News and Events

Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nchi za nje kutekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nchi za nje kutekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi kwa kuhamasisha uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda ambayo ndio kiu ya uchumi wa Tanzania hivi sasa.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Mabalozi Wateule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliofika Ikulu kumuaga Rais pamoja na kufanya nae mazungumzo ambapo alisisitiza kuwa sekta ya viwanda imepewa kipaumbele na kutiliwa mkazo mkubwa na Serikali zote mbili.

Miongoni mwa Mabalozi hao ni Balozi Emmanuel John Nchimbi ambaye anakwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil, Balozi Mbelwa Brighton Kairuki anaekwenda nchini China, Balozi Geogre Kahema Madafa anaekwenda Italy, Balozi Profesa Elizabeth Kiondo anakwenda nchini Turkey.

Wengine ni Balozi Dk. James Alex Msekela UN nchini Geneva, Balozi Samwel William Shelukindo anaekwenda Paris, France na Balozi mteule Lt. Jeneral (Mstaafu) Paul Ignance Mella anaekwenda D.R. Congo.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa shabaha kuu ya Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vikubwa, vidogo na vya kati hivyo ni vyema wakatumua fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa nchi hizo wanazokwenda kufanyia kazi.

Akizungumzia kwa upande wa Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa licha ya Zanzibar kuwa ni visiwa ambavyo vimezungukwa na bahari sambamba na kuwepo ukanda wa bahari kutoka Tanga hadi Mtwara lakini maeneo hayo hakuna viwanda vya samaki ambayo ni bidhaa inayotokana na bahari.

Alieleza kuwa eneo la bahari la Zanzibar ni maarufu sana kwa samaki aina ya jodari ambaye ni samaki anaependwa duniani lakini wamekuwa hawavuliwi ipasavyo na badala yake hutokea meli kubwa za kigeni za uvuvi ambazo huja kuwavua kwa njia za wizi.

Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya ajira na kupunguza changamoto iliyopo katika sekta hiyo hapa nchini hasa kwa vijana.

Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya Mabalozi hao kuitangaza Zanzibar na Tanzania nzima kiutalii ambapo kwa upande wa Zanzibar sekta hiyo imekuwa ni muhimu kutokana na kuchangia asilimia 80 ya pato la Taifa.

Dk. Shein alieleza kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ifikapo mwaka 2020 ni kupokea watalii zaidi ya laki tano kutokana na mikakati iliyopo hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar inavivutio vingi vya kitalii.

Pia, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuvitangaza vivutio vya kitalii vilivyopo nchini vikiwemo Mbuga za wanyama, sehemu za kihistoria, fukwe na vyenginevyo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwatakia heri na fanaka Mabalozi hao katika utendaji wao wa kazi kwenye Balozi hizo na kueleza kuwa kwa vile anatambua utendaji wao wa kazi ana matumaini makubwa kuwa watatekeleza vyema dhamana zao hizo.

Nao Mabalozi hao walimthibitishia Dk. Shein kuwa wamepokea maelekezo yote aliyowapa na kuahidi kuyafanyia kazi hasa kwa maeneo maaluma ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Akitoa maelezo kwa niaba ya Mabalozi wenziwe, Balozi wa Tanzania nchini Brazil Balozi Emmanuel John Nchimbi, alimuhakikishia Dk. Shein kuwa watafanya kazi kwa juhudi kubwa na maarifa kwa maslahi ya nchi yao na wananchi wake.

Balozi Nchimbi kwa niaba ya wenziwe walitoa pongezi na shukurani kwa kwa Rais Dk. Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kuteuliwa kwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi hizo.

Mabalozi hao walimuhakikishia Dk. Shein kuwa katika wadhifa wao huo juhudi za makusudi watazichukua kwa mashirikiano ya pamoja katika kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo na Tanzania unaimarishwa zaidi sambamba na kuimarisha maslahi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.