News and Events

Hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume,


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.Hitma hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Sita, Mhe. Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd

Hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume,

Viongozi wengine walihudhuria katika hitma hiyo ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, viongozi wa serikali zote mbili na viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge na Wawakilishi, wananchi kutoka sehemu mbali mbali pamoja na Mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar.Hitma hiyo ya kumuombea dua Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pia ni miongoni mwa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ilitanguliwa na Qur-an tukufu, iliyosomwa na Ustadh Sharif Muhidin na kuongozwa na Sheikh Mohammed Kassim Said kutoka Kamisheni ya Mufti na Mali ya Amana.

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Juma Faki Chum alitoa mawaidha na kumuelezea marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na kumuombea MwenyeziMungu ampe makaazi mema Peponi.Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika tarehe 7, Aprili, viongozi hao na wananchi waliohudhuria katika hitma hiyo walimuombea dua, marehemu mzee Abeid Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa afisi hiyo ya CCM Kisiwandui dua iliyoongozwa na viongozi wa dini tofauti akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Kabhi wka upande wa dini ya Kiislamu, Askofu Augostino Shayo kutoka Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar na Kashap Pandra aliyesoma kwa niaba ya Wahindu.

Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu mzee Abeid Amani Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyeweka shada la maua kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia, ni Amiri Jeshi Mkuu Dk. John Pombe Magufuli, Kombo Mzee Kombo aliyeweka shada la maua akiwakilisha wazee.Wengine walioweka shada la maua ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, Balozi Ali Karume aliyewek kwa niaba ya familia ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na Balozi mdogo wa Msumbiji anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Jorge Augusto Menezes aliyewawakilisha Mabalozi wenzake wa hapa nchini.

Aidha, Mama Mwanamwema Shein aliungana na akina mama wengine katika hitma hiyo iliyofanyika katika Afisi hiyo ya CCM Kisiwandui, akiwemo mjane wa marehemu mzee Abeid Karume, Mama Fatma Karume,  Mama Shadya Karume na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Wawakilishini na wananchi kutoka sehemu mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa aliwasisitiza wananchi kuimara umoja na mshikamano sambamba na kuimarisha Mungano uliopo ambao umeasisiwa na viomhozi Wakuu wa Taifa hili akiwemo Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

April 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi leo imetimia miaka 45 tokea utokee msiba huo.