RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametunukiwa Tuzo ya Juu ya Heshima inayofahamika kama “Legion d’ Honner” na Rais wa Jamhuri ya Ufaransa Emmanuel Macron kutokana na mchango wake mkubwa wakati akiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Tanzania.

Rais Dk. Mwinyi alitunukiwa Tuzo hiyo leo na Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania Mhe. Frederic Clavier kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Ufaransa Emmanuel Macron, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar ambapo Balozi huyo alihudhuria akiwa na ujumbe wake.

Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani zake za dhati kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa kumtunukia Tuzo hiyo iliyotokana na kuthamini kwa dhati mchango wake mkubwa alioutoa wakati akiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Tanzania takriban kwa miaka 10.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa amepokea Tuzo hiyo ambayo ni heshima kubwa kwani hutolewa kwa watu mbali mbali duniani hasa kwa mchango wake unaopaswa kupewa heshima hiyo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba takriban miaka 10 akiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Tanzania ambapo katika kipindi hicho Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika operesheni tano za kudumisha amani hasa zile za Bara la Afrika ambazo zote zimeonesha mafanikio makubwa.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa heshima hiyo na kueleza kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jamhuri ya Ufaransa.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Wafanyabiashara wa Ufaransa na Taasisi mbali mbali za Ufaransa ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi wa Unguja na Pemba.

Alisisitiza kwamba amani na utulivu uliopo Zanzibar ni matokeo ya mazungumzo kati ya vyama vya siasa vya Zanzibar ambavyo viliamua kwa makusudi kwamba waungane waijenge Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuleta amani ndani visiwa vya Zanzibar kwa azma ya kuleta maendeleo ya haraka.
Alisema kuwa kwa vile Ufarasa iko tayari kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ana matumaini makubwa kwamba malengo yaliyoiwekwa ya maendeleo ya Zanzibar yatafikiwa kwa haraka. 

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Bi Aline Coouelle kwa kitendo chake cha kukabidhi kitabu alichokichapisha kwa azma ya kuitangaza Zanzibar kimataifa kutokana na vivutio vyake kadhaa vilivyopo.

Mapema Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier alisema kwamba kuanzia mwaka 2008 hadi 2012 na kuanzia mwaka 2014 Rais Dk. Mwinyi alianzisha uhusiano wa karibu kati ya Jeshi la Ulinzi la Tanzania na Jamhuri ya Ufaransa wenye lengo la kuendeleza uhusiano mzuri.

Balozi Clavier alieleza kwamba Rais Dk. Miwnyi alikuwa kiungo kizuri, kilicholeta uhai katika ushirikiano wa nchi mbili hizo.

Aliongeza kuwa akiwa Waziri katika kipindi hicho, Rais Dk. Mwinyi aliendeleza misingi ya utamaduni wa Tanzania katika nyanja za kimataifa, utamaduni uliowekwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa kudumisha amani na usalama.

Alisema kuwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi wakati huo Vikosi vya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Tanzania vilishiriki operesheni za Umoja wa Mataifa katika operesheni Tano za kudumisha amani hasa zile za Bara la Afrika.

Balozi Clavier alifahamisha kwamba Ufaransa inatambua kwamba Rais Dk. Mwinyi ana moyo wa kupenda watu, na utamaduni wa Ufaransa unawapenda watu wa aina yake.

“Umefanya kazi muhimu za utabibu kwa miaka kadhaa, kama daktari, umeweza kutoa mchango wako wa kisanyansi, hasa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ambayo Ufaransa inashirikiana nayo kwa karibu”,”alisema Balozi Clavier.

Aidha, Balozi Clavier alieleza kuwa Ufaransa inapenda kumpongeza Rais Dk. Miwnyi kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi wa mwaka 2020.

Alisema kuwa mafanikio hayo ambayo yalitarajiwa sana yalitengeneza fursa ya mazungumzo muhimu ya kisiasa hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa utulivu wa visiwa vya Zanzibar. “Kwa kweli umeweka historia kubwa”,alisisitiza Balozi Clavier.

Hivyo, Balozi Clavier alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Jamhuri ya Ufaransa iko tayari kushirikiana na yeye katika azma ya kufanikisha Sera zake za kiuchumi.

Alimueleza kwamba Shirika la Maendeleo la Kifaransa (AFD), Makampuni ya Kifaransa, na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Ufaransa na Tanzania, wamejiandaa kuunga mkono vipaumbele vya Rais Dk. Mwinyi hasa katika Uchumi wa Buluu.

Balozi Clavier alisisitiza kwamba Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Ufaransa hivi karibuni itasaini Makubaliano ya Ushirikiano na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Zanzibar ambao huo ni mwelekeo mzuri unaoendelezwa na Ufaransa.

Sambamba na hayo, kwa upande wake Benoit Araman Meneja Mkuu wa Kampuni ya gesi ya ORYX ya Ufaransa alieleza kiu ya Wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa kuja kuekeza Zanzibar hasa katika sekta ya utalii umeme pamoja na sekta nyenginezo.

Pia, wajumbe hao waliofuatana na Balozi huyo wa Ufaransa walieleza kuvutiwa na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuvitangaza vivutio vyake jambo ambalo waliahidi kuendelea kuliunga mkono ambapo tayari Bi Aline Coouelle ameshachapisha kitabu ambacho kinaitangaza Zanzibar