RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa watu wanne waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea katika kijiji cha Buyubi Mkoani Shinyanga.Ajali hiyo ambayo imehusisha basi la Kampuni ya Classic lililokuwa likitokea Kampala nchini Uganda kwenda Jijini Dar es Salaam,  ilitokea jana majira ya saa 10 za alfajiri katika kijiji cha Buyubi kwenye kona ya Didia, Mkoani Shinyanga na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 26.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba yeye mwenyewe binafsi pamoja na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar wamepata mshituko mkubwa kufuatia ajali hiyo iliyotokea Mkoani Shinyanga ambayo wengi ya waliopoteza maisha na waliopata majeraha ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Bugema Uganda wanaosoma katika Kada ya Afya.“Nawaomba familia za Marehemu wote, ndugu, jamaa na marafiki kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hichi cha msiba kwa kuwapoteza Watanzania wenzetu pamoja na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wale wote waliopata majeraha kupona kwa haraka”, zilieleza salamu hizo za Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaungana na familia zote za Marehemu katika kipindi hichi kigumu cha msiba.Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba, amewataja watu waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Wahida Yussuf mkaazi wa Pemba, Josephina Joseph Mkinga mkaazi wa Dar-es-Salaam, Rehema Haji Juma mkaazi wa Unguja na Nassor Juma Khamis mkaazi wa Fuoni Unguja.

Pia, aliwataja majeruhi watano ambao wamepata majeraha ya kudumu katika viungo vya miili yao ambapo majeruhi wengine 12 walitibiwa na kuruhusiwa na hali zao zinaendelea vizuri na kubainisha kwamba basi hilo lilikuwa na abiria 43 ambapo wapo abiria wengine ambao hawakumumia.Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda Magiligimba ajali hiyo imesababishwa na mwendo kasi, ambapo dereva wa basi hilo alishindwa kukata kona ya Didia na kusababisha ajali na badala yake alikimbia ambapo jeshi hilo la Polisi limeahidi kuendelea kumtafuta.