News and Events

DK.SHEIN AKUTANA NA BODI YA WAKURUGENZI KAMISHENI YA UTALII,UONGOZI WA WIZARA YA FEDHA NA MIAPANGO


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameitaka Kamisheni ya Utalii kuongeza kasi katika kuimarisha dhana ya utalii kwa wote kwani tayari dhana hiyo imeanza vizuri katika kufikia lengo lililokusudiwa.

DK.SHEIN AKUTANA NA BODI YA WAKURUGENZI KAMISHENI YA UTALII,UONGOZI WA WIZARA YA FEDHA NA MIAPANGO

Dk. Shein aliyasema hayo leo, alipokutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Kamisheni ya Utalii pamoja na uongozi wa Bodi hiyo katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar.

Katika vikao vya leo, Dk. Shein kwa nyakati tofauti alikutana na Uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Bodi ya Wakurugenzi ya Kamisheni ya Utalii na uongozi wa Kamisheni ya Utalii, Bodi ya Wakurugenzi wa Gazeti ya Zanzibar Leo ambapo mapema alikutana na uongozi wa Fedha na Mipango, Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Barabara na uongozi wake.

Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na juhudi za Kamisheni hiyo katika hatua za kukusanya mapato kwa njia ya leseni na kusisitiza kuwa Utalii ndio unaotegemewa kwa kiasi kikubwa katika kuongeza pato la taifa hivyo ni vyema juhudi za makusudi zikachukuliwa katika kupata mafanikio hayo.

Mapema, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Barabara na uongozi wake na kutoa pongezi kwa mafanikio yaliopatikana.

Alisema kuwa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya Kamisheni ya Utalii na Uongozi wa Kamisheni hiyo na kueleza haja ya kukuza mashirikiano kati ya Mamlaka hiyo na Wizara kwa lengo la kuimarisha sekta ya uwekezaji.

Akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi ya Gazeti la Zanzibar Leo pamoja na uongozi wake, ambayo iko chini ya Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Dk. Shein alieleza kuridika kwake na gazeti hilo la Serikali hasa pale lilipoanza kuchapishwa hapa Zanzibar kwani fedha nyingi zilikuwa zikitumika pale lilipokuwa likichapishwa nje ya Zanzibar.

Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo ni uwamuzi wa Serikali kwani ilijianda kulichapisha gazeti hilo hapa Zanzibar huku akieleza haja kwa uongozi wa gazeti hilo kutoa zawadi kwa waandishi wao.

Aidha, Dk. Shein aliongeza kuwa ni vyema gazeti hilo likatoa taarifa zake vizuri ili wananchi wapate habari za kwao kwani wananchi wamekuwa wakipenda kusoma na kufahamu habari za kwao.

Aidha, alisisitiza haja ya kuzidisha mashirikiano kati ya uongozi wa Wizara hiyo pamoja na Bodi ya gazeti la Zanzibar Leo sambamba na wafanyakazi wake wote huku akisisitiza haja ya kuifahamu vyema sheria iliyounda gazeti hilo.

Sambamba na hilo, Dk. Shein aliahidi kulitafutia ufumbuzi suala la usafiri kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa gazeti hilo.   

Nao Uongozi wa Mfuko wa Barabara ulieleza mafanikio yaliopatikana katika Mfuko huo ikiwa ni pamoja na kurahisisha upekekaji maendeleo kwenye maeneo yalioongezeka ufikwaji, hivyo kuwasogeze wananchi huduma muhimu za kijamii karibu zaidi.

Pia, uongozi huo ukieleza kuwa hatua inazozichukua katika kuondokana na uchakavu wa barabara ikiwa ni pamoja na kuzijenga upya ama kuzifanyia matengenezo makubwa zilizokuwepo awali.

Nao uongozi wa Kamisheni ya Utalii ilieleza kuwa idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka 294,243 mwaka 2015 hadi 376,242 mwaka 2016 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 27.9.

Uongozi huo ulieleza kuwa idadi ya watalii kutoka katika masoko mapya yakiwemo Urusi, Ukraine, Jamhuri ya Czech, China, India na Izrael imeongezeka kutoka 25,677 mwaka 2015 hadi 53,852 mwaka 2016 ambayo sawa na aslimia 110.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa idadi ya watalii wanaorudi matembezi yao hapa Zanzibar imeongezeka hadi kufikia asilimia 17 huku ukieleza kuwa makusanyo ya Kamisheni ya Utalii yameongezeka ktoka Bilioni 1.4 mwaka 2014 hadi Bilioni 2.2 mwaka 2016/2017.