HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA KILELE CHA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 54
YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR, UWANJA WA AMAAN
TAREHE: 12 JANUARI, 2018

Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli;
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan;
Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa;
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi;
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar,

Waheshimiwa Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,

Waheshimiwa Viongozi Wakuu Wastaafu Mliohudhuria,

Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,

Mheshimiwa Job Ndugai;
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid;
Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,

Mheshimiwa Profesa Ibrahim Khamisi Juma,
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Omar Othman Makungu,
Jaji Mkuu wa Zanzibar;

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa,

Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud;
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,

Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya
Siasa Mliohudhuria,

Ndugu Wananchi,

Mabibi na Mabwana,

Assalamu Aleikum

Kwa unyenyekevu mkubwa namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Ardhi na vyote viliomo ndani yake, kwa kutujaalia uhai na afya njema na tukaweza kukusanyika hapa hivi leo, kwa ajili ya kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ya tarehe 12 Januari, 1964.

Kwa niaba ya Wananchi wa Zanzibar, natoa shukurani zangu za dhati, kwako Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuungana nasi katika sherehe hizi.  Kadhalika, natoa shukurani zangu za dhati kwa viongozi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waliopo madarakani na waliostaafu kwa kuhudhuria kwenu.  Vile vile,  nawashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa dini na vyama vya siasa na wananchi wote kwa kuhudhuria kwa wingi katika sherehe hizi muhimu na adhimu.  Ahsanteni sana kwa mahudhurio yenu.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Leo ni siku muhimu sana katika historia ya wananchi wa Zanzibar, ambapo miaka 54 iliyopita, waliikata minyororo ya utawala wa kisultani na vibaraka vyao.  Wananchi wa Zanzibar, walikataa madhila makubwa ya kutawaliwa waliyotendewa na utawala wa Kisultani, wakoloni, mabwanyenye na mabepari ya kunyimwa haki zao za msingi katika kuendesha maisha yao.  Walibaguliwa katika kupata huduma za afya, elimu, fursa za kuitumia ardhi yao, walinyimwa fursa za kazi zenye staha na heshima ya mwanadamu, walinyimwa makaazi bora, walidhulumiwa mashamba yao na kukosa nafasi ya kuendesha maisha yao na kadhalika.  Kwa lengo la kukabiliana na uonevu huo, Chama cha Afro-Shirazi kilichoongozwa na Rais wake Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kilivinjari na kilisimama imara kwa ajili ya kuwakomboa wanyonge wafanyakazi na wakulima wa Zanzibar.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Leo tunapoadhimisha sherehe za Mapinduzi kwa kutimiza miaka 54, hatuna budi kuwakumbuka na kuwashukuru wazee wetu waasisi wa Chama cha Afro-Shirazi, walioongozwa na Rais wake wa Kwanza Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kwa ushujaa wao wa kuzipigania haki zetu, kuleta usawa na maelewano na kuondosha kila aina ya pingamizi walizokuwa wakizipata wananchi wa Unguja na Pemba. Leo ni siku ya kumbukumbu ya ushindi wa wananchi wa Zanzibar na kwamba Mapinduzi yaliuinua na yaliusimamisha utawala wa wanyonge,  wakulima na wafanyakazi; yaliweka usawa na kuwakabidhi tena wafanyakazi na wakulima wa Zanzibar, heshima yao na utu wao, katika nchi yao.