RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM,  ameungana na mamia ya wananchi katika mazishi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Ramadhan Abdalla Ali “Kichupa”, aliefariki dunia mapema leo asubuhi katika Hospitali ha Rufaa Mnazimmoja na kuzikwa kijijini kwake Jambiani, Mkoa wa Kusini Unguja.

Mazishi hayo yaliofanyika kwa utaratibu wa Chama (CCM), yalioongozwa na Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho, Dk. Ali Mohamed Shein, ambapo viongozi mbali mbali wa Chama na serikali walihudhuria, akiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla pamoja na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mstaafu, Balozi Seif Ali Iddi.

Wengine ni pamoja na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Taifa Shaka Hamdu Shaka, Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Wenyeviti wa CCM wa Mikoa, Wakuu wa Mikoa, Mawaziri pamoja na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi kutoka Mikoa mitatu ya Unguja.

Akisoma wasfu wa Marehemu, Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Suleiman Mzee “charas” alisema Marehemu   Kichupa alizaliwa mnamo mwaka 1941 katika Kijiji cha Jambiani Mkoa Kusini Unguja na kupata elimu ya msingi na sekondari Kijijini hapo na Makunduchi.

Alisema Marehemu alijiendeleza kielimu ndani na nje ya Tanzania, ambapo mnamo mwaka 1978 alipata mafunzo ya Siasa nchini China na Korea Kaskazini.

Alisema mnamo mwaka 1984, Marehemu Kichupa alipata mafunzo ya Siasa katika Chuo cha Siasa Murutunguru Ukerewe Mwanza.

Alisema katika Uhai wake Maehemu alikuwa Mwanasiasa gwiji na kufanikiwa kushika nyadhifa mbali mbali za Uongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Chama cha Mapinduzi, ikiwemo Katibu wa Tawi la ASP Jambiani Kikadini (1963-1965) na Katibu Msaidizi wa ASP Wilaya Kusini Unguja mnamo mwaka 1965.

Alieleza kuwa Mwanasiasa huyo alishika Wadhifa wa Afisa Tawala Wilaya kusini katika ya mwaka 1967 – 1977, Katibu wa CCM Wilaya Kusini Unguja 1977- 1992, pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja kati ya 1992- 1997.

Aidha, alishika wadhifa wa Katibu wa Mkoa Mjini Magharibi kati ya mwaka 1997 – 2012, Mbunge wa Jimbo la Muyuni kati ya 1990-2010, Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kati ya 1977 hadi anafariki.

Vile vile alishika wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Tekelezaji Wazazi Taifa pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja kati ya mwaka 2012 hadi anafariki dunia.

Katibu Suleiman alimsifia Marehemu Kichupa kwa kuwa a;likuwa mwanachama muaminifu wa ASP na baadae CCM, na kiongozi shupavu ambae alikuwa mstari wa mbele katika kukipagania chama cha Mapinduzi.

Aidha, alimtaja marehemu kama muumin safi wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea asieyumbishwa na dhoruba yoyote iliyotishia uhai wa CCM.

“Kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi na Serikali zote mbili, Mwenyekiti waCCM Taifa, Makamu Wenyeviti CCM Zanzibar na Bara na Katibu Mkuu wa CCM, wanatoa mkono wa pole kwa wafiwa, ndugu jamaa na wanachama wote wa CCM na kuwaomba wawe na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba.

Marehemu Ramadhan Abdalla Ali “kichupa” ameacha Kizuka mmoja, watoto 12 na wajukuu 65.