News and Events

Dk.Shein ametoa pongezi kwa Serikali ya Djibouti kwa matayarisho mazuri ya uimarishaji uchumi wake


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi kwa Serikali ya Djibouti kwa matayarisho mazuri ya uimarishaji uchumi wake kwa kukamilisha ujenzi wa Bandari mpya ya mizigo ya mchanganyiko pamoja na Bandari ya makontena na uimarishaji wa Maeneo yake ya Kiuchumi.

Dk. Shein alieleza kuwa kuimarika kwa shughuli za bandari hizo kwa pamoja kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa uchumi wa nchi hiyo na kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.

Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kufanya ziara katika bandari hizo pamoja na kutembelea Maeneo Huru ya uwekezaji na kupata maelezo yaliyoeleza jinsi nchi hiyo ilivyoweka mikakati yake katika kuinua uchumi wake.
Alieleza kuwa Zanzibar ina historia kubwa katika masuala ya Maeneo Huru ya Kiuchumi ambapo harakati hizo zilianza tokea mwaka 1892 ambapo Zanzibar ilitangazwa kuwa ni Bandari Huru.

Juhudi hizo zinaendelezwa na hivi sasa zimekuwa zikiendelezwa kwa kasi kubwa ambapo mnamo mwaka 1992 Maeneno kadhaa yalitangazwa Kisheria kuwa ni Maeneo huru ya Kiuchumi.
Rais Dk. Shein alizipongeza juhudi za Rais Ismail Guelleh wa nchi hiyo kwa kukuza uchumi kwa kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo Bandari pamoja na Maeneo Huru ya Kiuchumi na sekta nyenginezo ambazo zinaipelekea nchi hio izidi kuimarika na kupata maendeleo zaidi.

Dk. Shein alisema kuwa kama ilivyo Djibouti katika mikakati yake ya ujenzi wa Bandari mpya, Zanzibar nayo imo katika hatua kama hizo za ujenzi wa Bandari mpya ya mizigo katika eneo la Mpiga Duri ambayo ujenzi wake utaanza hivi karibuni kwani tayari mchakato wa ujenzi huo umeshaanza.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar iko tayari kushirikiana na kujifunza sambamba na kufanya kazi kwa pamoja na Djibouti katika uendelezaji wa shughuli za kiuchumi ikiwemo Bandari na Maeneo Huru ya Kiuchumi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa ziara kama hizo pamoja na viongozi wengine na watendaji haitokuwa ya mwisho kwani zitasaidia katika kufikia lengo la kushirikiana na kuimarisha uhusiano kati ya pande mbili hizo.
Katika ziara yake hiyo katika Ofisi za Maeneo Huru ya Kiuchumi mjini Djibouti, Dk. Shein alipata maelezo juu ya uendeshaji wa Kamouni hiyo inayojumuisha mkonga wa mawasiliano kupitia katika bahari pamoja na maeneo ya nchi kavu kwa nchi mbali mbali zikiwemo za Afrika ya Mashariki.

Kwa upande wa Zanzibar aliongeza kuwa itaweza kujifunza ni mambo gani ambayo wao wameyafanya na kupelekea kufanikiwa kuwa na Maeneo Huru yaliyopata mafanikio zaidi katika ukanda huo.
Zanzibar itapata fursa ya kuwa na mashirikiano katika kukuza biashara na uwekezaji kupitia ZIPA na Maeneno Huru ya Kiuchumi yaliopo Fumba, ili biashara ambazo zinaweza kufanywa kwa ande mbili hizi kwa mashirikiano ziweze kufanyika kwa mafanikio.

Aliongeza kuwa mashirikiano hayo yatasaidia katika kujifunza namna bora ya uendeshaji wa shughuli za Maeneo Huru ya Kiuchumi kwa njia ya kubadilishana uzoefu na utaalamu kwa watendaji wenyewe.
Kwa mujibu wa maelezo yao, uongozi wa Maeneo Huru ya Djibouti ulieleza kuwa tayari eneo lao limezidiwa na mahitaji ya biashara kiasi cha kwamba wamelazimka kutafuta eneo jengine na kulianzisha upya ambalo lina ukubwa wa ekari 600.
Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza azma yake ya kuwa na eneo la Bandari Huru ambapo kutakuwa na biashara mbali mbali pamoja na kuwa na uwanja wa ndege kwa ajili ya ndege za mizigo zitakazosafirisha kuipelekea nchi nyengine. Aidha, Maeneo Huru hayo yatakuwa na bandari ndogo ndogo.

Mapema Dk. Shein alitembelea Bandari ya makontena pamoja na bandari ya mizigo mchanganyiko ambazo zote zimejengwa hivi karibuni na Kampuni za Ujenzi kutoka China.
Kwa mujibu wa maelezo ya uongozi wa Bandari hizo, kwa pamoja zitaimarisha zaidi biashara baina ya nchi za Ghuba pamoja na nchi zilizopo Kusini mwa Afrika zikiwemo nchi za Afrika Mashariki.

Nao viongozi mbali mbali waliofuatana na Rais Dk. Shein, walieleza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya pande mbili hizo hatua ambayo itakuwa chachu ya kuendeleza na kuimarisha uchumi na maendeleo kati yao.
Wakati huo huo, Dk. Shein akiwa na ujumbe wake alitembelea Bandari ya Ziwa Assal lililoko upande wa Magharibi ya Djibouti katika Mkoa wa Tadjoura na kuona pamoja na kupata maelezo juu ya shughuli za bandari hiyo za usafirishaji wa chumvi kutoka katika Ziwa hilo na kwenda nje na ndani ya nchi hiyo.

Pia, Dk. Shein alipata maelezo juu ya uzalishaji wa chumvi unaofanywa katika eneo hilo ambapo kwa maelezo ya Mkuu wa Mkoa wa Tadjoura Abdalmalik Mohammed Ziwa hilo limekuwa likitoa chumvi kwa wingi hali inayotokana na uwepo wa Bonde la Ufa ambalo ni ziwa linalotoa chumvi kwa wingi duniani.