RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametia saini kitabu cha maombolezi ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk. John Joseph Pombe Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.Rais Dk. Mwinyi ametia saini kitabu hicho cha maombolezi huko katika viwanja vya ukumbi wa Karimjee, ulioko Jijini Dar es Salaam na kueleza jinsi alivyopokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha kiongozi huyo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza jinsi Hayati Rais Magufuli alivyoitumia nchi kwa nidhamu kubwa sana ikiwa ni pamoja na kusimamia kiuchumi na kimaendeleo kwa misingi ya amani, utulivu, umoja na mshikamao.Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi aliungana na waumini wa dini ya Kislamu katika sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Maamur Upanga, Jijini Dar es salam.

Mapema Rais Dk. Mwinyi alimfariji na kumpa pole Mjane wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko Ikulu Jijini Dar es Salaam.Rais Dk. Mwinyi akiwa na Mama Mariam Mwinyi walimpa pole Mjane wa Marehemu Hayati Magufuli Mama Janet Magufuli na kumtaka awe na subira yeye pamoja na familia yake katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alishiriki kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan mara tu baada ya kuapishwa na kushika wadhifa huo wa Urais.