Media » News and Events

Dk.Shein ameipongeza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum

Alieleza kuwa uogozi wa Awamu ya Saba umeingia madarakani ukihakikisha kuwa unafuatilia kwa karibu katika kutatua migogoro ya ardhi na haitokuwa tayari kuibua migogoro mipya na kuutaka uongozi huo kushirikiana kwa pamoja katika kutatua changamoto za ardhi zilizopo.Aidha, Dk. Shein alieleza kuridhishwa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na uongozi wa Wizara hiyo na kuupongeza uongozi huo kwa kazi nzuri ya uwasilishaji wa Mpangokazi wao hasa ikizingatiwa kuwa Wizara yao ina mamabo mengi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa kulisimamia vyema zao la karafuu hasa kwa kutambua umuhimu wa zao hilo katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar.Dk. Shein alieleza imani yake kubwa kwa viongozi hao na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa kuwatumikia wananchi vizuri sambamba na kuongeza kasi ili waweze kufanya kazi vizuri zaidi ili Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iendelee kupata sifa Kitaifa na Kimataifa.Katika maelezo yake, Dk. Shein aliueleza uongozi wa Wizara hiyo kuwa sifa kubwa ya kiongozi ni kuwasikiliza anaowaongoza wakiwemo wananchi na kuwataka kwenda kwa wananchi kwa lengo la kuwasikiliza changamoto walizonazo pamoja na mafanikio waliyoyapata ambayo watawaeleza viongozi hao.

Akielezea umuhimu wa Mpango wa Ugatuzi, Dk. Shein alisisitiza haja ya kukushanya mapato na kuhakikisha kodi zinalipwa ipasavyo ili Serikali iweze kufanya mambo yake kwa ubora zaidi.Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa ni vyema viongozi wote wa taasisi za Serikali wakatambua kuwa wao wapo kwa lengo la kuwatumikia wananchi kwa mambo ambayo wameyapanga wenyewe na ili wawaridhishe ni vyema wakafanya vizuri.Dk. Shein alieleza haja kwa uongozi huo kuendeleza utaratibu uliowekwa wa viongozi kuzunguza na waandishi wa habari kwa lengo la kuwaeleza mafanikio yaliofikiwa na Serikali kwani Serikali imefanya mambo mengi ambayo mengine wananchi hawayajui.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kufanya utafiti ili kuweza kugundua changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi na majibu yake yakiwemo masuala mazima ya udhalilishaji pamoja na wale wanaofanya vitendo vilivyo nje ya maadili ya Kizanzibari kwa upande wa Unguja na Pemba.Pia, Dk. Shein alizungumzia haja ya kukaa pamoja kwa viongozi wa Mikoa na kuangalia namna na uhifadhi wa taka na ukusanyaji wake sambamba na kuelewa muhusika mkuu wa kushughulikia ya taka ni nani.

Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd aliipongeza Wizara hiyo kwa mafaniko iliyoyapata kupitia taasisi zake na kusisitiza mashirikiano ya pamoja katika kutekeleza majukumu waliyonayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanafuata sheria katika masuala ya ujenzi na kuepuka ujenzi holela.Aidha, Balozi Seif alisisitiza haja katika Mpango mzima wa Ugatuzi kuhakikishwe kuwa wananchi na viongozi wanapewa elimu ya kutosha kuhusiana na mpango huo sambamba na kuimarisha mashirikiano ya pamoja ili kuona yale yote yaliopangwa yanafanyiwa kazi. 

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa upande wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mafanikio waliyoyapata na jinsi walivyowasilisha taarifa yao huku akipongeza kwa mwanzo mzuri wa Mpango wa Ugatuzi.

Waziri wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri alimpongeza Dk. Shein kwa uongozi wake mahiri katika kusimamia taasisi za Serikali kwa lengo la kuhakikisha utoaji wa huduma kwa wananchi unaimarika na zinapatikana kwa wakati na zikiwa katika hali ya ubora.Alimuhakikishia Rais kuwa Ofisi yake inaendelea kutekeleza kwa vitendo mipango mikuu ya Kitaifa na maelekezo anayoyatoa Rais ili kufanikisha upatikanaji wa huduma hizo muhimu kwa ustawi wa maisha ya wananchi wote.

Aidha, Uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba ulieleza namna wananchi wa Mkoa huo walivyohamasika kwa kiasi kikubwa katika kulitumia soko la Tumbe kwa shughuli zao mbali mbali zikiwemo uuzaji samaki pamoja na minada sokoni hapo.Uongozi huo ulieleza mikakati iliyowekwa kwa kupitia uongozi wa Mikoa katika kuhakikisha vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto vinatokomezwa.

Sambamba na hayo, ulieleza namna unavyofanya juhudi katika kutatua migogoro ya ardhi kwa mashirikiano ya pamoja kati yao na Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira hasa migogoro inayohusiana na mipaka pamoja na umilikaji wa ardhi.Pia, uongozi huo ulitoa pongezi kwa ziara ya Dk. Shein aliyoifanya mwezi Agosti 2017 katika Mkoa wa Kaskazini Unguja katika vijiji vya Mlilile na Mbuyumaji, ambapo maagizo aliyoyatoa katika ufikishaji wa huduma za katika maeneo hayo zimeanza kutekelezwa na tayari Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) wameshafikisha umeme Mlilile na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA)  tayari wameshachimba kisima Mbuyumaji na huduma zilizosalia ni skuli, barabara na kituo cha afya.