Publications

Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk,Shein katika kilele cha mei mosi.


Mheshimiwa Waziri wa Nchi (OR) Kazi na
Utumishi wa Umma,

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Huru vya
Wafanyakazi Zanzibar,

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba,

Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri mliohudhuria,

Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi,

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya
Wafanyakazi Zanzibar,

Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO),

Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya wa Waajiri Zanzibar,

Viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali,

Ndugu Wafanyakazi,

Mabibi na Mabwana,

Assalamu Aleikum,

Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu; Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uhai na uzima tukaweza kukusanyika kwa wingi katika Ukumbi huu wa ZSTC, Wawi, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani - May Day.

Napenda nitoe shukurani zangu za dhati kwa viongozi na watendaji wa Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizi na kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi.  Mwaliko wenu ni kielelezo cha uhusiano mzuri uliopo baina ya wafanyakazi na Serikali na jinsi mnavyounga mkono mambo ambayo Serikali imeyatekeleza kwa ajili ya maendeleo na manufaa ya wafanyakazi na wananchi wote kwa jumla.
 
Kwa hakika, sherehe hizi za leo ni muhimu na zinanipa furaha kubwa kwa kuwa pamoja nanyi wafanyakazi wenzangu, wakati tunaungana na wafanyakazi wengine duniani kote katika kusherehekea sikukuu hio ya wafanyakazi.  Ni dhahiri kwamba sherehe hizi zimefana sana. Natoa pongezi kwa wafanyakazi walioshiriki katika maandamano pamoja na msoma utenzi na vikundi vya burudani kwa kutupa ujumbe wenye mnasaba na siku hii ya leo.  Ahsanteni na Hongereni sana.

Ndugu Wafanyakazi,
Napenda niwapongeze kwa dhati viongozi wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi kwa uwamuzi wao wa busara wa kuamua maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani kwa mwaka huu yafanyike hapa Pemba.  Hatua hii inawapa nafasi wafanyakazi waliopo Pemba kushiriki kwa wingi katika sherehe hizi na kuwapa fursa ya kuonesha mshikamano wao kwa vitendo katika siku hii maalum ya wafanyakazi duniani kote.

Naupongeza uongozi wa Mkoa wa Kusini Pemba, hasa Mheshimiwa Mwanajuma Majid, Mkuu wa Mkoa huu, viongozi wengine wote,  wafanyakazi pamoja na wananchi wote wa Mkoa huu kwa kukubali kuwa wenyeji wa sherehe hizi.  Nakupongezeni kwa kuzifanikisha sherehe hizi. Nasema hongereni sana.

Kadhalika, natoa pongezi kwa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi, Zanzibar (ZATUC) kwa kushirikiana vizuri na Serikali kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma na kwa kazi nzuri mnayoifanya katika kutekeleza majukumu yenu.  Ushirikiano mzuri uliopo baina ya ZATUC na SMZ imepelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itekeleza kwa mafanikio makubwa sera za kazi ilizojiwekea. Vile vile, Serikali imefanikiwa kunyanyua maslahi ya wafanyakazi mara kadhaa katika kipindi hiki cha miaka mitano.  Kila mmoja wenu ni shahidi wa mafanikio hayo.

Nachukua fursa hii kutoa pongezi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman pamoja na watendaji wa Wizara hiyo kwa kazi nzuri ya kuratibu na kuweka uhusiano mzuri kati ya Serikali, wafanyakazi na waajiri; na kwa kusimamia ipasavyo Sera na Sheria mbali mbali zinazohusu kazi na ajira.

Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini namna inavyoshirikiana na shirikisho hili pamoja na vyama vyote vya wafanyakazi wa sekta mbali mbali.  Kwa mara nyengine, napenda nikuhakikishieni kuwa Serikali ninayoiongoza inazingatia sana umuhimu wa uhusiano huu na siku zote itakuwa tayari kushirikiana nanyi kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wafanyakazi wote Unguja na Pemba. Wahenga wamesema “ Umoja ni nguvu”.

Ndugu Wafanyakazi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa awamu zote inatambua kwamba wafanyakazi ni miongoni mwa nguzo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.  Wafanyakazi tuna mchango muhimu katika uzalishaji mali na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.  Kwa hivyo, ni dhahiri kuwa wafanyakazi wa sekta mbali mbali za umma na sekta binafsi ni tegemeo la Serikali katika kupata maendeleo ya haraka na ustawi wa jamii.

Kwa kutambua mchango wa wafanyakazi kwa maendeleo ya nchi na maendeleo ya wafanyakazi wenyewe, Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume aliwahi kuwaambia wafanyakazi; maelezo yafuatayo:- Nanukuu.
“Tunataka maisha ya wafanyakazi yawe ya juu na ya kujitegemea wenyewe.  Tunajua kwamba hayo yote yatatekelezwa na wafanyakazi wenyewe, kwani ndio azma yao.  Kabla ya Mapinduzi hatukuwa na uwezo wa kufanya hivyo, lakini sasa tunao”. 
Mwisho wa kunukuu.

Kwa kuzingatia msingi huu, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuwajengea mazingira mazuri wafanyakazi ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 -2015, Dira ya Maendeleo 2020 na Mipango mengine ya Maendeleo.  Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha maslahi, kuimarisha utendaji kwa kuwapatia vifaa vya kazi, mafunzo, afya na usalama, kutunga sera, sheria na kanuni za utumishi bora pamoja na kukuza ushirikiano na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi.  Ni jambo la faraja kuona kwamba tumeweza kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa malengo hayo ya Serikali katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba.

Ndugu Wafanyakazi,
Miongoni mwa mafanikio tuliyoyapata ni kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kupandisha mishahara ya watumishi wa umma kutoka kima cha chini cha mshahara wa Tsh.100,000 hadi Tsh.125,000 kwa mwezi sawa na asilimia ishirini na tano (25%) pamoja na kufanya marekebisho ya mishahara ya wataalamu mbalimbali wakiwemo Madaktari, Walimu wa Sayansi nakadhalika. Tulifanya marekebisho hayo ya mwanzo katika mwaka 2011.  Vile vile, mwishoni mwa mwaka 2013 na mwanazoni mwa mwaka 2014, Serikali ilipandisha kima cha chini cha mshahara kutoka Tsh.125,000 hadi Tsh. 150,000 sawa na asilimia ishirini (20%) pamoja na kurekebisha mishahara ya watumishi wazoefu, waliotumikia utumishi wa umma kwa miaka kumi na tano (15) na zaidi ambao wana mishahara kati ya Tsh.150,000 hadi Tsh.225,000.

Kadhalika, katika jitihada za kunyanyua kipato cha mfanyakazi, Serikali imeidhinisha posho ambazo tayari zimeanza kutolewa kwa Makatibu Muhtasi na Madereva wa viongozi, Mahakimu wa Mahkama za Mwanzo, Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Waendesha Mashtaka wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.  Vile vile, Serikali   inatoa posho kwa Matarishi na Wakuu wa Masjala za Siri, Walimu Wakuu na Wakuu wa Vitengo,Walezi na Wahudumu wa nyumba za kulelea wazee na watoto yatima na watumishi wa Mamlaka mbali mbali za Serikali.  Aidha, Madaktari Bingwa na Wasaidizi wao katika kada ya Afya wanapatiwa posho la “On call ” na posho kwa wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu.

Kadhalika, Serikali imefanya marekebisho ya mishahara kwa Walimu wenye kiwango cha Elimu ya Stashahada ya kawaida (Ordinary Diploma) na wenye uzoefu wa miaka 15 na kuendelea.

Miongoni mwa hatua za msingi zilizochukuliwa katika kuimarisha utendaji kazi, ni kuanzisha Miundo ya Utumishi katika Mawizara na Taasisi mbali mbali za Serikali. Katika kipindi hiki cha miaka mitano, Wizara zote tayari zimeshatengeneza miundo yao ya utumishi na kuipitisha katika Kamisheni ya Utumishi wa Umma kwa uthibitisho. Hatua iliyopo hivi sasa ni kupangwa kwa watumishi wa Wizara hizo katika Miundo ya Utumishi iliyotayarishwa. Hata hivyo, taasisi nyengine za Serikali yakiwemo mashirika na taasisi zinazojitegemea zimo katika hatua za utayarishaji wa Miundo yao ya Utumishi kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma.

Hatua hizo zote zimechukuliwa kwa lengo la kukupunguzieni wafanyakazi nyote ukali wa maisha,  kuongeza ufanisi katika Utumishi wa Umma na uadilifu wenu katika kazi. Serikali imekusudia kuwa suala hili liwe endelevu kutegemea hali ya uchumi wetu pamoja na ukusanyaji wa mapato.

Ndugu Wafanyakazi,
Katika utekelezaji wa hatua za utoaji maslahi kwa wafanyakazi, pamejitokeza baadhi ya kasoro za kiutendaji. Napenda nikuhakikishieni wafanyakazi nyote, kuwa Serikali itaendelea kuzifanyia kazi kasoro zote zilizojitokeza wakati wa kufanya marekebisho ya mishahara na maposho mbali mbali.  Hakuna mfanyakazi atakayedhulumiwa haki yake.  Naelewa kuwepo kwa tatizo kwenye Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali hasa kuhusiana na malimbikizo katika mishahara baada ya kufanyiwa marekebisho.

Serikali inaendelea kuyahakiki malimbikizo hayo na tayari tumeshafanya uamuzi wa kuyalipa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016.  Nasaha zangu kwa walimu na wafanyakazi wote wenye matatizo kama hayo wawe na subira na moyo wa kuendelea kuchapa kazi wakati masuala yao yanashughulikiwa.  Wahenga walisema. “Subira huvuta kheri”.  Kwa hivyo, wanaohusika waendelee kuwa na subira.

Ndugu Wafanyakazi,
Katika jitihada zinazoendelea kuchukuliwa za kulinda maslahi ya wafanyakazi walioajiriwa katika sekta binafsi,  Serikali imeitaka sekta binafsi nayo kuongeza mishahara na posho za wafanyakazi wao.  Wafanyakazi wa sekta hiyo wameongezewa kiwango cha mishahara yao kutoka Tsh. 70,000 mwaka 2010 hadi 145,000 kwa sasa, sawa na ongezeko la asilimia 107.  Vile vile, waajiri wengi wametekeleza, agizo la Serikali la kuwapa maposho wafanyakazi wao kwa kuzingatia aina ya kazi na uzoefu wao kazini.

Napenda kuitumia fursa hii kwa kuwapongeza waajiri binafsi waliotekeleza agizo hili la Serikali.  Ni vyema na wale ambao bado hawajachukua hatua, wazingatie umuhimu wa jambo hilo.  Kadhalika, nasisitiza umuhimu wa kuwapa mikataba wafanyakazi wenu, kupeleka michango yao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) kwa wakati pamoja na kuwapa haki nyengine kwa mujibu wa sheria za kazi na kanuni za Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi.

Ndugu Wafanyakazi,
Kwa upande wa sheria za kazi,  inafurahisha kuona hivi sasa tumefikia hatua nzuri katika kuimarisha masuala mengi ya kiutendaji katika taasisi zetu na tumeweza kuimarisha haki na maslahi ya wafanyakazi kutokana na Kutungwa kwa Sheria Namba 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011. Sheria hii imetuwezesha kuweka miundo imara ya uendeshaji na usimamizi wa utumishi wa Umma na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Aidha, kutokana na sheria hii, tumeweza kuunda Kamisheni ya Utumishi wa Umma pamoja na Tume ya Utumishi Serikalini, Tume ya Utumishi ya Mahakama, Tume ya Utumishi ya Baraza la Wawakilishi na Tume ya Utumishi ya Idara Maalum. Taasisi hizi ni muhimu katika kulinda maslahi na haki za wafanyakazi hapa nchini na zimetoa mchango mkubwa katika kuweka misingi mikuu ya maadili ya Utumishi wa Umma na usimamizi wa rasilimali watu.

Vile vile, katika kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, jumla ya Kanuni 12 za Sheria za kazi zimetungwa na zimeanza kutumika. Kanuni hizo ni za Sheria ya Ajira Nambari 11, Sheria ya Mahusiano Kazini Nambari 1 zote za mwaka 2005 na Kanuni za mwaka 2014 za Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari 2 ya mwaka 2011.

Nasaha zangu kwa wafanyakazi wote nchini ni kwamba muendelee kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za kazi zinavyotuelekeza.  Natoa wito kwenu muendelee kuongeza kasi na ari ya kujituma, muipende kazi, muyazingatie maadili ya kazi wakati wote na muwe watiifu na waadilifu katika kuwatumikia wananchi na kutekeleza dhamana mlizopewa kwa ustadi na uaminifu wa hali ya juu.

Ndugu Wafanyakazi,
Napenda nikuelezeeni habari njema kwa akina mama wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ( ZSSF),  ambapo siku kumi tu zilizopita, tarehe 21 Aprili, 2015 nilialikwa katika kufungua Mkutano wao pamoja na kuzindua mfumo mpya wa kulipa mafao ya uzazi kwa kina mama wanaokwenda kujifungua. Kuanzia sasa, kina mama wanaokwenda kujifungua ambao ni wanachama wa ZSFF watapewa mafao ya uzazi ili liwasaidie kuimarisha afya zao na za watoto katika kipindi hicho muhimu. Nilifahamishwa kwamba malipo ya mafao ya uzazi hayaathiri malipo ya mafao, ambayo muhusika atapata wakati atakapostaafu. Nachukua fursa hii kuipongeza ZSSF kwa uamuzi huo wa busara.  Vile vile, nilizindua Mfuko wa kuchangia kwa hiari katika Hifadhi ya Jamii.  Hii ni fursa kwa watu wanaojiajiri wenyewe kujiunga na Mfuko wa ZSSF na kufaidi mafao hayo.  Hatua hizo zote zimelenga katika kumnufaisha mfanyakazi, kumpunguzia ukali wa maisha na kumuwezesha aishi vizuri wakati atakapomaliza utumishi wake Serikalini au katika sekta binafsi.
 
Ndugu Wafanyakazi,
Miongoni mwa mafanikio tunayojivunia ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Saba ni kuimarika kwa utaratibu wa majadiliano ya pamoja katika sehemu za kazi.  Ni dhahiri kuwa hali hii imesaidia sana kuondoa migogoro na manung’uniko miongoni mwa wafanyakazi dhidi ya viongozi wao makazini.

Kuimarika kwa vyombo vya majadiliano kati ya waajiri na wafanyakazi katika sehemu za kazi ni hatua muhimu katika kuwashirikisha wafanyakazi kwa lengo la kukuza demokrasia, kuimarisha amani na utulivu kazini na kuongeza ufanisi. Serikali itaendelea kuwashirikisha wafanyakazi katika mambo yanayowahusu kupitia vyombo mbali mbali vya Utatu.  Napenda nitoe wito kwa wawakilishi wa Kamati za UTATU (zenye kujumuisha mwajiri, wawakilishi wa wafanyakazi kupitia Shirikisho la Wafanyakazi na Wajumbe kutoka Serikalini) kuitumia ipasavyo fursa hiyo.  Ni vyema kwa wawakilishi hawa wa wafanyakazi wawasilishe hoja zenye maslahi na wafanyakazi na nchi yetu,  kwa lengo la kuzijadili kwa pamoja na kuzipatia ufumbuzi kwa maslahi ya wafanyakazi na nchi yetu.    Kwa hakika majadiliano ndiyo njia nzuri na ya peke yake ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazotukabili.

Ndugu Wafanyakazi,
Kwa madhumuni ya kuimarisha afya na usalama kazini, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya Usalama na Afya Kazini ili kuweka mfumo mzuri wa afya katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuwakinga wafanyakazi na ajali na majanga mengine yanayotokea katika sehemu za kazi.  Natumia fursa hii kutoa rai kwa wakuu wa taasisi za umma na binafsi kuzingatia suala hili la usalama na afya kazini kwa kuchukua hatua zinazofaa kwa kushirikiana na Idara ya Usalama na Afya Kazini.  Afya na Usalama wa wafanyakazi katika sehemu ya kazi ni jambo la msingi kwa ustawi wa wafanyakazi na waajiri.

Aidha, Serikali ipo katika hatua za kuanzisha Bima ya Afya.  Tumeshafikia hatua nzuri katika kuifikia azma hiyo.  Kuanza kwa huduma hiyo, kutapunguza usumbufu wanaoupata wafanyakazi katika kupata huduma za afya; wao na familia zao.

Sambamba na hatua hiyo, natoa wito kwa wafanyakazi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao, angalau mwaka mara moja, hili ni jambo la msingi kwa afya zetu.  Ni dhahiri kuwa hatua hii inasaidia kujifahamu na kuchukua hatua za kuukabili ugonjwa utakaogundulika tangu mapema, kabla hali haijawa mbaya zaidi.  Vile vile, ni jambo la busara kwa wafanyakazi kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi kwa lengo la kuziimarisha afya zetu.  Michezo na mazoezi ya aina mbali mbali yanasaidia sana kuimarisha afya za miili yetu. Natoa pongezi kwa wafanyakazi na taasisi ambazo zinazingatia umuhimu wa michezo kwa wafanyakazi wao. Hongereni sana.

Ndugu Wafanyakazi,
Nimefurahi kuona kwamba juhudi zilizochukuliwa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ya kuanzisha Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara zetu zote, zimeanza kuzaa matunda mazuri kwa kuwa tumeshuhudia kuwa baadhi ya Wizara zimeongeza kasi ya kufanya utafiti katika mambo yanayohusu sekta zao.  Ni muhimu tukafahamu kuwa utafiti na maendeleo ni mithili ya pete na chanda. Nchi zilizopiga hatua za maendeleo kwa haraka ni zile zilizoweka kipaumbele katika kuimarisha na kuwekeza kwenye shughuli za utafiti. Napenda kutumia fursa hii kuzihimiza Wizara na taasisi zilizopo nchini kuongeza kasi ya kufanya utafiti na kuyatumia matokeo ya tafiti zinazofanywa katika sekta mbali mbali kwa manufaa ya nchi yetu. Idara zinazohusika zihakikishe kwamba zinakuwa na wataalamu wenye uwezo wa kufanya utafiti na kubuni njia zitakazoweza kurahisisha utendaji kazi na kuongeza tija na ufanisi kwenye Mawizara, Kampuni, Taasisi na Mashirika.

Ndugu Wafanyakazi,
Ni jambo la kawaida katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani kuzungumzia hali ya tatizo la ajira nchini.  Zanzibar kama ilivyo kwa nchi mbali mbali duniani inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.  Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya (HBS) wa mwaka 2010, tatizo la ajira limefikia asilimia 17.

Katika kuhakikisha kuwa vijana wanapata fursa za ajira, Serikali imechukua hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuzindua Mpango Mkakati wa Ajira kwa vijana wa mwaka 2014/2018.  Mpango huu umeweka vipaumbele katika sekta za ujasiriamali, elimu ya amali pamoja na ufundi stadi.  Kadhalika, Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Ajira kwa vijana ambapo vipaumbele vimewekwa katika sekta ya kilimo kupitia mashamba darasa, shughuli za uvuvi, ufugaji na utalii.  Nawashajihisha vijana kuzitumia fursa zilizopo kupitia Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma ili waweze kujiajiri wenyewe.

Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, Serikali imewezesha kupatikana kwa nafasi za ajira 25,019, Serikalini na katika sekta binafsi. Kati ya hizo, nafasi za ajira 4,850 zilikuwa za taasisi mbali mbali za Serikali na nafasi za ajira 20,169 zilitokana na sekta binafsi, zikijumuisha ajira za nje ya nchi na taasisi zinazojitegemea.  Nafasi hizo ambazo zimetolewa kwa wananchi wa Zanzibar wenye sifa zilizohitajika, zitawasaidia wananchi hao kujipatia kipato na kutoa mchango wao katika maendeleo ya Zanzibar.

Ndugu Wafanyakazi,
Katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira na kuwajengea uwezo wa kipato wananchi, Serikali imeanzisha mifuko mbali mbali ukiwemo Mfuko wa Uwezeshaji uliozinduliwa tarehe 21 Disemba, 2013. Lengo kuu la kuanzishwa kwa mfuko huu ni kuwapatia mitaji wananchi wakiwemo vijana ili waweze kujiajiri wenyewe.  Vile vile, tumeanzisha Mfuko wa Vijana ili kuwasaidia vijana katika shughuli zao za kujiendeleza kiuchumi.

Napenda niwaase vijana kwamba wasichague kazi.  Kazi ni kazi, lililo muhimu ni kuwa kazi iwe ya halali. Uwezo wa kuajiri Serikalini hauwendani na idadi ya vijana wanaotafuta ajira katika Serikali.  Lazima vijana waizingatie hali hiyo na wachukue hatua za kuwa wabunifu na kujiajiri katika nyanja mbali mbali za ujasiriamali. Serikali imeweka mazingira mazuri na fursa mbali mbali za kuwawezesha vijana kujiajiri wenyewe. Zitumieni fursa hizo kikamilifu.

Ndugu Wafanyakazi,
Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar, kwa niaba ya wafanyakazi wote kwa ushirikiano na mchango wenu muhimu katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na amani.  Ni dhahiri kuwa bila ya amani tusingeweza kufikia mafanikio tuliyokwisha kuyapata.

Wito wangu kwenu na kwa wananchi wote ni kuendelea kusimamia amani, umoja na mshikamano wetu hasa katika wakati huu ambao nchi yetu inaelekea katika mambo mawili muhimu; Kura ya Maoni katika tarehe itakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.  Kushiriki katika chaguzi hizi ni haki ya kikatiba kwa kila mwananchi aliyetimiza sifa.  Halitakuwa jambo jema utaratibu huu wa kidemokrasia ukawa ni chanzo cha kuvuruga amani, umoja na mshikamano wetu.  Nawanasihi wananchi wayaendeleze mafanikio yetu katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano.  Tuendeleze mapenzi baina yetu na kusaidiana katika kupatikana mustakbali mzuri wa Zanzibar. Serikali zote mbili zimeshaanza kuchukua hatua ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapiga kura kwa amani, uhuru na haki.

Ndugu Wafanyakazi,
Kabla sijamaliza hotuba yangu, napenda kulipongeza Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (ZATUC) kwa kuwasilisha risala nzuri ambayo imeonesha mafanikio tuliyoyapata pamoja na changamoto ziliopo mbele yetu. Nimezisikiliza kwa makini changamoto zinazotukabili na nina imani kuwa tuna uwezo wa kuzitolea ufafanuzi changamoto hizo, hasa tukizingatia kwamba nyingi kati ya changamoto hizo zinagusa masuala ya utendaji katika ngazi ya Wizara.  Wahusika wa Wizara zote wapo hapa na bila ya shaka watakuwa wamezisikia. 

Napenda nianze kwa kuzitolea maelezo hoja tatu, ambazo nahisi zinahusu masuala ya utendaji na uendeshaji wa Wizara na taasisi zinazohusika. Hoja hizo ni; (1) Kutoshirikishwa kwa wawakilishi wa Wafanyakazi katika vikao vya Kamati za Uongozi, (2) kutofanyika kwa vikao vya Kamati ya Uongozi vya baadhi ya mawizara na taasisi pamoja na (3) Kuchelewa kulipwa kwa madai ya wafanyakazi yakiwemo ya likizo na malipo ya baada ya saa za kazi (overtime).

Napenda tufahamu kwamba malalamiko ya ushirikishwaji mdogo wa wawakilishi wa wafanyakazi katika vikao vya Kamati za Uongozi pamoja na kutofanyika kwa vikao vya Kamati za uongozi katika baadhi ya taasisi, haya ni masuala ya uongozi na uendeshaji ya Wizara na taasisi zinazohusika. Nina hakika kwamba ziko baadhi ya taasisi ambazo zinafanya vizuri juu ya hili. Kwa hivyo, kwa zile Wizara na taasisi ambazo ushirikishwaji wa wawakilishi wa wafanyakazi bado hawajautekeleza zinapaswa zichukue hatua madhubuti zinazohakikisha kuwa wafanyakazi wanashirikishwa kwa mujibu wa sheria zinazohusika.

Aidha, kuhusu ucheleweshaji wa kulipa madai ya wafanyakazi yakiwemo malipo ya likizo na malipo ya baada ya saa za kazi “overtime”, tatizo hili nalo ni la kiuongozi ambalo ufumbuzi wake hauna budi kutokea ndani ya Wizara au taasisi zinazohusika.  Hata hivyo, katika hotuba yangu hii nimeshatoa maelezo kuhusu juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuwalipa wafanyakazi malimbikizo yaliyopo hasa wafanyakazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ambako bado tatizo hili linaonekana kuwa ni kubwa. Nachukua fursa hii kwa mara nyengine tena kuagiza kwamba kila Wizara ihakikishe inafanya jitihada za kutatua tatizo hili la mrundikano wa malipo. Wito wangu kwa wafanyakazi wote wanaodai malimbikizo mbali mbali ni kuendelea kuwa na subira katika wakati huu ambao Wizara zinatekeleza maagizo yaliyokwishapitishwa na Serikali ya kulipa malimbikizo hayo.

Kuhusu hoja ya kukatwa kwa kodi katika viinua mgongo na pencheni za wastaafu ni kuwa Serikali haitozi kodi katika mafao hayo. Kwa upande wa hoja ya ukubwa wa kodi wanayokatwa wafanyakazi katika mishahara yao (income tax), napenda kuelezea kwamba kila nchi ina utaratibu wake wa kutoza kodi.  Kwa sasa, kwa utaratibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kima cha chini cha mshahara ambacho ni T.Shs. 150,000 hakikatwi kodi. Kadhalika, iwapo mishahara itarekebishwa wafanyakazi wanaopokea kima cha chini hawatotozwa kodi kufuatana na utaratibu tulionao.

Kuhusu suala la kuchelewa kuundwa chombo cha majadiliano, nimeelezwa kwamba hatua za awali za uundaji wa chombo hiki muhimu zimeshachukuliwa kama inayoelekezwa katika kifungu cha 80 (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari 2 ya mwaka 2011.  Kanuni za kuanzishwa kwa chombo hicho na taratibu nyengine za uendeshaji zimeshatungwa.  Hii ni hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya kuunda chombo hicho.

Kuhusu hoja ya kucheleweshwa kwa uundwaji wa Idara ya Fidia, hilo ni suala la kisheria.  Kwa msingi huo, utekelezaji wake unahitaji kupitia katika taratibu kadhaa za kiutendaji na hatimae kufikishwa katika Serikali kuu kwa uamuzi wa mwisho. Hivyo,  Serikali inaendelea na hatua za kufanya tathmini ya uundwaji wa chombo hicho kwa mujibu wa sheria zilizopo. Hata hivyo, kwa sasa shughuli zinazohusu masuala ya fidia katika sekta ya umma hazijasita ambapo zinafanywa kwa taratibu zilizopo kupitia wizara zinazohusika. 

Ndugu Wafanyakazi,
Namalizia hotuba yangu kwa kukushukuruni kwa mwaliko wenu pamoja na mahudhurio yenu makubwa katika sherehe hizi.  Kadhalika, natoa shukurani maalum kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kupitia Ofisi yake ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuzipa Serikali zetu.  Tunathamini sana misaada yenu ya kifedha na kitaalamu katika kuendeleza sekta ya kazi.  Tunaahidi kwamba tutaendelea kushirikiana na ZATUC pamoja na wafanyakazi wetu,  ili kuongeza ufanisi.

Nakutakieni kila la kheri katika siku hii ya wafanyakazi na utekelezaji mwema wa kazi zenu.  Mwenyezi Mungu atupe kila la kheri na uwezo wa kutekeleza mipango yote ya maendeleo kwa manufaa ya kila mmoja wetu na nchi yetu.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.