Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) na kusisitiza haja ya kuimarishwa ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), aliyefika Ikulu kwa ajili ya kumsalimia Rais.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Meja Jenerali Mabele kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza ushirikiano kati ya JKT na JKU hasa katika kuimarisha mafunzo na uzalishaji mali pamoja na mambo mengine hasa ikizingatiwa kwamba JKT tayari imeshapiga hatua kubwa katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya ujenzi.

Alisema kuwa kwa vile kikosi cha JKT kimeanza shughuli hizo kwa muda mrefu na tayari kina uzoefu wa kutosha, hivyo ni vyema kwa kikosi cha JKU nacho kikapanua wigo kutoka kikosi hicho ambacho kimekuwa kikitumiwa katika shughuli mbali mbali nchini hasa za miradi ya ujenzi ambayo mafanikio yake yanaonekana.

Alisisitiza kwamba ni vyema kikosi cha JKU nacho kikajengewa uwezo ili ifike muda kiwe na Kampuni yake ya ujenzi kama ilivyo kwa kikosi cha JKT ambacho kimeweza kujijengea sifa kubwa katika shughuli za miradi ya ujenzi hapa nchini.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kufurahishwa na ukaribu uliopo kati ya JKT na JKU na kueleza haja kwa kikosi cha JKU kuwa na taratibu zote za kijeshi zinazotakiwa ili kiweze kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuwa na nidhamu ya kijeshi.

Aliongeza kuwa wakati umefika kwa kikosi cha JKU kuweza kuzalisha mali na kujijengea utaratibu maalum wa kuhakikisha tija inapatikana kama ilivyo kwa kikosi cha JKT.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele kwa kupata wadhifa wa kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), pamoja na kupandishwa cheo cha Meja Jenerali.

Mapema, Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele alimueleza Rais Dk. Mwinyi ukaribu na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya kikosi cha JKT na JKU, ambapo ulianza mnamo mwaka 2001 ambapo mashirikiano zaidi yalizan katika masuala ya mafunzo pamoja na mialiko ya sherehe na shughuli nyengine za kimaendeleo.

Aliongeza kuwa katika upande wa mafunzo, mashirikiano makubwa yameweza kupatikana kati ya vikosi hivyo.

Aidha, Meja Jenerali Mabele alieleza kuwa kwa mara ya kwanza kikosi chake cha SUMA JKT kimeweza kupata fursa ya ujenzi wa mradi wa Tawi la Chuo cha Mwalimu Nyerere hapa Zanzibar hapo mwaka jana hatua ambayo imeweza kuonesha namna gani mashirikiano yanatekelezwa hasa ikizingatiwa kwamba kikosi hicho pia, kimekuwa kikiwatumia askari wa JKU katika ujenzi wa mradi huo kwa azma ya kupata uzoefu.

Meja Jenerali Mabele alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba katika uongozi wake ameahidi kushirikiana na kikosi cha (JKU) ili kuhakikisha kikosi hicho kinazidi kupiga hatua na kufikia malengo yaliyokusudiwa hasa katika masuala ya uzalishaji, mafunzo na mengineyo.

Alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba kikosi cha JKT kwa upande wake kitaendelea kujifunza kupitia JKU jinsi ya uimarishaji na uendelezaji wa Uchumi wa Buluu ambao ndio dira ya Uchumi wa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi.

Sambamba na hayo, Meja Jenerali Mabele alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba kikosi hicho kitaendelea kuzikumbuka jitihada alizozichukua wakati akiwa Waziri wa Ulinzi katika kukiimarisha kikosi hicho ambacho hivi sasa kimepata mafanikio makubwa na kuahidi kwamba kitaendelea kuwatumikia wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi akikutana na ujumbe kutoka Kampuni ya 54 Genetics kutoka Marekani ukiwa umefuatana na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, na kueleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Kampuni hiyo kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya hasa katika masuala ya Tanzudata ambayo ni muhimu katika kusaidia kutafuta vyanzo vya maradhi na jinsi ya kupata kinga ikiwa ni pamoja na kuzitumia maabara za kisasa.

Nae Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui alisema kwamba suala zima la vinasaba ni muhimi kwani litasaidia kujua aina za maradhi yanayowasumbua wananchi wa Zanzibar na kujua namna ya kuwakinga.