RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ujenzi wa jengo jipya la Abira (Terminal III), katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume unapaswa kwenda sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wasafiri.Dk. Mwinyi amesema hayo leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, wakati alipolitembelea Jengo jipya la Abiria (Terminal III) lililo katika hatua za mwisho kukamilika ujenzi wake.

Amesema ujenzi wa jengo hilo umefanywa ili kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa wasafiri, hivyo akawataka wasimamizi wa ujenzi kuhakikisha kasoro mbali mbali zilizopo katika jengo hilo zinarekebishwa ili kuwepo utoaji mzuri wa huduma.Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ameridhishwa na hatua iliofikiwa ya ujenzi huo na kuwataka wasimamizi wa ujenzi kurekebisha mapungufu madogo madogo ili kuwa na uwanja wa kisasa na kuepuka hali iliyopo katika jengo la zamani.

Aliyataja maeneo yanayohitaji kushughulikiwa kuwa ni pamoja na kuongeza vizimba vya Uhamiaji, eneo la ukaguzi wa mizigo pamoja na kuongeza mashine kwa watendaji wa masuala ya‘Custom’.Dk. Mwinyi aliwataka wasimamizi wa ujenzi huo kuhakikisha kunakuwepo mabango yanayoainisha taarifa za safari za ndege,kama ilivyo katika viwanja vyote vya Kimataifa Duniani, jambo ambalo halijafanyika hadi hivi sasa.


Aidha, aliwataka kukamilisha hatua mbali mbali zilizobaki mbele ya jengo hilo, ikiwemo upandaji wa majani, ujenzi wa uzio na barabara ili kuupa haiba Uwanja huo, akibainishaku wa sura ya nchi huanzia pale mtu anaposhuka.

Nae,Katibu Mkuu Wizara Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil Bakar,alisema ujenzi wa jengo hilo uko hatua za mwisho kukamilika, ambapo unatarajiwa kukabidhiwa Serikalini mapema mwezi wa Mei, 2021.Alisema ujenzi huo umefikia zaidi ya asilimia tisini, na kusema baadhi ya mambo yatakayoshughulikiwa katika kipindi kifupi kijacho kuwa ni pamoja na ushughulikiaji wa mifumo ya‘Internet’, mifumo ya Uhamiaji pamoja na mifumo ya ukaguzi.

Karika ziara hiyo, Rais Dk. Mwinyi alitembelea maeneo mbali mbali ya jengo hilo, ikiwemo eneo la ukaguzi wa mizigo, eneo la Usalama , ukaguzi wa Paspoti, eneo la Abiria wanaosubiri ndege, vyumba vya wageni mashuhuri (VIP), eneo la wasafiri wa nje, eneo la kupokelea mizigo, eneo la wasafiri wa nje/ndani pamoja na sehemu ya Abiria wanaosubiri ndege.

Aidha, katika ziara hiyo Dk. Mwinyi aliambatana na Viongozi mbali mbali wa Serikali, akiwemo Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Rahma Kassim Ali, Katibu wa Baraza Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, pamoja na viongozi wengine wa Serikali.