Media » News and Events

Ufunguzi wa Msikiti Saeed Al Bawardy uliopo Bandamaji, Jimbo la Chaani,

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Msikiti Saeed Al Bawardy uliopo Bandamaji, Jimbo la Chaani, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika maelezo yake, Alhaj Dk. Shein aliwasisitiza Waumini wa dini ya Kiislamu kujiepusha na makundi ya watu ambao kwa kutumia mbinu mbali mbali hufanya bidii kupanda mbegu za fitina na kuchochea mifarakano, husda na chuki.

Alhaj Dk. Shein aliwataka Waumini wa dini ya Kiislamu kushikamana na subira,mapenzi na kuendesha maisha yao kwa kuzingatia misingi ya busara na pale wanapokutana na misukosuko na inapoibuka mizozo wazirejeshe nafsi zao kwa MwnyenyeziMungu kwani yeye ameshawaonesha njia kwa mitihani kama hiyo.

Aliongeza kuwa katika kuendesha mambo yao ili yafanikiwe ni lazima wawe tayari kushauriana wakati wote kama MwenyeziMungu alivyofahamisha katika Suratul Ash-Shuura aya ya 38.

Zaidi ya hayo, Alhaj Dk. Shein katika nasaha zake aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu waendelee kuishi kwa kupendana, kuvumiliana na kustahamiliana huku akiwataka kujiepusha na kiburi, hasira, chuki na fitna, ili waweze kusihi kwa furaha na kuepuka kujitia katika matatizo yasiyo na faida kwa maisha ya hapa duniani na kesho Akhera na kusisitiza kwua Serikali iko pamoja nao.

Aidha, Alhaj Dk. Shein alitoa shukurani kwa mfadhili wa msikiti huo Sheikh Saeed Al Bawardy pamoja na Sheikh Yakoub Osman na mtoto wake Adil kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa msikiti huo pamoja na kutoa shukurani kwa mjenzi Sheikh Amour.

Alhaj Dk. Shein aliendelea kuikumbusha Ofisi ya Mufti kuwa na utaratibu wa kukagua utunzaji wa misikiti kwani imebainika kuwa kuna misikiti mingi ya kisasa inayojengwa kwa gharama kubwa hivyo kuna haja ya kujua maendeleo yake na utunzaji wake ili iweze kudumu na kutumiwa vizuri katika kufanya ibada huku akiwataka waumuni hao kuutunza msikiti huo.


Akielezea juu ya ufumbuzi wa changamoto zinazokikabili kijiji cha Bandamaji,zikiwemo ukosefu wa maji safi na salama pamoja na barabara fursa ya skuli ya sekondari Alhaj Dk. Shein alieleza hatua zinazokusudiwa kuchukuliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika kuhakikisha kuwa ipo haja ya kurejesha madarasa ya elimu ya sekondari katika Skuli ya Bandamaji kama ilivyokuwa hapo awali.

Aidha,kwa upande wa tatizo la maji safi na salama alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mradi wa Maji wa Ras-Al- Khaimah tayari vimeshachimbwa visima viwili ambavyo kukamilika kwake kutaondosha kabisa changamoto hiyo.

Pamoja na hayo,alieleza kuwa hatua inayofuata ni kuviendeleza visima hivyo kwa gharama inayokadiriwa kuwa TZS milioni 300 ambapo kwa upande mwengine Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Watu wa China, ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo na si muda mrefu litafanikiswa.

Kwa upande wa barabara Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa mipango mbali mbali ya maendeleo ili kuimarisha ustawi wa wananchi ambapo hivi sasa inaendelea kukamilisha taratibu zilizobaki ili kuanza ujenzi wa barabara ya Bububu-Kinyasini-Mkokotoni kupitia Kinyasini, Chaani na Mkwajuni.

Nao wananchi wa Bandamaji katika risala yao iliyosomwa na Ustadh Makame Bakar Shadhil walitoa pongezi kwa Alhaj Dk. Shein kwa kuwafungulia msikiti wao pamoja na kumpongeza na kumshukuru mfadhili wa msikiti huo ambaye mbali na kuwajengea msikiti huo pia amewachimbia kisima, amewajengea madrasa,amewapakia rangi skuli yao paoja na kuwajengea vyoo sita. Aidha, walieleza changamoto walizonazo katika kijiji hicho ikiwemo maji safi na salama pamoja na barabara.

Nae Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih alieleza fadhila za kujenga misikiti ambapo katika ufunguzi huo viongozi mbali mbali wa Serikali na vyama vya siasa, wananchi pamoja na Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Alhaj Balozi Seif Ali Idd.