RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi amefutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na kueleza kwamba kitendo cha kufutarisha ni utamaduni uliopo wa viongozi wakuu wa Zanzibar ambao ameamua kuuendeleza.Hafla hiyo ya futari iliyoandaliwa na Rais Dk. Mwinyi kwa ajili ya wananchi wa Mkoa huo wa Kaskazini Pemba ilifanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete, Pemba ambayo ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa pamoja na makundi maalum ya wananchi wa Mkoa huo.

Katika maelezo yake, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa kumekuwa na utamaduni wa viongozi wa nchi kila inapofika mwezi Mtukufu wa Ramadhani huwa wanafutarisha wananchi mbali mbali katika mikoa yao na yeye akaona utamaduni huo ni mzuri na wa busara hivyo ameazimia kuuendeleza.Alisema kuwa angependa wananchi wengi wawepo lakini kutokana na ugumu wa kufanya hivyo ameamua kuwaalika kwa makundi ambapo ni matarajio yake kwa wale waliopata nafasi ya kuwawakilisha wenzao wajue lengo ni kuwepo kwa watu wengi.

Alitoa shukurani kwa wananchi wote waliojitokeza kwa wingi katika futari hiyo na kupongeza kwa kutekelezwa vyema dhamira yake ya kuwaalika wananchi hao na dhamira ya wananchi hao ya kukubali mwaliko wake huo.Aidha, Alhaj Dk. Miwnyi alieleza kwamba ameona haja ya kuandaa furari hiyo ili aweze kuungana na wananchi wa Mkoa huo katika mwezi huu mtufu wa Ramadhani.

Katika shukrani zak hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza utaratibu wake ambao ameuanza wa kufutari na wananchi wa mikoa ya Unguja na Pemba ambapo kesho Jumaatano ya Machi 05.2021 anatarajia kufutari na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba.

Sheikh Hamad Hassan Bakari kutoka Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huo, alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa mwaliko wake huo alioufanya kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na kumuombea dua Rais ili azidi kuongoze kwa amani na usalama.

Nae Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi kwa upande wake aliungana na viongozi wanawake wa kitaifa pamoja na wananchi wa Mkoa huo wa Kaskazini Pemba katika futari hiyo maalum aliyoianda Alhaj Dk. Mwinyi hapo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi aliungana na waumini wa dini ya Kiislamu wa Mkoa huo wa Kaskazini Pemba katika sala ya Taraweh katika msikiti wa Ibadhi Mtemani ambapo mara baada ya sala hiyo alipata frsa ya kuwasalimia wananchi na kuwaeleza kwamba yeye ni muumini wa amani na anaelewa kwamba maendeleo hayaji bila ya kuwepo kwa amani.Alisema kuwa hivi sasa Zanzibar imefanikiwa kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa hivyo, kilichobaki ni kushirikiana kwa pamoja katika kuiletea Zanzibar maendeleo.

Aliongeza kuwa Zanzibar inaendelea kuwa na amani na utulivu mkubwa hivyo ni vyema wananchi wote wakahakikisha hazina hiyo inalindwa ili nchi izidi kupata maendeleo.Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwaomba Waumini wa msikiti huo kuendelea kumuombea dua ili aweze kutekeleza vyema jukumu alilopewa na wananchi la kuiongoza nchi ikiwa ni pamoja na kutekeleza vyema ahadi alizozitoa kwa wanachi pamoja na dhamira zake nyengine za kuiletea Zanzibar maendeleo.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza azma ya ziara yake ya siku mbili kisiwani Pemba ikiwa ni pamoja na kufutari pamoja na wananchi wa mikoa yote miwili ya Pemba.