RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza haja kwa nchi za Afrika kushirikiana katika kuimarisha sekta ya biashara.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania Yonas Yosef Sanbe ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo kuwa nchi za Afrika zina kila sababu ya kushirikiana katika kuimarisha sekta ya biashara hasa ikizingatiwa kwamba zina rasilimali za kutosha.Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo wa Ethiopia kuwa Zanzibar inathamini ushirikiano wa uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Ethiopia na Tanzania na kumuhakikishia kwamba hatua hiyo itaendelezwa kwa azma ya kuimarisha maendeleo endelevu.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Sanbe kwamba kuwepo kwa safari za Kampuni ya Ndege ya Ethiopia katika nchi nyingi za bara la Afrika ikiwemo Tanzania kutauimarisha zaidi ushirikiano katika sekta ya biashara pamoja na sekta nyenginezo.Rais Dk. Mwinyi pia, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Ethiopia katika kuiletea maendeleo nchi hiyo pamoja na wananchi wake.Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa nchi za Afrika kuendelea kushirikiana katika kuendleza sekta mbali mbali za maendeleo.

Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuendeleza ushirikiano na uhusiano uliopo kati ya pande mbili hizo.Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Balozi Sanbe kwa kumpa taarifa juu ya hali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii inavyoendelea nchini humo pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Ethiopia katika kuhakikisha mafanikio yanapatikana.

Mapema, Balozi wa Ethiopia Nchini Tanzania Yonas Yosef Sanbe alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Ethiopia ni wa kihistoria ambao umeasisiwa na Hayati Rais Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mfalme Haile Selassie.Balozi Sanbe alieleza kuwa uhusiano huo na ushirikiano uliopo bado unaonekana kwa kuacha alama kwani jina la aliekuwa kiongozi wa nchi hiyo Mfalme Haile Selassie linatumika hapa nchini ambako bado kuna skuli kuna Skuli ya Sekondari ya Haile Selassie kwa upande wa Zanzibar pamoja na barabara ya Haile Selassie iliyopo Jijini Dar-es-Salaam.

Hivyo, Balozi huyo wa Ethiopia nchini Tanzania alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba nchi yake inathamini sana uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria na ameahidi itaendelea kushirikiana na Tanzania ikiwemo Zanzibar katika kuanzisha nyanja nyengine za mashirikiano ikiwemo biashara.Alifahamisha kwamba ushirikiano na uhusiano kati ya Zanzibar na Ethiopia unahitajika zaidi kwani hata utamaduni wa wananchi wa Ethiopia na Zanzibar umeshabihiana kwa kiasi kikubwa hivyo, kuna haja kwa pande mbili hizo kuutunza ili uzidi kuleta manufaa.

Aidha, Balozi Sanbe alimueleza Rais Dk. Mwinyi dhamira ya nchi yake ya kuanzisha mafunzo ya lugha ya Kiswahili katika Taasisi za Elimu ya Juu kwa lengo la kuikuza lugha hiyo sanjari na kuimarisha uhusiano na nchi nyengine za Bara la Afrika.

Balozi Sanbe alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Mwinyi maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yalivyofikiwa nchini humo na juhudi za Serikali yake katika kuhakikisha kwamba mipango iliyopangwa inatekelezwa ipasavyo.Pamoja na hayo, Balozi huyo wa Ethiopia amesisitiza haja ya kuiamrisha diplomasia ya kibiashara kati ya nchi hiyo na Tanzania huku akieleza jinsi Kampuni kadhaa za uwekezaji kutoka Ethiopia zilivyoeleza azma ya kuja kuekeza hapa Tanzania.