News and Events

Dk.Shein akitoa salamu zake kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika mjini Dodoma.


MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa ataendelea kushirikiana na Mwenyekiti wa CCM Taifa,Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kama alivyofanya kwa Marais wastaafu Rais Benjamin William Mkapa na Rais Jakaya Kikwete katika uongozi wao wakiwa marais Jamhuri ya Muungao wa Tanzania.

Dk.Shein akitoa salamu zake kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika mjini Dodoma.

Dk.Shein aliyasema hayo wakati akitoa salamu zake kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, uliofanyika mjini Dodoma huko katika ukumbi wa Mkutano wa Kikwete.

Katika mkutano huo Dk. Shein, aliwahakikishia Wajumbe hao wa Mkutano Mkuu maalum kuwa ataendelea kufanya kazi kwa pamoja na mwenyekiti huyo na kushirikiana nae katika kukitumikia chama hicho pamoja na kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani na pongezi kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na kueleza matumaini yake makubwa aliyonayo kutokana na
uongozi wa Mwenyekiti huyo ndani ya chama hicho kikubwa na kikongwe katika vyama vya bara la Afrika.
Aidha, Dk. Shein aliwaeleza wajumbe hao umuhimu wa kuendelea kufaya kazi kwa kushirikiana kwa pamoja sambamba na kufuata kanuni na maadili ya Chama.

Aliongeza kuwa kuna haja kwa wanaCCM wakaendelea na utamaduni wa kuzipitia kanuni na maadili ya chama hicho ili kiendelee kupata mafanikio makubwa zaidi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa CCM kwa kukubali kwa pamoja mabadiliko ya Katiba ya CCM kwa lengo la kukiimarisha na kukipa maendeleo zaidi chama hicho.