News and Events

Maadili mema ya Kiislamu.kufundishwa watoto hapa nchini


VIONGOZI wa dini ya Kiislamu hapa nchini wametakiwa kuendelea kutoa mafunzo kwa jamii hasa kuwafundisha watoto maadili mema ya Kiislamu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo wakati alipokuwa akisalimiana na Masheikh pamoja na vionhozi wa dini ya Kiislamu huko Fumba, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, katika ukumbi wa nyumba za mradi wa Makampuni
ya Said Salim Bakhressa.

Alhaj Dk. Shein ni kawaida yake kila ifikapo siku ya Sikukuu baada ya Sala ya Idd na kabla ya kuanza kwa Baraza la Idd, hukutana na Masheikh mbali mbali wa Dini ya Kiislamu kwa ajili ya kusaliana nao na kuwatakia Idd njema.

Katika maelezo yeke, Alhaj Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao wa dini waliofika katika ukumbi huo kuna umhimu wa kuongeza nguvu katika kuwavundisha watoto maadili mema pamoja na mila na silka za Kizanzibari.

Aidha, Alhaj Dk. Shein alisisitiza kuwa elimu ndio jambo kubwa katika msingi wa maisha ya mwanaadamu hivyo wanapaswa kuilitilia mkazo hasa kwa watoto ili mema wayafuate na mabaya wayaache.

Alieleza kuwa iwapo binaadamu atakosa elimu itakuwa ni vigumu kwake kufuata maarisho ya MwenyeziMungu, hivyo ni vyema suala la elimu kwa upande wa viongozi hao wa dini wakalipa kipaumbele zaidi hasa kwa watoto ambao wanahitajia missing mema.

Alhaj Dk. Shein aliongeza kuwa watoto wanahitaji miongozo pamoja na malezi yalio mema ili waweze kuongokewa katika maisha yao hivyo viongozi wa dini ya Kiislamu wanapaswa kulifanyia kazi jukumu hilo ili watoto wawese kwua na malezi pamoja na maadili na miongozo ya Kiislamu.

“Msichoke kutuelimisha sisi pamoja na watoto wetu hasa watoto wadogo ambao wanahitajia kupewa elimu na mafunzo mema pamoja na kuwafundisha maadili yao ya Kiislamu”,alisema Alhaj Dk. Shein.

Pamoja na hayo,Alhaj Dk. Shein aliwataka viongozi hao wa dini kuendelea kuwaombea dua Waislamu waliotikia wito wa Allah (SW) kwenda Makka Saudi Arabia kwa lengo la kuitekeleza Ibada ya Hijja mwaka huu.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani na pongezi kubwa sana kwa Mewnyekiti wa Makammpuni ya Bakhressa Sheikh Said Salim Bakhresa kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kuujenga mji huo mpya wa Fumba.

Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yaliopatikana na yanayoendelea kupatikana yametokana na Mwenyekiti huyo kuwa na mashirikiano mazuri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi pamoja na wananchi wa Zanzibar.

Katika hafla hiyo fupi mbali ya viongozi mbali mbali wa dini wakiwemo Masheikh wa Wilaya ya Magharibi B, Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji, Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Soraga na Mahseikh wengineo pia viongozi wa Serikali nao walihudhuria.

Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan na viongozi wengineo.