RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi wa Zanzibar   kutumia vyema fursa ya kuwepo Skuli ya ‘Turkish Maarif Zanzibar’ kwa kuwapeleka watoto wao ili kupata elimu.Dk. Mwinyi ametoa wito huo leo katika Ufunguzi na Mahafali ya Kwanza ya Kidato cha Sita ya Skuli ya ‘Turkish Maarif Zanzibar’ , iliiopo Mombasa Jijini Zanzibar.

Akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi;  Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amesema kuwepo kwa Skuli hiyo kunaendana na malengo ya Serikali ya kupanua haki ya elimu nchini,  hivyo akawataka wananchi kutumia vyema fursa ya kuwepo kwake na kupeleka watoto wao kusoma.Alisema uwepo wa skuli hiyo ni kigezo cha hatua ya maendeleo ya Elimu Zanzibar, pamoja na kuunga mkono malengo ya Serikali na hivyo akipongeza Uturuki kwa kufungua skuli hiyo.

Aidha, aliwapongeza wanafunzi wote waliomaliza masomo yao ya kidato cha sita kwa kufanikiwa vyema , hususan wale waliopata alama za daraja la juu, na kusisitiza umuhimu wa kuudmisha nidhamu katika kufikia mafanikio.Alisema nidhamu pamoja na bidii ndio msingi wa kila kitu ikiwemo masomo,  hivyo akasisitiza muhimu wa wanafunzi kuhudhuria skuli kikamilifu pamoja na kupenda masomo yao.

“Niwasihi watoto wanaomaliza kidato cha sita leo hii watafurahi, ila wajue hii ni hatua moja huko waendako Vyuo vikuu watahitajika kuendelea na nidhamu zaidi, maana watapaswa kujisimamia wao wenyewe”, alisema.Vile vile aliwataka kuongeza bidii ili waweze kufanikiwa zaidi katika masomo yao ngazi za juu.

Katika hatua nyengine, aliwataka wazazi na walezi kusimamia kikamilifu maendeleo ya elimu ya watoto wao, sambamba na wanafunzo kuepuka yale yopte yatakayodumaza masomo yao, huku akiahidi Serikali kuendelea kulinda haki zao.Aidha, alipongeza juhudi za wazazi na walezi katika kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji pamoja na kushirikiana na serikali kupiga vita vitendo hivyo na kusisitiza umuhimu wa kuondokana na muhali.

“Tuwafundishe watoto wetu jinsi ya kujilinda dhidi ya udhalilishaji na kutoa taarifa pamoja na kuchukua hatua…….…….Zanzibar bila ya udhalilishaji inawezekana”, alisema.

Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohamed Said alisema Wizara hiyo imejipanga kufanya mageuzi mkubwa katika elimu ya msingi nchini, kwa kuanzisha mitaala ya kujenga umahiri ndani ya kipindi cha miaka mitano, ikiwa ni hatua ya kuwajengea msingi bora wa elimu.Aliwataka walimu kuwasaidia wanafunzi wa elimu ya msingi ili waweze kujiamini pale watakapofikia elimu ya ngazi za juu.

Mapema, Mwalimu Mkuu wa Turkish Maarif Zanzibar, Ahmeid Ali Makame, alisema jumla ya wnaafunzi 49 walijisajili kufanya mitihani ya kidato cha sita mwaka 2021 katika masomo ya Sayansi na Sanaa na kufanikiwa kuwa miongoni mwa skuli bora kwa kupasisha wanafunzi 14 wa daraja la kwanza.Aidha, katika Risala yao, wanafunzi hao wamewashukuru walimu wao kwa kubeba dhima na kufanya juhudi kubwa zilizowezesha kufikia maf anikio, sambamba na wazazi kwa kuwasimamia vyema katika masomo yao.

Vile vile walitoa shukuran kwa Serikali kwa kuendelea kuiunga mkono skuli yao pamoja na juhudi za kuendeleza elimu nchini.Katika hafla hiyo Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishiriki, ambapo Mama Mariam Mwinyi alipata fursa ya kukata utepe pamoja na kutembelea madarasa mbali mbali kuangalia shughuli za kitaaluma.