RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa baraka zake na kuunga mkono mashirikiano yanayoimarishwa kati ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika suala zima la kuimarisha uwekezaji nchini.Rais Dk. Mwinyi ametoa baraka hizo katika mazungumzo aliyoyafanya kati yake na uongozi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) chini ya Mkurugenzi wake Mtendaji Shariff Ali Shariff pamoja na uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) chini ya Mkurugenzi wake Mtendaji Dk. Maduhu Isaac Kazi, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa jambo wanalolifanya na kuendeleza utaratibu wa kukuza mashirikiano ni jambo la busara na lina tija kubwa katika masuala ya uwekezaji hapa nchini kwani fursa zilizopo zinafaa kufanywa kwa pamoja.Hivyo, alisema kuwa uwamuzi huo anauunga mkono na kuzitakia maendeleo makubwa Taasisi hizo kwa azma ya kufikia lengo lililokusudiwa.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ipo haja ya kuuimarishwa zaidi utaratibu wa Hati ya Maelewano (MOU) iliyokuwepo hapo awali kwani wakati umefika kwa yale yaliyokuwa hayamo yaweze kuigizwa kwenye (MOU) hiyo kwa lengo la kupata tija zaidi kwa pande zote mbili.Alisema kuwa suala la kubadilishana uzoefu kati ya Taasisi mbili hizo ni jambo muhimu sana hatua ambayo itasaidia kupatikana kwa mafunzo kwa watendaji wa Taasisi hizo kwa azma ya kuimarisha sekta ya uwekezaji hapa nchini.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza ndoto yake ya kuona kwamba Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) inakuwa na Kituo Kimoja cha Kutoa Huduma.Aliongeza kuwa hatua hiyo ya kuwa na Kituo Kimoja cha Kutoa Huduma itasaidia kuondosha urasimu na ucheweleshaji wa kutoa huduma kwa wawekezaji na kuifanya sekta ya uwekezaji kuwa rahisi hapa nchini.Hivyo, Rais Dk. Mwinyi amezishajihisha Taasisi hizo na kuzitaka kuwa kioo na kielelezo thabiti katika kuhakikisha suala zima la uwekezaji linaleta manufaa kwa Taifa.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Shariff Ali Shariff alieleza kwamba mashirikiano yanayoimarishwa kati ya Taasisi mbili hizo ni njia moja wapo ya kuimarisha Muungano uliopo hasa ikizingatiwa kwamba Taasisi hizo zinategemeana.Alisema kuwa mashirikiano hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza sekta ya uwekezaji hapa nchini na kueleza kwamba ziara ya siku tatu ya Taasisi ya (TIC) hapa Zanzibar ina azma ya kuangalia maeneo ya kushirikiana kwa lengo la kuitangaza Zanzibar.

Alieleza kwamba tayari kabla ya Taasisi hiyo kuja hapa Zanzibar katika ziara yake hiyo ya siku tatu imeanza kazi ya kuitangaza Zanzibar huko nchini Misri na kuweza kuwavutia wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar ambapo wapo waliojitokeza kuja kuekeza kiwanda cha dawa hapa Zanzibar.Pia, alieleza hatua zinazochukuliwa kwa pamoja katika kutengeneza Hati ya Makubaliano (MOU), kati ya Taasisi hizo na tayari wameshachagua timu ya kufanya kazi wakiwemo wataalamu wa masuala hayo ya uwekezaji.

Sambamba na hayo, Mkurugenzi Shariff alimuhahidi na kumuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba (ZIPA) inajitahidi kuleta mabadiliko ambapo hivi sasa inatoa vibali vya kazi kwa muda wa dakika 15 iwapo taratibu zote stahiki zimeshafanyika.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa (ZIPA) alieleza mikakati iliyowekwa na Mamlaka hiyo ya kuhakikisha Maeneo ya Viwanda yaliyopo Amani yanawekwa katika mazingira mazuri ili kuweza kuwavutia wawekezaji ambapo tayari kwa upande wao timu nzima ya watendaji itakuwepo katika eneo hilo.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dk. Maduhu Issac Kazi alieleza kwamba Taasisi hizo zimedhamiria kushirikiana katika suala zima la uwekezaji hasa katika maeneo mbali mbali ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu, kushirikiana juu ya masuala mazima ya huduma kwa uwekezaji na mambo mengineyo.

Pamoja na hayo, Dk. Kazi alieleza haja ya kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ambayo itakuwa na wajumbe wa Mamlaka ya (ZIPA) na (TIC) ambayo itazikutanisha Taasisi hizo japo mwaka mara mbili ili kujadili maendeleo ya uwekezaji kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara sanjari na Jamhuri ya Muungano kwa jumla.