News and Events

Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015 pamoja na uchaguzi wa marudio amekabidhiwa Dk.Shein


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein amekabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015 pamoja na uchaguzi wa marudio wa terehe 20 Machi 2016 na kuipongeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar huku akieleza kuwa hiyo ndio ripoti sahihi na hakuna ripoti nyengine.

Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kukabidhiwa Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015 pamoja na Uchaguzi wa Marudio wa terehe 20 Machi mwaka jana, Ripoti ambayo ni kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

Hafla hiyo, ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan, Mawaziri, Washauri wa Rais na viongozi wengine wa Serikali.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Ripoti hiyo ni muhimu sana katika utekelezaji wa kazi za Serikali na kuipongeza Tume ya Uchaguzi pamoja na viongozi wake wote kwa kazi nzuri ya kutayarisha Ripoti hiyo kwa umakini mkubwa na busara pamoja na hekima kubwa.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa wananchi wa Zanzibar kwa kushiriki uchaguzi wa kwanza wa Oktoba 25 mwaka 2015 pamoja na ule wa marudio wa Machi 20 mwaka jana na kutumia haki yao ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Tume ya Uchaguzi inaongozwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya mwaka 1984, hivyo aliwapongeza kwa kuzitumia nyenzo hizo kwa kutekeleza majukumu yao kutokana na changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015.

Dk. Shein alisema kuwa, kama inavyofahamika kuwa Tume hiyo haiingiliwi na taasisi wala mtu yoyote hivyo Tume ndio inayojua ukweli na hatimae ndio imetayarisha ripoti hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwa Serikali pamoja na wananchi wote.

Alisema kuwa kutokana na tukio hilo kuwa muhimu ndio maana amewaalika Mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuja kushuhudia tukio hilo muhimu na kusisitiza kuwa mapendekezo yote anayakubali.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alipongeza mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na Tume ya Uchaguzi ya Taifa na kutumia fursa hiyo kuwapongeza wale wote waliosaidia uchaguzi huo.

Dk. Shein alimueleza Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wake italisimamia kwa karibu suala la changamoto ya ofisi yao kwa kujengwa ofisi nyengine mpya au kufanyiwa ukarabati iliyopo hivi sasa huku akiahidi kufanya ziara siku ya Jumaatatu ili kujionea mwenyewe hali halisi ya ofisi hiyo.

Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jesha Salim Jecha alieleza kuwa Ripoti hiyo inaeleza utaratibu wote wa Uchgauzi tangu uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, mapitio ya uchaguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi, uteuzi wa wagombea.

Pia,  Mwenyekiti Jecha alieleza kuwa Ripoti hiyo inaeleza kuhusu kampeni, kupiga kura, kuhesabu kura hadi kutangazwa kwa matokeo na uteuzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Viti maalum.

Aidha, Mwenyekiti Jecha alisema kuwa Ripoti hiyo imeeleza kufutwa kwa uchaguzi na matokeo yake pamoja na usimamizi wa uendeshaji wa uchaguzi wa marudio mwaka 2016.

Aliongeza kuwa Ripoti ya Uchaguzi ni nyenzo muhimu sana itakayotumika kutoa maelezo ya mchakato wa shughuli zote zilizofanywa katika kipindi chote cha uchaguzi na kusisitiza kuwa uandishi wa Ripoti hiyo hauna tofauti na ripoti nyengine zinazohusiana na Uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani kwa chaguzi zilizopita.

Ripoti hiyo yenye lugha ya kiswahili ina Sura 15, kurasa 302, Majedwali 13 na Viambatisho 28 ambao kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo Ripoti hiyo itasambazwa sehemu mbali mbali zikiwemo Ofisi na Taasisi za Serikali na Mahkama.

Sehemu nyengine ni Baraza la Wawakilishi, Vyama vya Siasa, Maktaba ya Taifa, Maktaba za Vyuo vya Elimu ya Juu, Idara ya Nyaraka, Taasisi zisizo za Serikali pamoja na Wadau mbali mbali ambapo pia, itawekwa kwenye tovuti ya Tume ya Uchaguzi.

Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kueleza changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume hiyo na kueleza kuwa Serikali haina budi kusaidia ili kuzipatia ufumbuzi ikiwemo nafasi finyu katika jengo la Ofisi za Tume hiyo.

Mwenyekiti Jecha alieleza kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatoa shukurani kwa wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyengine na ambao kwa nafasi zao walisaidia kufanikisha uchaguzi huo.

Akiwataja miongoni mwao ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Maendeleo (UNDP) na Washirika wengine wa Maendeleo.

Wadau wengine aliowatajwa ni vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, waaangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje na wanancho wote wa Zanzibar.