News and Events

Uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Bodi ya Wakurugenzi ya ZSTC wakutana na Dk.Shein


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Serikali ndani ya Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) ikiwemo kutungwa kwa Sheria yamelipelekea Shirika hilo kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa biashara ya zao la karafuu.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) pamoja na uongozi wake.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Shirika la (ZSTC), kwa mafanikio makubwa iliyoyapata tokea kuanzishwa kwa mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Namba 11 ya mwaka 2011 na ile Sheria ya Maendeleo ya karafuu Namba 2 ya mwaka 2014.
Dk. Shein alieleza kuwa azma ya Serikali ya kurekebisha vituo vya kununua karafuu vya ZSTC sambamba na kuimarisha miundombinu ya barabara kwa maeneo yanayozalisha karafuu kwa wingi ni miongoni mwa hatua muhimu za kuliimarisha zao hilo na kukuza bishara ya karafuu.
Alieleza kuwepo Sheria hizo ndani ya Shirika hilo zitalisaidia katika kufikia lengo la kuimarika kwa biashara ya karafuu pamoja na biashara nyenginezo ambazo zina maslahi na wananchi huku wananchi na wauzaji wa karafuu nao wakiendelea kufaidika.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya kuimarishwa mashirikiano kati ya Bodi, Uongozi na Waziri ili Shirika hilo lizidi kuimarika sambamba na kuendelea na kasi yake ya utendaji huku akieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwaenzi wakulima wa karafuu kwa kutambua kuwa biashara hio sio hasara bali ni faida.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa ndani ya (ZSTC) mapato yanaonekana na Shirika linakopesheka kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata hivyo liendelee na kasi yake kwani uongozi wa Bodi na Wizara uliopo una weza kuleta mabadiliko na maendeleo makubwa.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliutaka uongozi wa (ZSTC) kutambua kuwa maghala yote ya Shirika hilo yaliopo Unguja na Pemba ni mali yao hivyo ni lazima wayasimamie vyema na kuyatunza kwani sheria imewaruhusu.
Nae Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, alitoa pongezi kwa Shirika hilo kwan kuendelea kufanya vizuri na kueleza haja ya kuendelea kufanya vizuri kwani ni shirika la zamani na lina historia yake.
Waziri wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali alisema kuwa Shirika hilo ni miongoni mwa mashirika yaliopata mafanikio makubwa nchini Tanzania ambalo halijawahi kupata misuko suko hatua ambayo imetokana na miongozo mizuri ya Rais Dk. Shein.
Balozi Amina alieleza kuwa masoko ya bidhaa zinazozalishwa na ZSTC yapo hata nje ya nchi na kusisitiza haja ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa kuwashirikisha wakulima pamoja na vijana kulima mazao ya biashara yakiwemo viungo huku akieleza uwezekano wa kuzalisha asali, mbazi na dengu badala ya karafuu peke yake.
Aidha uongozi wa ZSTC ulieleza changamoto zilizopo sambamba na mafanikio yaliopatikana huku ukieleza hatua zilizopatikana za mafanikio kwa kupata mununuzi wa bidhaa za kwianda cha makonyo kutoka nchini China ambaye ameahidi kunua bidhaa hizo tani 40 kila mwezi.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza haja ya kukiangalia kwa mtazamo wa uzalishaji wenye tija kiwanda cha makonyo kilichopo Wawi kwa kukifanyia ukarabati ama kukijenga upya ikiwa ni pamoja na kuweka mashine za kisasa kwa lengo la kuweza kuzalisha bidhaa kwa wingi.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) Kassim Maalim Suleiman, alieleza kuwa Shirika hilo bado linaenda vizuri na limeweza kupata mafanikio makubwa licha ya changamoto zilizokuwepo.
Mwenyekiti huyo alisifu mashirikiano makubwa yaliopo kati ya Bodi na uongozi wa Wizara huku akieleza miongoni mwa mafanikio yaliopatikana ikiwa ni pamoja na kuwa na hakiba ya TZS Bilioni 5.2 kuanzia Julai mwaka 2016 hadi Machi 2017.
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema kwa mwaka huo wa 2016 hadi 2017 Shirika limeuza karafuu tani 2156 zenye thamani ya TZS Bilioni 36.6 huku akieleza haja ya kutotegemea zao loa karafuu peke na badala yake kutafuta mazao mengine ambayo yatalipunguzia mzigo zao hilo.