HOTUBA YA MHESHIMIWA DR. HUSSEIN ALI MWINYI, RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KATIKA SHEREHE YA UWEKAJI JIWE LA MSINGI, JENGO LA OFISI YA UHAMIAJI MKOA WA MJINI MAGHARIBI
TAREHE 19 APRILI, 2024.


Mheshimiwa Hamza Hassan Juma; 
Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais,

Mheshimiwa Mhandisi Hamad Yussuf Masauni; 
Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,

Mhandisi Zena Ahmed Said; 
Katibu Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,

Dkt. Mohammed Said Mohamed (Dimwa) 
Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar,

Dkt. Anna Peter Makakala; 
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania,

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Zanzibar,

Mheshimiwa Idriss Kitwana Mustafa; 
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,

Dkt. Islam Seif; Katibu Mkuu, 
Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais,

Ndugu, Ally Senga Gugu, Katibu Mkuu, 
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,

Ndugu, Hassan Ali Hassan, 
Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar na Makamishna wengine mliopo,

Mheshimiwa Mahmoud Mohammed Mussa, 
Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar,

Ndugu Viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali mliopo,

Viongozi wa Dini mliopo,

Ndugu Waandishi wa Habari  na Wasanii wetu
wa ngoma ya kibati na utenzi,

Ndugu Wananchi na Wageni waalikwa mliohudhuria,

Mabibi na Mabwana.

ASSALLAAM ALAYKUM,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma kwa kutujaalia uhai na afya njema na kuutuwezesha kuhudhuria Sherehe hizi za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la Afisi ya Uhamiaji Katika Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 26 Aprili, 1964, viongozi wetu Waasisi Hayati Mwalim Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee, Abeid Amani Karume waliziunganisha Nchi zetu za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika, kuzaliwa kwa Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo siku chache zijazo, Watanzania kwa Umoja wetu tutaadhimisha siku hiyo muhimu katika historia ya nchi yetu.

Nachukua fursa hii kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa mafanikio makubwa ambayo tumeyapata katika sekta zote za maendeleo Katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nawashukuru Viongozi wetu wa Awamu mbali mbali Katika Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamia, kudumisha na kuimarisha Muungano wetu kwa faida ya pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa dhati kabisa nimpongeze Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa dhamira yake ya dhati ya kuimarisha shughuli na Taasisi zote za Muungano ziliopo hapa Zanzibar, zikiwemo Idara ya Uhamiaji kwa uimarishaji wa miundombinu ya kisasa, vitendea kazi, Majengo mazuri na Mifumo ya Kielektroniki katika kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wananchi na Wageni.

Ndugu Wananchi na Wageni waalikwa, 
Leo tupo hapa kushuhudia uwekaji wa Jiwe la Msingi la Jengo la Ghorofa tano la Afisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi. Ni dhahiri kuwa jengo hili litakapokamilika, litaongeza Ari na Kasi ya Utoaji wa Huduma za Uhamiaji katika Mkoa huu wa Mjini Magharibi na Manispaa zake zote tatu.

Katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano tumeshuhudia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Idara ya Uhamiaji ikipiga hatua kubwa  za mafankio ikiwemo hii ya kuimarisha miundombinu ya Utoaji huduma ambapo imeweza kujenga Ofisi za Kisasa katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba, sambamba na baadhi ya Wilaya Unguja na Pemba. Haya ni miongoni mwa matunda ya Muungano wetu ambayo wananchi wa Zanzibar tunanufaika nayo kupitia Muungano wetu. Tunashukuru sana.

Ndugu Wananchi na Wageni waalikwa,

Leo sote hapa ni Mashahidi wa mafanikio hayo baada ya kuweka  Jiwe La Msingi la Jengo la kisasa la Afisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi. Ni haki yetu kujipongeza na kuzipongeza Serikali zetu mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa katika kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma bora kupitia nyanja zote za Kiuchumi na Kijamii. Kwa msingi huo ni wajibu wetu sote kuulinda, kuumirasha, kuuendeleza na kuudumisha Muungano wetu kwa dhamira ile ile ya Waasisi wa Taifa letu ili ulete mafanikio zaidi kwa sisi tuliopo sasa na wale watakaokuja baadae. 

Nitumie fursa hii kumpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, kwa hatua mbalimbali ambazo amekuwa akizichukua katika kuendelea kuimarisha huduma zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji kwa pande zote mbili za Muungano. Mara kadhaa nimekuwa nikishuhudia akifanya ziara katika maeneo muhimu ya kuingia nchini ukiwemo Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Abeid Amani Karume.  

Kwa hakika, huduma za uhamiaji katika Mkoa huu, wa Mjini Magharibi zinahitajika kuwekewa mazingatio maalum ya kuimarishwa kwake. Katika Mkoa huu, kuna Vituo vya Uingiaji na Utokaji wa Watu Nchini ikiwemo, Bandari ya Malindi ambayo kwa mwaka imekua ikipokea zaidi ya Watalii wa Kimataifa 20,000 na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ambao pia umekua ukipokea zaidi ya Watalii 500,000 kwa mwaka. Hivyo, ni wazi   kwamba tunahitaji kuwa na Jengo kubwa na la kisasa kama hili, lenye Vifaa na Uwezo wa kuhudumia ongezeko la Wageni wanaokuja nchini kwa dhamira mbalimbali ikiwemo Uwekezaji katika Sekta mbalimbali za uchumi.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,

Kupitia hadhara hii, napenda niwahakikishie kwamba Serikali itaendelea kuimarisha Miundo mbinu mengine mbali mbali, kama vile Barabara, Maji Safi na Salama, Skuli za kisasa na Hospitali kubwa zenye huduma za kibingwa kote Unguja na Pemba ili kuweka mazingira bora ya utoaji huduma sambamba na kuboresha Teknolojia ya Mifumo ya Utoaji Huduma kwa njia ya Kielektroniki. Nimedokezwa hapa kwamba Idara ya Uhamiaji hapa Zanzibar ndani ya Jengo hili itawekewa mitambo na mifumo ya kisasa ya kuwezesha kutoa huduma kwa njia ya Mtandao. 

Nachukua fursa hii kuwapongeza sana Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala, akisaidiwa na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ali Hassan kwa kazi nzuri wanazofanya katika uimarishaji wa majukumu ya Idara ya Uhamiaji. Kwa pamoja, wamenithibitishia kwamba, kuimarisha Majengo, Utoaji wa Mafunzo kwa watumishi, kusimamia Stahiki za Watumishi wote, lakini pia wataendelea kuzifanyia maboresho ya mara kwa mara Sheria na Kanuni za Uhamiaji nchini. 

Ndugu Wananchi na Wageni waalikwa, 

Juhudi za Serikali zetu zote mbili ni kubwa katika kuhakikisha Watanzania na Wageni wanaoitembelea nchi yetu wanapata huduma zilizo bora za uhamiaji. Hivyo, ni wajibu wenu wananchi kushirikiana na Serikali kulinda na kutunza Miuondombinu hii ili iweze kudumu katika ubora wake kwa malengo yaliyokusudiwa. Inatupasa tuelewe kwamba sisi sote ni wanufaika wa Miradi hii mikubwa. Hivyo, namna bora ya kuonesha shukurani kwa Serikali zetu, ni kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza rasilimali hizi. Sote tumemsikia Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, alitaja jumla ya Fedha za Kitanzania Bilioni 9,908,782,283.59/= zitatumika hadi kukamilika kwa Mradi huu. Hizo ni fedha nyingi na thamani ya ujenzi wa jengo hili ina tija kubwakwa maendeleo ya nchi. 

Ndugu Wananchi na Wageni waalikwa,

Kwa namna ya kipekee napenda kuipongeza Idara ya Uhamiaji Tanzania, kwa juhudi inazochukua katika kuhakikisha inatoa huduma bora na za Kisasa kwa Wananchi, katika Mikoa na Wilaya zote nchini. Aidha, nawapongeza kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Taifa letu kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama. Niwaombe wananchi tushirikiane nao zaidi, katika kuhakikisha amani na usalama unaendelea kudumu katika nchi yetu.

Namalizia hotuba yangu kwa kutoa shukurani zangu tena kwa kualikwa kuja kushirikiana na wananchi wenzangu  katika sherehe hizi za uwekaji wa Jiwe la Msingi wa Ofisi ya Uhamiaji katika Mkoa huu wa Mjini Magharibi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano. Nawashukuru watu wote waliojitokeza na kufanikisha shughuli hii muhimu. Aidha, natoa shukurani kwa viongozi wa dini kwa dua, wasanii kwa kutupa burudani na vyombo vya habari kwa kuwapatia taarifa wananchi wenzetu kuhusiana na tukio hili. 

Namuomba Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu amani, umoja na mshikamano. Tunamuomba Mola wetu atupe uwezo wa kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa mafanikio ili nchi yetu izidi kupiga hatua za maendeleo. Nakutakieni nyote kila la kheri na Maadhimisho mema ya miaka 60 ya Muungano wetu.