa na Maustadhi kutoka vyuo mbali mbali vya Qur-an kutoka Unguja na Pemba yakiwemo Maulid ya Hom kutoka Jumuiya ya Maulid ya Hom Mtendeni,Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo nayo yalikuwa kivutio kikubwa katika sherehe hizo adhimu.

Katika sherehe hizo za Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) Madressa Qamaria ya Kibandamaiti, Mjini Unguja walisoma Qiyam Talaa, kilichotanguliwa na
Mlango wa nne uliosomwa na Ustadhi Abdalla Mjomba Daawa kutoka Madressa Qaqmaria ya Kibandamaiti, Mjini Unguja.

Qasweeda ya mwaka 1439 Alhijra, ilisomwa na wanafunzi kutoka Madrassa Ihsan Islamia kutoka Tumbatu Gomani, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maulid hayo Sheikh Sherali Chapsi alitumia fursa hiyo kama ilivyokaida kwa kila mwaka kumkabidhi Rais, Qasweda hiyo
maalum.

Maulid hayo yalimalizika kwa Mlango wa dua uliosomwa na Sheikh Wazir Hassan Choum, kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi na hatimae kufungwa kwa fatha iliyosomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Qabih chini ya mshereheshaji Sheikh Hamza