News and Events

Rais Ameenah alifika Ikulu mjini Zanzibar na kufanya mazungumzo na Rais Dk. Shein.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Rais wa Mauritius Dk. Ameenah Gurib Fakim ambapo viongozi hao wameahidi kushirikiana katika sekta mbali mbali za maendeleo kutokana na nchi zao kufanana kimazingira.

Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo Rais Ameenah alifika kwa ajili ya kumsalimia na kufanya mazungumzo na Rais Dk. Shein.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alipongeza ujio wa Rais Ameenah hapa Zanzibar na kueleza kuwa hatua hiyo itazidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Mauritius na Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla.

Dk. Shein alimuhakikishia Rais Ameenah kuwa Zanzibar itaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati yake na Mauritius huku akieleza kuwa Zanzibar ina mambo mengi ya kujifunza kutoka nchini humo hasa katika sekta ya kilimo ambapo nchi hiyo imeimarisha kilimo cha miwa ambacho huzalisha sukari pamoja na kuimarisha viwanda kwa ajili ya bidhaa hiyo.

Alieleza kuwa Mauritius na Zanzibar zina nafasi kubwa ya kuimarisha uhusiano katika sekta ya utalii, sekta ambayo ina umuhimu mkubwa na imeweza kuleta mafanikio na kuimarisha uchumi katika nchi mbili hizo.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa nchi mbili hizo zina nafasi kubwa katika kushirikiana kwenye sekta ya uvuvi sambamba na mambo yote yanayohusiana na uchumi wa bahari.

Alisisitiza kuwa ni vyema nchi mbili hizo zikaendeleza mashirikiana katika masuala ya athari za tabianchi kwa kutekeleza makubaliano mbali mbali ya Kimataifa yakiwemo yaliofikiwa katika mkutano wa tatu wa Kimataifa wa nchi za Visiwa uliofanyika nchini Samoa mnamo Septemba mwaka 2014 ambapo Dk. Shein alishiriki.


Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na maeneo aliyoyabainisha Rais Ameenah katika kuleta ushirikiano hasa katika kilimo cha miwa kwa ajili ya kuzalisha sukari pamoja na tafiti katika sekta hiyo ambayo itapelekea mashirikiano kati ya wataalamu kutoka Mauritius na wataalamu kutoka vyuo vikuu vilivyopo Zanzibar.

Nae Rais wa Mauritius Dk. Ameenah ambaye yupo Zanzibar kwa ajili ya mapumziko, alieleza kuvutiwa kwake na mazingira ya Zanzibar na kusisitiza kuwa kuna haja ya kuimarisha mashirikiano baina ya pande mbili hizo kwani nchi zote zina mazingira yaliofanana.

Rais huyo wa Mauriotius alieleza kuwa Mauritius imekuwa na mashirikiano mazuri ya muda mrefu kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar ambayo yamepekea kuendeleza sekta mbali mbali yakiwemo mashirikiano ya Kimataifa na Jumuiya za nchi za Afrika kama vile Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Dk. Ameenah alieleza kuwa Zanzibar na Mauritius zina nafasi kubwa ya kushirikiana katika sekta ya kilimo, hasa kilimo cha miwa kwa ajili ya kutengeneza sukari pamoja na kuendeleza viwanda vya sukari hasa ikizingatiwa kuwa Mauritius ina uzoefu mkubwa katika sekta hiyo.

Aliongeza kuwa Mauritius imepiga hatua kubwa katika kuendeleza tafiti zinazohusiana na kilimo cha miwa kwa ajili ya kutengenezea sukari hatua ambayo imeweza kuinua sekta hiyo sambamba na kuimarisha viwanda vya sukari.

Pamoja na hayo, Rais Ameenah alisisitiza haja kuimarisha ushirikiano na uhusiano kati ya nchi za bara la Afrika wenyewe kwa wenyewe badala ya kuelekeza nguvu kubwa kwa nchi zilizoendelea pamoja na Jumuiya zake.

Rais Dk. Ameenah alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya utalii, Mauritius iko tayari kushirikiana na Zanzibar kwani nchi hiyo ambayo ni kisiwa kama ilivyo kwa Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa yaliyotokana na utalii.

Sambamba na hayo, viongozi hao pia, walieleza haja ya kushirikiana katika sekta ya usafiri ambayo itapekea kuimarisha zaidi sekta ya utalii na kuwarahisishia watalii kuzitembelea nchi hizo hatua ambayo itazidi kuimarisha uchumi wa nchi mbili hizo.