News and Events

kufanyika kwa mashindano ya michezo ya Majeshi ni dalili njema ya kuwepo kwa mikakati katika vikosi


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kufanyika kwa mashindano ya michezo ya Majeshi mwaka huu ni dalili njema ya kuwepo kwa mikakati katika vikosi vya ulinzi na usalama ya kuunga mkono jitihada za Serikali zote mbili katika kuimarisha sekta ya michezo ili kurudisha hadhi ya Tanzania katika medani za michezo Kimataifa.

kufanyika kwa mashindano ya michezo ya Majeshi ni dalili njema ya kuwepo kwa  mikakati katika vikosi

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Michezo ya 17 ya Majeshi iliyoandaliwa na Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMATA) mwaka 2017, ufunguzi uliofanyika huko katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa Watanzania wanatamani sana kuwapata akina Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na Juma Ikangaa wengine kutoka katika vikosi vya ulinzi na usalama au kutoka timu za utraiani zitakazotoa wachezaji watakaoweza kuwakilisha katika michezo ya Kimataifa.

“Tunaamini kuwa wachezaji kama hawa tunao ila kinachokosekana ni jitihada za kuwaibua na kuwaendeleza zaidi jitihada ambazo ndizo zinazohitajika hivi sasa’,alisema Dk. Shein.Aidha, Dk. Shein alisema kuwa pamoja na kupata fursa ya burudani katika mashindano hayo, vile vile kupitia michezo hiyo, wanamichezo wanaoshiriki mashindano hayo hupata kujuana na kupata kujifunza kutoka kwa wenzao.Aliongeza kuwa fursa hiyo huchangia kuongeza idadi ya mashindano ya michezo ya ndani na kupanua zaidi nafasi ya wanamichezo kuweza kujinoa na kujiweka tayari kwa michezo mengine ambayo timu za majeshi huwa zinashiriki.

Dk. Shein alisema kuwa mashindano hayo pia, yanatoa nafasi nzuri kwa maafisa na wapiganaji wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza ushirikiano zaidi baina yao katika masuala mbali mbali.Pamoja na Hayo, Dk. Shein alitoa pongezi maalum kwa viongozi wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) kwa kuirudisha tena michezo hiyo mwaka huu kwani mashindano hayo kwa mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2004.Alisisitiza kuwa ni dhahiri kwamba kusita kwa mashindano hayo kwa kipindi cha miaka 13 kulileta athari, hivyo baada ya kuzibaini athari hizo jitihada zimefanyika na imewezekana kuyaendeleza tena mashindano hayo.

Dk. Shein alieleza kuwa hatua ya kuiendeleza tena michezo hiyo baada ya miaka 13 ya kusita kwake ni hatua muhimu ya kuendeleza sekta ya michezo katika Jamhuri ya Muugano wa Tanzania na ndani ya vikosi hivyo ambavyo vimekuwa vikitoa mchango muhimu kwa maendeleo ya michezo mbali mbali.Kwa maelezo ya Dk. Shein michezo ina umuhimu mkubwa katika jamii hasa katika kuleta amani, upendo, furaha, mshikamano pamoja na afya kwa wanamichezo ambapo pia, kwa hivi sasa michezo ni chachu ya ajira kwa vijana.

Aliongeza kuwa kwa upande wa vyombo vya ulinzi na usalama michezo ina mchango muhimu katika kuimarisha afya, nidhamu na kwa wapiganaji ni kuwa tayari wakati wowote katika kuilinda nchi na kuifanya Tanzania kuendeleza sifa ya kuwa na wapiganaji imara.

Mapema Mwenyekiti wa BAMMATA Bregedia Jenerali Martin Kemwaga ilitumia fursa hiyo kueleza historia ya Baraza hilo tokea kuanzishwa kwake, mafanikio yaliopatikana pamoja na changamoto zilizopo.

Nae Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo alieleza miongoni mwa malengo ya mashindano hayo kwa vikosi hivyo na kuahidi michezo hiyo kuendeleza vuguvugu lake kama ilivyokuwa siku za nyuma ambapo timu za majeshi zilitoa wanamichezo bora huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Zanzibar kwa kupata uwanachama wa CAF.Mashindano hayo yanatarajiwa kufungwa tarehe 25 mwezi huu ambapo jumla ya michezo mitano itashindaniwa ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete kwa wanawake, mpira wa kikapu kwa wanawake na wanaume, mpira wa mikono kwa wanawake na wanaume na mpira wa wavu kwa wanawake na wanaume ambapo kauli mbiu ya mashindano hayo ni “ Michezo ni Kazi na Mshikamano”.

Katika ufunguzi wa mashindano hayo nyimbo maalum kwa ziliimbwa na vikosi hivyo pamoja na viapo kwa wachezaji pamoja na waamuzi huku timu ya mpira wa miguu ya vikosi vya SMZ ikafungua dimba na timu ya Uhamiaji hapo hapo katika uwanja huo wa Amaan mjini Zanzibar ambapo Dk. Shein alizikagua timu hizo na kushiriki pamoja na viongozi wengine, wananchi na vikosi shiriki kuangalia pambano hilo.