Media » News and Events

Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa kuhurumiana

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Imamu Mkuu wa Masjid Assalaam Mlandege Sheikh Abubakar Mbarak Mumin(kulia kwa Rais) baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Tarawekh iliofanyika jana usiku 15-4-2021,katika Masjid Assalaam na (kushoto kwa Rais) Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Khalid Ali Mfaume

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa kuhurumiana ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wanyonge wakiwemo wajane, mayatima na mafakiri.

Alhaj Dk Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokuwa akiwasalimia Waumini wa dini ya Kiislamu huko katika Masjid Tawba maarufu Jongeyani uliopo Malindi kwa Tausi, Wilaya ya Mjini,  Mkoa wa Mjini Magharibi mara baada ya kumaliza Sala ya Ijumaa.

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba kila mmoja kwa nafasi yake ni vyema akaona haja ya kuyasaidia makundi hayo katika jamii ili na wao waweze kuitekeleza ibada ya funga ya Ramadhani ipasavyo.

Alisema kuwa Waumini wasipofanya hivyo maana yake ni kwamba kutakuwa na watu ambao wamo katika jamii lakini hawatizamwi vizuri hivyo, ni vyema kila mmoja katika mwezi huu na miezi mengine akayatimaza makundi hayo.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba tayari siku za nyuma aliwahi kutoa wasia kwa wafanyabiashara kutotumia mwezi wa Ramadhani kupandisha bei ya bidhaa licha ya duniani hivi sasa kuwa na tatizo la ugonjwa wa Covid 19 tatizo ambalo limepelekea bidhaa kuadimika na kusababisha bei kupanda.

Pia, alisema kuwa kwa upande wa usafiri wa ndege na meli nao umepanda hivyo, itoshe kwamba hayo yote tayari yameshapandisha bei na kusiwe tena na watu ambao wanatumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kuweka faida za ziada hali ambayo watakuwa hawawatendei haki wanyonge katika jamii na badala yake watakuwa wanawaumiza.

Alhaj Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wafanyabiashara wote kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa kuhurumiana hivyo, mfanyabiashara anatakiwa kupata faida ya kiasi na sio kupata faida mara mbili kwani hilo si jambo la busara.

Kutokana na hilo, Rais Dk. Mwinyi aliitaka Taasisi za Serikali zenye kushughulika na kuhakikisha kwamba bei elekezi zinafuatwa wafanye wajibu wao kuzuia wimbi la wafanyabiashara kupandisha bei mara kadhaa katika kipindi hichi cha mwezi wa Ramadhani.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Zanzibar ina amani na umoja hivyo ni vyema Wazanzibari wakamsukuru MwenyeziMungu kwa kufikia hatua hiyo na badala yake wakaendelea kujituma kwa azma ya kuleta maendeleo endelevu nchini.

Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba kazi iliyobaki kwa wananchi wa Zanzibar hivi sasa ni kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anajituma katika kusaidia kuleta maendeleo ya nchi.

Aliongeza kuwa hana shaka kwamba kila mmoja akiwajibika katika nafasi yake haitochukua muda mrefu maendeleo makubwa yatapatikana hapa Zanzibar.

Mapema Sheikh Said Abubakar Alghashimiy katika hotuba ya Sala ya Ijumaa alisisitiza umuhimu wa sala ya Taraweh kwa Waumini wa dini ya Kiislamu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kumpongeza Rais Dk. Miwnyi kwa kuungana na Waumini katika misikiti mbali mbali katika sala hiyo muhimu katika mwezi huu tukufu wa Ramadhani.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi alifika nyumbani kwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji huko Magogoni, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi kwa ajili ya kumjuulia hali.

Alhaj Dk. Mwinyi pia, tokea kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan ameanza utamaduni wa kuungana na waumini wa misikiti mbali mbali katika kusali nao sala ya Taraweh ambapo hapo jana aliungana na waumini wa masjid Salam uliopo Mlandege katika sala hiyo.