RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza Umoja wa Mataifa (UN), kwa azma yake ya kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi wake kupitia mashirika ya Umoja huo.Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi alitoa pongezi hizo leo wakati alipofanya mazungumzo na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), nchini Tanzania Bwana Zlatan Milisic ambaye alifika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha rasmi kwa Rais.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi aliupongeza Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kutoa mashirikiano makubwa katika kuendeleza miradi kadhaa ya maendeleo ambayo ina tija kwa ustawi wa wananchi wa Zanzibar.Rais Dk. Mwinyi alimueleza Mratibu huyo wa UN nchini Tanzania kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na juhudi zake za kuimarisha uchumi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi ikiwa imeweka kipaumbele katika utekelezaji wa mipango na Sera za Uchumi wa Buluu.

Rais Dk. Mwinyi katika mazungumzo yake hayo alieleza kuwa hali ya amani na utulivu ya Zanzibar imezidi kuimarika kutokana na mashirikiano mazuri yaliopo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo kipaumbele zaidi kilichowekwa hivi sasa ni kuhakikisha kunaimarishwa maendeleo endelevu.Aliongeza kwamba kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kumeipelekea Zanzibar kuimarika kisiasa, kiuchumi na kijamii na kueleza matumaini yake makubwa ya kupata maendeleo zaidi kutokana na mashirikiano hayo yaliopo.

Alieleza kwamba kuibuka kwa maradhi ya COVID 19 duniani kupelekea sekta ya utalii kuzorota, sekta ambayo imekuwa ikitegemewa kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha pato la Taifa na uchumi wa Zanzibar.Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Mratibu huyo wa UN, nchini Tanzania mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake huku akieleza matumaini yake kwa UN kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kupitia mashirika yake makuu.

Sambamba na hayo, Rais. Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Umoja huo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya hasa katika kuimarisha miundombinu na mifumo ya utoaji huduma na uendeshaji.

Alifahamisha haja ya kuendelea kuungwa mkono katika kupambana na vifo vya akina mama na watoto na kusema kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF limekuwa mdau mkubwa wa Zanzibar katika kuisaida kuendeleza sekta ya afya lakini hata hivyo, juhudi za makusudi zinahitajika ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) la kuhakikisha linauenzi Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni Urithi wa Dunia, kwani hivi sasa baadhi ya nyumba nyingi katika mji huo kuhitaji matengenezo kutokana na uchakavu wake.

Alieleza kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Afya Ulimwenguni, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Shirika hilo kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya hasa katika kupambana na maradhi ya COVID 19.Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hivi sasa Zanzibar inaadaa utaratibu wa kuwawezesha mahujaji kupata tiba ya chanjo ya COVID 19 ili kukidhi vigezo vilivyowekwa na Serikali ya Saud Arabia mwaka huu katika kushiriki ibada hiyo tukufu hatua ambayo mashirika ya Umoja huo yanaweza kuiunga mkono Zanzibar ili kufikia matakwa hayo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Mratibu huyo mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuimarisha uchumi wake sambamba na Sera na madhubuti zilizopo ikiwa ni pamoja na kuishirikisha sekta binafsi.

Nae Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), nchini Tanzania Bwana Zlatan Milisic alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya Umoja huo ya kuisaida Zanzibar katika kuendeleza miradi yake ya maendeleo na kuhakikisha mashirika yote yaliyopo Tanzania yanaendelea kuisaidia Zanzibar ili kufikia azma yake.Bwana Zlatan Milisic alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar wka kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita huku akieleza azma ya UN ya kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha miradi inayosimamiwa na mashirikia yake inaleta manufaa kwa wananchi wa Zanzibar.

Alipongeza mashirikiano na uhusiano mzuri uliopo kati ya mashirika ya UN na Zanzibar na kueleza kwamba Umoja huo utaongeza nguvu katika kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana hasa katika uchumi wa Zanzibar ukiwemo uchumi wa buluu pamoja na sekta za kiuchumi na kijamii kama vile afya, elimu, urithi wa mji mkongwe, usawa wa kijinsia, wanawake na watoto na mengineyo.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wawekezaji wa Kampuni ya “Eliya Food Overseas Limited” kutoka Dubai ukiongozwa na Bwana Shabbir Virjee ambao wameonesha nia na kueleza utayari wao wa kuekeza viwanda vya matunda, mbogamboga pamoja na viwanda vya uvuvi sambamba na kuonesha nia ya kusaidia wafanyabiashara wa soko la Darajani kwa kujenga sehemu maalum ya kuhifadhia bidhaa zao zikiwemo mboga mboga, samaki na bidhaa nyenginezo ili zisiharibike.

Rais Dk. Mwinyi aliueleza ujumbe huo wa wawekezaji wa Kampuni ya “Eliya Food Overseas Limited” kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari na imeshajipanga vyema kuwapokea wawekezaji wenye lengo la kuekeza Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira mazuri ya uwekezaji.