Media » News and Events

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka vipaumbele kwa akina mama na watoto    

Mama Shein aliyasema hayo leo huko katika nyumba ya watoto Mazizini katika uzinduzi wa huduma ya upimaji afya kwa watoto waliopo katika nyumba hiyo chini ya madaktari kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

Katika maelezo yake Mama Shein alieleza kuwa uwamuzi wa Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China uliopo Zanzibar kuwapima afya watoto wanaoishi katika nyumba ya kulelea watoto Mazizini, ni hatua ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais, Dk. Ali Mohamed Shein katika kuimarisha sekta ya afya.

Alieleza kuwa katika kufikia dhamira hiyo ya Serikali, Serikali ya China kupitia Ubalozi wake hapa Zanzibar umekuwa bega kwa bega kwa kuleta madaktari, kutoa mafunzo kwa wataalamu, kutoa vifaa na hata kujenga miundombinu ya afya hapa nchini.

Aliongeza kuwa ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee, iliyopo Mkoani Pemba, ni kielelezo kizuri cha mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na wananchi wake kwa wananchi wa Zanzibar katika maendeleo ya sekta ya afya.

“Wahenga walisema ‘Akufaae kwa dhiki, ndiye wako rafiki’, kwa hakika nyinyi ni marafiki wa kweli, misaada yenu mbali mbali imepelekea uhusiano wa nchi zetu kuzidi kuimarika siku hadi siku, hongereni sana”,alisema Mama Shein.

Aidha, Mama Shein alisisitiza kuwa upimaji huo ni vyema ukaenda sambamba na hatua ya utoaji tiba na ushauri kwa watoto hao ili waweze kuishi kwa furaha na kutoa wito kwa wazazi kuwa na utaratibu wa kwenda kliniki kuangalia afya za watoto na kutosubiri hadi tatizo likawa kubwa.

Pia, Mama Shein alitoa rai kwa Taasisi mbali mbali kuendeleza utaratibu wa kambi za kupima afya za watoto na wananchi kwa jumla kwani jukumu la kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora ni la kila mtu.

Mama Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Mke wa Balozi Mdogo wa China Bibi Liu Jie kwa uwamuzi wake wa kushiriki pamoja katika harakati za kuwasaidia wanawake wa Zanzibar ambapo kwa mara hii ameamua kuja na madaktari kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa ajili ya kutoa huduma za upimaji wa afya ya watoto pamoja na kutoa zawadi.

Alisisitiza kuwa hatua hiyo ya Bibi Liu ni ishara ya imani na mapenzi makubwa aliyonayo kwa watoto wa Zanzibar ambapo pia, ni kielelezo cha udugu na urafiki wa kihistoria kati ya Zanzibar na Wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China.

Sambamba na hayo, Mama Shein aliushauri Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar kufanikisha huduma hiyo ya upimaji wa afya kwa wazee wanaoishi katika nyumba za wazee Sebleni na Welezo pamoja na wale walioko nyumba ya Wazee Limbani Pemba.

“Wazee wetu wengi wana mitihani mbali mbali ya kiafya kwa hivyo, ni wajibu wetu kuwahudumia, kuwaenzi, kuwatunza na kuwaombea dua….Tumombe Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu amani, umoja na masikilizano, ili tuweze kupiga hatua zaidi za maendeleo, sisi na watoto wetu”,alisema Mama Shein.

Nae alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya China uliopo Zanzibar kwa mashirikiano mazuri unayoyaendeleza kwa kutambua historia ya nchi mbili hizi.

Nae Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico alieleza jinsi watoto wa nyumba ya kulelea watoto walivyofarajika na hutua hizo za Ubalozi Mdogo wa China uliopo hapa Zanzibar kwa kuwapelekea huduma za upimaji, dawa, chakula na vifaa vya michezo pamoja na zawadi mbali mbali na kusisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano wa China na Zanzibar utaendelezwa.

Mke wa Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anaefanya kazi zake hapa Zanzibar Mama Liu Jie alieleza kuwa zoezi hilo la upimaji wa afya kwa watoto hao litaendeshwa na kundi la 27 la madaktari kutoka China waliopo hapa Zanzibar.

Mama Liu Jie aliwapongeza Mama Mwanamwema Shein pamoja na Dk. Shein kwa juhudi zao za kuwajali wanawake na watoto sambamba na kuhakikisha kuwa maisha yao yanakuwa bora.
Alimpongeza Mama Shein pamoja na Mama Asha Balozi kwa utaratibu wao waliojiwekea wa kwenda kuwatembelea watoto hao mara kwa mara huku akieleza kuwa vijana ni tegemeo kubwa la maendeleo ya Zanzibar hivyo ni vyema wakaendelezwa, wakatunzwa, wakasomeshwa na wakaenziwa.

Aliongeza kuwa wazo la ujenzi wa nyumba ya watoto lilitolewa na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume mnamo Novemba 1, mwaka 1966 ikiwa ni miaka 51 hivi sasa tokea kuanzishwa kwa huduma hizo zilianzia nyumba ya Forodhani mjini Unguja na baada ya kuwepo changamoto kadhaa watoto hao walihamishiwa Mazizini kwenye jengo hilo lliiojengwa kwa mashirikiano kati ya Mama Shadya Karume Mwenyekiti wa ZAYEDESA na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, Mama Liu Jie alitumia fursa hiyo kuahidi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Ubalozi wake huo wa Zanzibar uko tayari kuchangia ustawi wa watoto wa Zanzibar kwa lengo la kuendeleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuwahudumia watoto ili waishi maisha bora.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Fatma Bilali alieleza kuwa nyumba hiyo ya Mazizini kwa hivi sasa ina jumla ya watoto 39 na walezi wao 33 ambapo vijana hao mara wanapofikia umri wa miaka 18 huwarejesha kwa familia zao.

Aliongeza kuwa huduma katika nyumba hiyo zimeimarishwa zikiwemo za chakula, mazingira bora ya malazi na makaazi pamoja na fedha kwa kila mwisho wa mwezi ambapo kila mtoto hupewa 20,000 huku wakiwa na usimamizi na matunzo mazuri.

Nao watoto wanaoishi katika nyumba hiyo walitoa pongezi kwa huduma hizo za afya walizopelekewa pamoja na msaada wa chakula, dawa na vifaa vya michezo.

Katika uzinduzi huo viongozi mbalimbali walihudhuria akiwemo Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Balozi, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Rizi Pembe Juma, Mke wa Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Mama Liu Jie, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Marina Joel pamoja na viongozi wengine.

Hafla hiyo ilienda sambamba na burudani ya nyimbo zilizoimbwa na watoto wa kituo hicho pamoja na nyimbo za kichina zilizoibwa na vijana wenye asili ya China pamoja na watoto wa Zanzibar.