Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi leo Agosti 25, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania.

Mhe. Rais awali alikutana na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Mubarak Mohammed Alsehaijan.

Rais Dk. Mwinyi ameishukuru Serikali ya Kuwait kwa kuendeleza uhusiano wa kihistoria kati yake na Zanzibar pamoja na kuipatia Zanzibar misaada mbalimbali katika sekta za kijamii.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Dk. Mwinyi alikutana na Balozi wa Jamhuri ya Rwanda, Meja Jenerali Charles Karamba. Katika mazungumzo hayo Balozi Karamba alimueleza Mhe Rais mpango wa Shirika la Ndege la Rwanda ‘Air Rwanda’ kuanza safari zake kati ya Kigali na Zanzibar ifikiapo katikati ya mwaka 2022, hatua ambayo itaimarisha sekta ya utalii kwa Zanzibar na Rwanda.


Balozi Karamba alitumia nafasi hiyo pia kumtaarifu Mhe. Rais juu ya mwaliko maalum waliouleta Zanzibar wa kuanzisha Ushirikiano baina ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Bodi ya Maendeleo Rwanda (RDB) unaolenga ushirikiano wa kiuwekezaji na kuwa na kituo kimoja cha kibiashara baina ya Zanzibar na Rwanda.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Regina Hess ambaye alifika Ikulu Zanzibar kuelezea mipango ya ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Zanzibar na Ujerumani hususani kwenye eneo la uboreshaji wa huduma za maji na michezo.

Mapema hii leo, Mhe Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alikutana na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika Jamhuri ya Slovakia Bwana Moustafa Khataw ambaye alimtaarifu Mhe. Rais mpango wa kuanza kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Slovakia mpaka Zanzibar.

Kwa upande wake Rais Dk. Mwinyi alimtaka Mwakilishi huyo kushajiisha wawekezaji wa Slovakia na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatilia mkazo dira ya Uchumi wa Buluu, ikiwemo uvuvi wa bahari kuu pamoja na Mafuta na Gesi huku akibainisha kuwepo rasilimali za kutosha baharini ambazo bado hazijatumika ipasavyo.