News and Events

Dk.Shein ameondoka nchini kuelekea nchini Uingereza kwa safari maalum ya wiki mbili.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, ameondoka nchini leo kuelekea nchini Uingereza kwa safari maalum ya wiki mbili.

Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali walimuaga Dk. Shein wakiongozwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Dk. Shein katika safari hiyo amefuatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein pamoja na Watendaji wengine wa Serikali.

Wakati huo huo, Dk. Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Muungano wa visiwa vya Comoro, Azali Assoumani kwa kutimiza miaka 42 ya Uhuru wa
Taifa hilo.

Kwa niaba yake binafsi, kwa niaba ya watu wa Zanzibar na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Shein alitoa pongezi hizo kwa kiongozi huyo na wananchi wake wote katika Taifa hilo kwa kutimiza umri huo pamoja na kupongeza mafanikio ya kiuchumi na kijamii yanayondelea kupatikana.

Aidha, Dk. Shein alimuhakikishia kiongozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake sambamba na kuimarisha uhusiano wa kihistoria ulipo baina ya pande mbili hizo na watu wake.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alimtakia mafanikio kiongozi huyo pamoja na
wananchi wake na kuwatakia maendeleo katika kuimarisha amani na utulivu uliopo katika Muungano wa visiwa hivyo.