News and Events

Dk.Shein amefanya mazungumzo na Balozi wa Brazil nchini Tanzania Carlos Alfonso Iglesias Puente


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Balozi wa Brazil nchini Tanzania Carlos Alfonso Iglesias Puente ambapo katika mazungumzo hayo wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano hasa katika sekta muhimu za kiuchuni na kijamii ikiwemo sekta ya biashara ya viungo vinavyozalishwa Zanzibar.

Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu Mjini Zanzibar, ambapo Balozi Puente kwa upande wake alieleza kuwa kuwepo kwa biashara ya viungo kutoka Zanzibar kwenda nchini humo moja kwa moja kutaiongezea mapato Zanzibar kwani Brazil inavipenda na inavitumia sana viungo vya Zanzibar lakini nchi yake imekuwa ikipata usumbufu kwa kuvinunua kupitia nchi nyengine duniani.

Balozi Puente aliongeza kuwa hali hiyo huipelekea nchi yake kununua viungo hivyo kwa bei ya juu ambapo pia, kwa upande mwengine Zanzibar imekuwa haipati pato la kutosha kama ambavyo biashara hiyo ingefanywa moja kwa moja baina ya pande mbili hizo bila ya kupitia nchi nyengine ili kuondoa changamoto hiyo iliyopo.

Hivyo, Balozi Puente alimuhakikishia Dk. Shein kuwa nchi yake iko tayari kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika sekta ya biashara na kueleza hatua zitakazochukuliwa katika kuhakikisha jambo hilo linafanyika ikiwa ni pamoja na kuandaa ziara za kutembeleana kwa viongozi wa sekta hizo, kubadilishana uzoefu na utaalamu, hatua ambayo Dk. Shein aliiunga mkono.

Viongozi hao pia, katika mazungumzo yao walisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano katika sekta hizo za kiuchumi na kijamii ambapo Brazil imeahidi kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya, kilimo, ufugaji, mafuta na gesi, mafunzo, biashara na sekta nyeginezo.

Kuhusu sekta ya afya, Balozi huyo wa Brazil alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake ina mpango wa kuanzisha mradi wa maradhi ya mifupa kwa upande wa Tanzania Bara ambapo alimuahidi kuwa Zanzibar nayo itaingizwa katika utekelezaji wa mradi huo mwishoni mwaka huu.

Kwa upande wake Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa miongoni mwa vipaumbele ambavyo vimewekwa na Serikali anayoiongoza hivi sasa kwa upande wa sekta ya afya ni kuondoa kabisa ama kupunguza vifo vya akina mama na watoto, na kuongeza kuwa iwapo nchi hiyo itaiunga mkono Zanzibar katika kutoa mafunzo na kubadilishana uzoefu na utaalamu itakuwa ni jambo la busara na litasaidiai katika sekta hiyo.

Aidha, Dk. Shein aliwakaribisha wawekezaji wa Brazil kuja kuwekeza Zanzibar katika sekta ya utalii hasa katika ujenzi wa hoteli kubwa za kitalii pamoja na kumbi za mikutano kwa lengo la kuuimarisha utalii wa Zanzibar sambamba na sekta ya uwekezaji.

Aliongeza kuwa kwa vile Brazil imepiga hatu kubwa katika sekta hiyo, hatua hiyo itaisaidia Zanzibar kupanua wigo wa maendeleo, ambapo pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza haja ya kuwepo kwa mashirikiano katika sekta ya mafuta na gesi kati ya pende mbili hizo, jambo ambalo Balozi Puente alilipokea kwa mikoni miwili na kuahidi kulifanyia kazi.

Dk. Shein aliisifu nchi hiyo kwa juhudi zake za kuwatumia Wanadispora, ambapo hivi sasa nchi hiyo imekuwa mfano wa kuingwa katika utekelezaji wa mipango na Sera zinazohusu Diaspora ambapo yeye mwenyewe akiwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipata fursa ya mwaliko wa kuhudhuria Mkutano wa Diaspora mwaka 2008 uliofanyika nchini humo.

Balozi Puente alimuhakikishia Dk. Shein kuwa ataendelea kuitangaza Zanzibar kiutalii nchini mwake wa kumueleza hatua na juhudi atakazozichukua katika kuhakikisha wawekezji kutoka nchini mwake wanakuja kuekeza Zanzibar hasa kutokana na nchi mbili hizi kufanana kimazingira na hali ya hewa.

Pamoja na hayo, Balozi Puente aliisifu Zanzibar kwa jinsi inavyovutia kiutalii pamoja na kuwa na vivutio na rasilimali nyingi za kitalii zikiwemo fukwe, maeneo ya kihistoria, utamaduni, mila, silka na desturi nzuri za Wazanzibar sambamba na ukarimu kwa wageni walionao wananchi wa Zanzibar mambo ambayo yanawavutia wageni kutoka nchi mbali mbali.

Balozi Puente alimpongeza Dk. Shein kwa kuweka milango wazi kwa wawekezaji na watalii kutoka nchini Brazil na kumuhakikishia kuwa atahakikisha kwa upande wake juhudi hizo anaziunga mkono kwa manufaa ya pande zote mbili.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo haja ya nchi hiyo kufungua Ubalozi wake mdogo hapa Zanzibar ili pande mbili hizo zizidi kuimarisha uhusiano na ushirkiano wake kama zilivyofanya baadhi ya nchi nyengine zikiwemo India, China, Misri na nyeginezo ambazo zimeweka Ofisi ndogo za Kibalozi hapa Zanzibar.