Salamu za pongezi ametumiwa Sultan wa Oman,Sultan Qaboos Bin Said Al Said na Dk.Shein

Salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wa Oman katika kusherehekea siku hii adhimu kwa Taifa hilo.

Aidha, katika salamu hizo, Dk. Shein alimuhakikishia Sultan Qaboos Bin Said Al Said kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati
yake na Oman sambamba na kuimarisha udugu uliopo kati ya wananchi wa Oman na wananchi wa Zanzibar.

Sambamba na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa siku hii adhimu inaendelea kutoa nafasi zaidi ya mashirikiano kati ya pande mbili hizo pamoja na kupongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Oman katika kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.

Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo pamoja na familia yake na wananchi wote wa Oman afya njema na sherehe njema katika kuadhimisha siku hiyo huku akimtakia kiongozi huyo mafanikio zaidi katika kuendelea kuipatia maendeleo zaidi ya kiuchumi nchi hiyo kwa madhumuni ya kulinufaisha Taifa hilo pamoja na wananchi wake.

Oman ilipata uhuru wake kutoka ukoloni wa Kireno mnamo Novemba 18 mwaka 1650 chini ya kiongozi na muasisi wa Taifa hilo Imam Sultan Bin Saif Bin Malik Al Yarubi ambaye alisimamia kung’oka kwa koloni hilo kutoka nchini Oman pamoja na bandari zote za nchi hiyo zilizokuwa chini ya Ureno.