RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Donald Wright na kujadili masuala mbali mbali ya kiuchumi na kimaendeleo yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nane.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Ikulu Zanzibar ambapo viongozi hao kwa pamoja walieleza jinsi hatua za maendeleo zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi huku Balozi wa Marekani akiahidi kwamba nchi yake itaendelea kuziunga mkono hatua hizo.

Katika mazungumzo hayo, Balozi wa Marekani Donald Wright aleleza jinsi alivyoridhishwa na juhudi hizo zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane katika utekelezaji wa maendeleo kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi.

Balozi Wright alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Marekani iko tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kuendeleza sekta zilizopewa kipaumbele na Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi.

Alisema kwamba zipo Kampuni nyingi kutoka nchini Marekani ambazo zimevutiwa na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane na ziko tayari kuja kuekeza hapa Zanzibar.

Aliongeza kuwa Wawekezaji kutoka nchini Marekani wako tayari kuekeza katika maeneo mbali mbali ya Uchumi wa Buluu ikiwemo utalii, uvuvi, miundombinu ya bandari pamoja na mafuta na gesi asilia.

Alisema kuwa Kampuni kubwa za Marekani zimefurahishwa na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kuvitangaza visiwa vidogo vidogo kwa kuekeza katika miradi ya maendeleo ambapo tayari Kampuni nyingi zimeonesha nia ya kuitumia fursa hiyo.

Pamoja na hayo, Balozi huyo alieleza kwamba kwa upande wa sekta ya afya, alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake anazozichukua katika kupambana na UVIKO 19, ambazo zimeonesha kuleta mafanikio mazuri.

Balozi Wright alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Marekani iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza sekta ya afya ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya UVIKO 19 pamoja na maradhi mengineyo ambayo yanawasumbua wananchi wa Zanzibar.

Alisema kwamba Serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nane katika kuendeleza sekta ya elimu, ambapo hivi sasa inaendelea kufanikisha njia bora zitakazowawezesha wanafunzi wa Zanzibar kufaidika na fursa mbali mbali za elimu zinazotolewa na Marekani kwa nchi zinazoendelea.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema kwamba amefurahishwa na dhamira ya Serikali ya Marekani ya kutaka kushirikiana na Zanzibar katika uendelezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopangwa na Serikali anayoiongoza.

Rais Dk. Mwinyi alimuhakikishia Balozi huyo wa Marekani kwamba Zanzibar ina fursa nyingi za kiuchumi kwa wawekezaji katika sekta mbali mbali huku akimuhakikishia kwamba Zanzibar iko salama na kila uchao wawekezaji wengi wanaendelea kujitokeza kwa azma ya kuja kuekeza hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba amevutiwa sana na utayari wa Serikali ya Marekani wa kushirikiana na Zanzibar katika kuwajengea uwezo watendaji sambamba na kuimarisha vipaji vya wataalamu mbalimbali ili kuhakikisha kwamba Zanzibar inatekeleza vizuri na kwa ufanisi miradi yake iliyojipangia.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa Serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza sekta ya afya na hasa kwa hivi sasa katika mapambano dhidi ya UVIKO 19.

Aliongeza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Nane inaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa hivi sasa za kutoa kinga ya maradhi hayo kwa njia ya chanjo.

Alisema kwamba tiba za chanjo zinaendelea kutolewa kwa makundi mbali mbali hatua kwa hatua ikiwa bado ni kwa njia ya hiyari huku akieleza kwamba amevutiwa na wananchi walio wengi kwa jinsi wanavyolitekeleza zoezi hilo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza azma ya Serikali ya Marekani ya kuimarisha vituo vinavyotoa huduma za elimu Unguja na Pemba.