RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa inapendeza kuona Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa inaungana na Mataifa mengine duniani katika kukuza na kuimarisha mashindano ya kusoma na kuhifadhi Qurani.Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo katika hafla ya mashindano ya 21 ya Qurani ya juu 30, yaliyofanyika katika uwanja wa Benjamin William Mkapa Jijini Dar-es-Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali pamoja na maelfu ya wananchi.

Katika hotuba yake, Rais Dk. Mwinyi aliwataka Watanzania kuona kuwa ushiriki wao katika mashindano hayo ni fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania kama inavyofanya katika mashindano mengine ya Kitaifa inayoshiriki.Alisema kuwa ni jambo jema na la kheri kushuhudia kwamba mashindano ya Kuhifadhi Qurani, kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu yanazidi kupata nguvu na umaarufu duniani hivi sasa.Aliongeza kuwa nchi mbali mbali zinaendelea kuandaa mashindano hayo kwa ngazi ya Kitaifa na Kimataifa.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Watanzania wa rika mbali mbali wamekuwa wakionesha umahiri mkubwa katika mashindano na kupeperusha bendera ya nchi yao Kimataifa, katika mataifa kadhaa ikiwemo Saud Arabia, Iran,Oman, Malaysia na nchi nyenginezo.Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba ni vyema kwa madrasa za hapa nchini pamoja na taasisi nyengine za dini ya Kiislamu zikahakikisha kwamba zinawaandaa vizuri vijana wenye vipaji vya kuhifadhi Quarani ili pale wanaposhiriki waiwakilishe vyema Tanzania na warejee nyumbani wakiwa na zawadi na tunzo mbali mbali.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi aliwapongeza washiriki wote wa mashindano hayo kwa kufikia hatua hiyo lakini aliwapongeza zaidi walimu na Masheikh waliowaandaa vijana hao waliofikia kiwango hicho.Alhaj Dk. Mwinyi alotumia fursa hiyo kumuomba Mwenyezi Mungu awape fadhila nyingi na kheri walimu na Masheikh wote waliotoa mafunzo ya kitabu kitukufu cha Qurani hadi mafundisho yake yakaweza kufahamika.

Alisisitiza kwamba ni wajibu kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kuisoma Qurani kwa hukumu zake na kuzingatia zaidi yale yanayoelekezwa ndani yake kwani inapatikana elimu kamili ya maisha yote ya mwanaadamu.Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Miwnyi aliwahimiza Waumin wa Dini ya Kiislamu kuzingatia mafunzo, maamrisho na makatazo yaliyomo katika kitabu Kitukufu cha Qurani ili kukuza ucha Mungu wao.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba pamoja na kuwa washiriki wa mashindano hayo ni Waislamu shughuli hiyo ilihudhuriwa pia, na baadhi ya wasio kwua waislamu jambo ambalo linaifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa tofauti na mataifa mengine.“Huu ndio utamaduni mzuri ambao waasisi wa Taifa letu, wametujengea na tumelelewa nao, watu wa dini na madhehebu tofauti tunaweza kuishi na kwua pamoja kwa kustahamiliana, kuvumiliana na kushirikiana hata katika masuala yanayohusu dini mbali mbali zinazofuatwa na Watanzania”,alisema Alhaj Dk. Mwinyi.

Katika hotuba yake hiyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Marehemu Dk. John Pombe Magufuli alionesha njia kwa mifano katika kujenga ustahamilivu na kuwataka Watazania kuishi kwa upendo na umoja bila ya kujali tofauti zao ambapo katika mashindano ya mwaka 2019 yeye mwenyewe alikuwa mgeni rasmi.

Mapema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alitoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa wale wote walioshiriki katika mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Nae Rais wa Taasisi ya Al- Hikma Foundation Sheikh Sharif Abdulqadir akimkaribisha Alhaj Dk. Mwinyi alieleza jinsi taasisi hiyo inavyojishughulisha na shughuli hizo kwa muda mrefu na kuwapongeza Watanzania kwa kuunga mkono.

Mufti Mkuu wa Tanzania Shekh Abubakar Bin Zubeir Bin Ally alisema kwamba mashindano hayo ya Qurani yameifanya Tanzania izidi kutajika duniani kote na kuwapongeza washiriki wote wa mashindano hayo.

Sheikh Alhad Mussa Salum, Sheikh Mkuu wa Dar-es-Salaam aliwataka Watanzania wampende Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kama walivyokuwa wakimpenda Hayati Rais Magufuli.Mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Hikma Sheikh Nurdin Kishki alitoa pongezi kwa Serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuunga mkono mashindano hayo huku akiipongeza Benki ya PBZ Islamic kwa kuwa mdhanini Mkuu wa mashindano hayo pamoja na wadhamini wengine. 

Katika mashindano hayo, mshindi ni Jibrila Omar Hassan kutoka Niger ambaye amejinyakulia TZS Milioni 20, Cheti cha ushiriki pamoja na vocha ya TZS milioni moja na mshindi wa Pili ni Hassan Ibrahim kutoka Sudan aliyepata milioni 12 na mshindi wa tatu ni Sangare Halid kutoa Ivory cost aliyepata milioni 7.5 na mshindi wa nne ni Omar Abdallah Salim kutoka Tanzania Bara aliyepata zawadi ya TZS milioni 5 na wa tano ni Mustafa Ali kutoka Nigeria aliyepata TZS milioni tatu.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika mashindano hayo aliwemo Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam pamoja na viongozi wengine wa dini na Serikali wa ndani na nje ya Tanzania ambapo mashindano hayo yamezishirikisha nchi 21 za Afrika na kuwashirikisha washindanaji 23 kutoka nchi mbali bali za Afrika isipokuwa mshindanaji mmoja kutoka Senegal hakuweza kufika.