RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuunga mono juhudi za wahisani katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii.Dk. Mwinyi ameeleza hayo alipozungumza na Dk. Charlotte Hawkins, aliefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kusalimiana.

Alisema Zanzibar inahitaji wataalamu wengi zaidi kutoka nje kuja nchini na kusaidiana na wataalamu wazalendo ili kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo za Afya na Elimu.Alisema ujio wa Daktari Hawkins hapa nchini na kujikita katika kukabiliana na changamoto inayowakabili watoto wanaozaliwa na hitilafu katika miguu imewawezesha watoto wengi kunufaika na huduma zilizotolewa.

Alimpongeza Daktari huyo kwa kazi kubwa na nzuri aliyofanya katika kipindi chote akiwa nchini, na kubainisha azma ya Serikali ya kuvutia wahisani na wataalamu   kwa kuzingatia kuwa haiwezi kuwafikia watoto wote wenye mahitaji.Alieleza kuwa pamoja na Daktari huyo kupitia changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa shughuli zake, amechangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa maisha ya watoto. ambapo baadhi ya nyakati Serikali hulazimika kuwasafirisha nje kwa matibabu.
   
Dk. Mwinyi alimuomba Daktari huyo kuendelea na juhudi za kusaidia jamii katika kukabiliana na changamoto hiyo ,huku akiahidi Serikali itahakikisha inampa kila aina ya ushirikiano kufanikisha malengo yake.
   
Nae, Dk. Charlotte Hawkins, Daktari bingwa wa Upasuaji kutoka nchini Uingereza, pamoja na mambo mengine aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya zanzibar kwa mabadiliko makubwa yanayofanyika katika kuimarisha sekta ya Afya hapa nchini.Alitumia fursa ahiyo kupongeza mashirikiano makubwa aliyopata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zazibar kupitia Wizara ya Afya pamoja na watendaji wa Wizara hiyo, hatua iliomuwezesha kufanikisha vyema majukumu yake.

Mapema, Waziri wa Afya Ahmeid Nassor Mazrui alisema Dk. Charlotte Hawkins amekuwa nchini kwa kipindi cha miaka 13 sasa, akisaidia juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto zinazowakbili watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa na miguu yenye hitilafu.Alisema katika kipindi hicho amefanya kazi kubwa na nzuri ya kutoa huduma katika Hospitali ya Abdalla Mzee Kisiwani Pemba kwa kuboresha miguu bandia pamoja na kutengeneza viatu vya ngozi, ikiwa ni hatua ya kwanza ya kuondoa hitilafu ya miguu kwa watoto.

Alisema pia amesaidia kwa kiasi kikubwa kujenga uwezo na kurekebisha miundo mbinu katika skuli mbali mbali ambapo watoto wenye hitilafu ya miguu wanasoma.

Waziri Mazrui alimpongeza Daktari huyo kwa kubeba dhima ya kuwashajiisha wahisani kutoka nje kutoa michango yao ya hali na mali pamoja na wataalamu wengine kuja nchini kusaidia upatikanaji wa huduma za afya.