RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale ya Zanzibar, ni muhimu katika kuitangaza sekta ya Utalii nchini.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na Waziri wa Maliasili na Utalii wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro, aliefuatana na mwenyeji wake Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Lela Mohamed Mussa.Amesema Wizara hizo zina wajibu wa kuendeleza ushirikiano uliopo kati yao ili kusaidia juhudi za kuitangaza sekta ya Utalii nchini, akibainisha kuwepo ushindani mkubwa Duniani hivi sasa.

Aliushukuru Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania kwa juhudi kubwa inazochukua kuimarisha sekta ya Utalii nchini, huku akaahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuunga mkono juhudi hizo kwa kufanya kila linalowezekana kufanikisha malengo yaliowekwa.Dk. Mwinyi alisema Utalii ndio sekta kuu ya uchumi wa Zanzibar na kubainisha nguvu kubwa zilizoelekezwa na Serikali katika kuutangaza Utalii wa Zanzibar.

Alisema ni jambo jema kwa hatua iliyochukuliwa na viongozi hao ya kukaa pamoja na kujadili changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta hiyo kwa dhamira ya kuzitafutia ufumbuzi.Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaunga mkono juhudi zilizoanza kuchukuliwa ili kufanikisha uandaaji wa mikutano mbali mbali ya kimataifa kuhusiana na Utalii hapa nchini, hususan Zanzibar.

Mapema, Waziri wa Maliasili na Utalii ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro alisema dhamira ya kukutana na Waziri mwenzake wa Utalii ni kujenga ushirikiano katika kuendeleza sekta ya Utalii nchini.Alisema katika kikao cha Viongozi hao wameafikiana kutengeneza ‘Hati ya Makubaliano’ (MOU) na kuainisha maeneo ya ushirikiano kupitia ngazi tofauti, ili kuratibu vyema shughuli za utalii.

Alisema katika mazungumzo yao wamejadili changamoto mbali mbali, ikiwemo ya ‘Visa Rejea’ , akibainisha utaratibu huo kuwa mbali na kuangalia maslahi makubwa lakini unapunguza idadi ya ujio wa watalii, kiasi cha kuwepo uwezekano wa kushindwa kufikia malengo ya kupokea watalii Milioni tano nchini, kama ilivyoainishwa katika Ilani ya CCM ya 2020-2025.

“Tumejadili mkutano wa 65 wa UNWTO ufanyike Tanzania ili kuiweka nchi kwenye ramani ya Utalii”, alisema.

Alieleza kuwa Mawaziri hao wameazimia kuweka mikakati ili kufanikisha mkutano huo katika kikao cha ushindani wa nchi wanachama kitakachofanyika baadae nchini Cape Verde.Alisema Zanzibar ni eneo zuri kiutalii hivyo kupitia fursa hiyo inaweza kunufaika vyema, sambamba na kubainisha heshima kubwa iliyopata Tanzania ya kuandaa mkutano wa Expo utakaofanyika mwakani Jijini Arusha.