Media » News and Events

Dk.Shein ameipongeza Ofisi ya Rais,Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais,  Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi wake kwa Mwaka 2016/2017,Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2017/2018 na Utekelezaji wake kwa kipindi cha
robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba, 2017.

Dk. Shein alionesha furaha yake kwa kuonesha mafanikio makubwa yaliopatikana katika utendaji wa kazi uliowasilishwa na Ofisi hiyo na kueleza kuwa Ofisi hiyo ambayo inashugulikia Katiba, Sheria na Utawala Bora ina changamoto nyingi lakini hata hivyo ni vyema zikapatiwa ufumbuzi.

Aliongeza kuwa mbali ya kuwa na Utawala Bora lakini lengo la Serikali ni kutoa huduma bora na zenye kiwango kizuri ili wananchi wasinungunike na kuitaka Ofisi hiyo kuendelea kufanya vizuri zaidi katika kuwatumikia wananchi na kuwapa huduma bora.

Aidha, alileza kuwa katika nchi za Afrika Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mwanzo zilizoanzisha Wizara ya Utawala Bora ambapo kwa hivi sasa Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa sana hivyo, ni vyema ikaimarisha ubora na weledi wake.

Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa pale wanaposikia malalamiko ya wananchi ni vyema wakayafanyia kazi na kuitaka Ofisi hiyo kuwasikiliza wananchi mawazo yao kwani ni njia moja wapo ya kufuata Utawala Bora.

Pia, alisisitiza suala zima la uwajibikaji sambamba na kuimarisha na kuendeleza ushirikiano na umoja miongoni mwa viongozi hao na watendaji wa Ofisi hiyo na kuitaka kuendelea kufanya kazi kwa kasi ili tija iweze kupatikana.

Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd aliipongeza Ofisi hiyo kwa mafaniko iliyoyapata huku akisisitiza haja ya kuendelea kutoa elimu
kwa wananchi juu ya suala zima la kupambana na vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uongozi wa Ofisi hiyo kwa uwasilishaji mzuri wa Mpangokazi
wake na kusifu mashirikiano mazuri anayoyapata kutoka Wizara hiyo ambayo yanamsaida katika utendaji wake wa kazi.

Waziri wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Katiba,Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa uongozi wake thabiti na shupavu unaowafanya wasaidizi aliowateua kwa imani kubwa kusimamia na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu na sheria na taratibu zilizopo.

Alieleza kuwa utaratibu aliouanzisha wa Bangokitita ambao huwakutanisha na watendaji wakuu wa Wizara mbali mbali ni mzuri na unastahiki kupigiwa mfano kwa
sababu unajenga kivitendo misingi ya Utawala Bora ambayo inahimiza masuala mazima ya uwazi na uwajibikaji.

Aidha, Waziri Haroun alisema kuwa Mfumo wa kisasa wa usimamizi wa kesi kwa njia ya kielektroniki umewekwa katika Mahkama Kuu Vuga kwa maajiribio na utawekwa katika Mahkama nyengine zote Unguja na Pemba kufikia mwaka 2020.

Katika kusimamia maadili ya viongozi wa Umma Waziri Haroun alileza kuwa elimu imetolewa kwa viongozi wa Umma kuhusu umuhimu wa maadili ya viongozi wa Umma, sheria ya Maadili ya Umma na utaratibu wa kujaza fomu za tamko la mali na madeni.

Aliongeza kuwa katika kuzuia vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi mikutano iliyolenga kukuza uelewa wa jamii kuhusu majukumu ya Mamlaka na umuhimu wa kuepuka vitendo vya rushwa ilifanyika kwa taasisi za Serikali Unguja na Pemba.

Nao uongozi huo ulipongeza hatua hizo za Rais za kukutana na viongozi na kujadili Mipangokazi ya Mawizara na kueleza kuwa mfumo huo umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa na kupelekea baadhi ya nchi jirani kuufuatilia na kuanza kuuiga mfumo huo ambao Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeuanza kwa miaka sita hivi sasa.

Wakati huo huo,  Dk. Shein alikutana na uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kuipongeza Ofisi hiyo kwa mafanikio iliyoyapata na kumpongeza Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd kwa kuisimamia vyema Ofisi hiyo.

Dk. Shein alimpongeza Balozi Seif kwa kuiongoza vyema Ofisi hiyo licha ya kuwa ni na kuwa na mambo mengi na Idara nyingi lakini ameweza kuiongoza vyema na kuweza kupata manufaa kutokana na kuwa ndio Ofisi inayoratibu masuala ya Serikali.

Dk. Shein alieleza matarajio yake kuwa juhudi zaidi zitaendelea kuchukuliwa na uongozi wa Ofisi hiyo ili Serikali iendelee kupata tija na mafanikio bora zaidi huku akitumia fursa hiyo kueleza jinsi Zanzibar ilivyopiga hatua katika kuimarisha mapato yake hatua iliyopelekea kufanya mambo yake mengi wenyewe..

Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kufanya kazi kwa kujituma ili Ofisi hiyo iendelee kuleta sifa na kuendelea kumsaidia Makamo wa Pili wa Rais katika
kutekeleza majukumu yake .

Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd aliipongeza uongozi wa Ofisi hiyo kwa kukusanya taarifa nzuri na kuwasilisha katika kikao hicho kwa ufaisi ulio bora huku akiitaka Ofisi hiyo ijiandae vyema katika kikao kijacho kama hicho sambamba na kuwapongeza viongozi na watendaji wa Ofisi hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alimpongeza Dk. Shein kwa namna anavyoiongoza Zanzibar ambapo kila mmoja anashuhudia mageuzi makubwa ya utendaji kazi kwa watumishi hasa sekta ya umma.

Aliongeza kuwa mageuzi hayo yamechochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi katika sekta zote ambapo wasaidizi wake wote wanazingatia sana miongozo na maelekezo yake katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia shughuli za Srrikali katika maeneo yao.

Nao uongozi wa Ofisi hiyo ulieleza kufarajika kwao na hatua za Dk. Shein za kuanzisha na kuendeleza vikao hivyo ambavyo vimekuwa vikiwasaidia sana viongozi na watendaji wa ofisi hiyo katika utekelezaji wa kazi zao pamoja na mafanikio yaliofikiwa na Serikali katika kutoa huduma mbai mbali katika jamii.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uongozi wa Ofisi hiyo kwa uwasilishaji mzuri wa Mpangokazi wake na kusisitiza haja ya uongozi huo kujitahidi ili kuonesha taswira nzuri ya Makamu wa Pili wa Rais pamoja na Ofisi yenyewe.