Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi leo Agosti 26, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Jamhuri ya Msumbiji nchini Tanzania, Mhe. Balozi Ricardo Amrosio Mtumbuida aliyefika kujitambulisha, Ikulu Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alipongeza ushirikiano uliopo kati ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika suala zima la kulinda amani.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Ricardo Amrosio alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020 na kuweza kushika wadhifa wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislam ya Pakistan nchini Tanzania, Mhe. Balozi Muhammad Saleem na kuzungumzia masuala mbalimbali ya kimaendeleo na uhusiano wa kibiashara baina ya Pakistan na Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi amesema kuna umuhimu wa Pakistan kuendelea kushirikiana na wafanyabiashara wa Zanzibar katika sekta binafsi kupitia Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (Zanzibar Chamber of Commerce) kwa kutembeleana kuimarisha mahusiano na fursa za kibiashara.

Kwa Upande wake Mhe. Balozi Muhammad Saleem amesema Zanzibar inaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa na Pakistan kutokana na ushirikiano uliopo wa kibalozi kupitia sekta za elimu, Uchumi wa Buluu, biashara pamoja na fursa za masomo.