Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Saud Arabia nchini Tanzania Mohammed Mansour Al Malik.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kutokana na Saud Arabia kuwa na wawekezaji wakubwa waliowekeza katika sekta ya utalii nchini humo na hata nje ya nchi yao kuna haja ya kuja Zanzibar kuangalia fursa za kuekeza.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa katika visiwa vya Zanzibar kuna vivutio kadhaa vya kitalii ambavyo vimeweza kuwavutia watalii kutoka nchi mbali mbali duniani hivyo, ni vyema kwa wawekezaji wa Saud Arabia kuja kuekeza Zanzibar.

Aliongeza kuwa ujio wa watalii hapa Zanzibar umekuwa ukiongezeka kila mwaka hivyo iwapo kutajitokeza wawekezaji ambao watawekeza katika sekta ya utalii kutoka nchini Saud Arabia, sekta hiyo itazidi kuimarika kutokana na nchi hiyo kuwa na wawekezaji wakubwa na wenye Kampuni kubwa za kitalii.

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyowekwa katika kuhakikisha ujio wa watalii hapa Zanzibar unaongezeka ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume pamoja na Bandari ya Mpigaduri.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali ya Saud Arabia kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya
afya, elimu, miundombinu ya barabara na nyenginezo.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Saud Arabia imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kutoa nafasi za masomo kwa vijana wa Zanzibar kwenda kusoma katika vyuo vya nchi hiyo hatua ambayo imeweza
kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini.

Pia, Dk. Shein aliipongeza nchi hiyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya miundombinu hasa ya barabara kwa kusaidia ujenzi wa barabara huko kisiwani Pemba ikiwemo barabara ya Wete hadi
Gando na Wete hadi Konde kupitia Mfuko wa Maendeleo wa nchi hiyo (Saud Fund).

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliipongeza nchi hiyo kutokana na azma yake ya kusaidia ujenzi wa barabara ya Chake hadi Wete, ukarabati wa Hospitali Kuu ya MnaziMmoja pamoja na kukiimarisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na watu wake itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Saud Arabia huku akisisitiza haja kwa nchi hiyo kufungua Ubalozi Mdogo hapa Zanzibar.

Nae Balozi wa Saudia Arabia nchini Tanzania, Mohammed Al Malik alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Saud Arabia itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo huku akimuahidi kuwa juhudi za makusudi atazichukua katika kuhakikisha wawekezaji wa sekta ya utalii wanakuja kuekeza Zanzibar.

Balozi Mohammed Mansour Al Malik alimueleza Dk. Shein kuwa ameyaona mazingira ya Zanzibar na kueleza kuwa ni mazingira ya pekee ambayo yana kila sifa ya kuwa kivutio cha watalii kutoka kila pembe ya duniani ikiwemo Saud Arabia.

Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi atazichukua katika kuhakikisha anakuwa balozi wa kuitangaza Zanzibar kwa watu wa Saud Arabia pamoja na wawekezaji na wafanyabiashara wa nchi hiyo. Aliongeza kuwa nchi yake ina wawekezaji wengi ambao wamewekeza nchi kadha duniani katika sekta ya utalii, hivyo atatumia fursa hiyo kuwashawishi kuja kuekeza na Zanzibar.

Aidha, Balozi Mohammed Mansour Al Malik alimueleza Dk. Shein kuwa Serikali ya Saud Arabia chini ya Mfuko wa Maendeleo wa nchi hiyo (Saud Fund),utaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, afya, elimu pamoja na kuongeza idadi ya nafasi za masomo.