News and Events

Maendeleo yaliopatikanwa Pemba yaelezwe kama ilivyoagizwa katika ilani ya CCM 2015 - 2020.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein amewataka viongozi wa CCM kisiwani Pemba kuyaeleza mafanikio yaliyopatikana nchini ambayo yametekelezwa naserikali kama ilivyoagizwa katika Ilani ya CCM 2015 - 2020.

Maendeleo  yaliopatikanwa Pemba yaelezwe  kama ilivyoagizwa katika ilani ya CCM 2015 - 2020.

Dk. Shein ambaye pia,ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Chuo cha Kiislamu Micheweni wakati alipokuwa na mkutano wa ndani kati yake na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kaskazini Pemba na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya za Mkoa huo.Katika maelezo yake, Dk. Shein aliwataka viongozi hao kutembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ile iliyopo kwenye majimbo yao kwani kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao badala ya kusubiri ziara za Rais.

Dk. Shein alisema kuwa iwapo viongozi hao watafanya hivyo watakisaidia chama,watawasaidia viongozi na wananchi pamoja na kumsaidia yeye kwani wana wajibu wa kuangalia miradi hiyo na kuonyesha ni jinsi gani wameridhika ama hawakuridhika na baadae kutoa taarifa.Katika maelezo hayo, Dk. Shein alisema kuwa anachokieleza ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo imeonesha majukumu ya viongozi hao.

Dk. Shein aliwataka viongozi hao kuondosha ukimya na kutokuwa wanyonge kwani wao ndio wenye Serikali na wanapaswa kueleza mafanikio hayo kwa wananchi na kutowaacha watu wengine wakaanza kupotosha ukweli na kujipa tamaa kuwa kuna siku watawabadilisha nia wanaCCM wa Pemba ambao wako imara katika chama chao.Aidha,alieleza kuwa chama cha siasa ndio kinachotafuta dola hivyo ni lazima viongozi hao washirikiane kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuyaimarisha matawi ya chama chao.

Dk. Shein alisema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika kuinua uchumi kwa kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ambapo sasa Serikali inakusanya wastani wa Tsh. Bilioni 50 kwa mwezi kutoka wastani wa Tsh. Bilioni 13.5 kwa mwezi zilizokuwa zikikusanywa wakati alipoingia madarakani mwaka 2010.Dk. Shein alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo la mapato, serikali imepata uwezo wa kuimarisha huduma za jamii zikiwemo elimu, afya, majisafi na salama na amewahakikishia viongozi hao kwamba serikali itatekeleza ahadi yake ya kuongeza kwa asilimia mia (100%) kima cha chini cha mishahara jambo ambalo halijawahi kufanyika duniani kote.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha sekta zake mbali mbali, hivi sasa imo katika mikakati kapambe ya kuhakikisha kuwa sekta ya habari inaimarika na wananchi wanapata habari kupitia Shirika lao la habari la ZBC vizuri na tayari hilo limeanza kuonekana na muda mfupi ujao wananchi wa Unguja na Pemba wataona mabadiliko kutoka matangazo ya ZBC.Katika suala zima la uchaguzi ndani wa chama hicho, Dk. Shein alisema kuwa yeye mwenyewe binafsi pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho Dk. John Pombe Magufuli watahakikisha rushwa haitokuwa na nafasi katika uongozi wa chama hicho mwaka huu, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa atakaegundulika kufanya hivyo.

Aidha, Dk. Shein aliwataka viongozi hao kuweka mbele maslahi ya chama na kujiepusha na makundi na ubinafsi na kusisitiza kuwa watu wanaobainika kuwa na uwezo wa kuongoza na wanachama kujiridhisha, ndio wanaofaa kupewa kuongeza bila ya hila, rushwa au mbinu zozote zisizokubalika katika uchaguzi wa chama hicho mwaka huu.Dk. Shein alisisitiza kuwa ndani ya CCM ni lazima kuwepo viongozi waadilifu kama ilivyokuwa wakati wa uongozi wa ASP na TANU na kueleza kuwa mambo yaliokinyume na maadili hayatovumiliwa ikiwa ni pamoja na kufanya kampeni kabla ya wakati wake.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa CCM ni kuhakikisha inajenga barabara tena kwa kiwango cha lami katika maeneo yote yanayozalisha zao la karafuu, ili iwe rahisi kwa wananchi kusafirisha zao hilo.Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mambo mengi na ni vyema viongozi hao wakayasimamia sambamba na kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2015-2020.