Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduizi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameziagiza sekta zote zilizoguswa na Ripoti ya Jiolojia na Utafiti wa Madini kuyafanyia kazi maeneo yao kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, Nishati na Madini ili ripoti hiyo ilete tija kwa taifa.
Alisema, matumizi sahihi ya ripoti hiyo yatachangia uwekezaji utakaozalisha ajira katika sekta zote husika, na sekta ya ardhi itaweza kuweka mpangilio mzuri wa matumizi ya ardhi ya kilimo, ujenzi na makaazi, na pia kuiwezesha nchi kujikinga mapema na maafa kabla ya kutokezea.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo ukumbi wa Golden Tulip, Kiembesamaki Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akizindua Ripoti ya jiolojia na utafiti wa Madini, Zanzibar.Katika kufanikisha agizo hilo, Dk. Mwinyi amesisitiza kwa Wizara ya Maji Nishati na Madini kuzipatia haraka nakala ya ripoti hiyo taasisi zote zilizoguswa ili zianze kuifanyia kazi mapema iwezekanavyo.
Alibainisha kupitia ripoti hiyo nchi itakuwa na uwezo wa kujikinga na maafa kabla ya kutokezea hatua aliyoieleza itathibitisha dhana ya Jiolojia ya Zanzibar kuwa ni kichocheo cha Uchumi wa nchi.Pia, amewasisitiza wakandarasi wa majengo na kamisheni ya maafa kuitumia ripoti hiyo wanapopanga mipango yao kunusuru majanga yasitokee pamoja na kutengeneza ramani ambayo itarahisisha kujua maeneo hatarishi.
Amesema, uzinduzi wa ripoti hiyo utasaidia kuimarisha dhamira ya Serikali ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha Utalii kwani mapango yaliyogundulika katika ripoti hiyo, yataweza kutumika kama sehemu za vivutio vya utalii baada ya kuimarishwa.
Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kufarajika kwake na ushirikiano wa Wizara mbili za SMZ na SMT kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu wa ndani kushirikiana na wenzao wa Wizara ya Madini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Taasisi ya Utafiti wa Miamba na Madini (GST) ya Dodoma kufanikisha utafiti na hatimae kuandaa ripoti hiyo.
Mapema Waziri wa Maji Nishati na Madini wa Zanzibar, Shaibu Hassan Kaduara amesema, Zanzibar inahitaji kufanya utafiti wa kina zaidi hususani baharini kwani viashiria vinaonesha kuwa bado kuna madini zaidi yanayoweza kupatikana ambayo hayajagundulika katika utafiti huo uliotajwa kuwa ni wa awali.
Naye, Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Antony Peter Mavunde amesema, Kisiwa cha Pemba kinaweza kuwa na miradi mikubwa kupitia Sekta ya madini baada ya kugundulika kwa madini muhimu yanayohitajika kwa kiasi kikubwa duniani ambayo hutumika kutengenezea injini za ndege, vigae vya marumaru na vifaa vya hospitali. Pia kutasaidia ukuaji wa viwanda, upatikanaji wa malighafi na kuongezeka fursa za ajira.
Amesema, chimbuko la ripoti hiyo ni maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi ya kuzitaka Wizara mbili za Madini za SMZ na SMT kuimarisha ushirikiano kwa dhamira ya kuimarisha Uchumi wa Zanzibar.
Amebainisha kuwa sekta ya Madini kwa Tanzania bara imekuwa ikichangia kiasi kikubwa cha mapato ya nchi na kuongoza kuingiza fedha za kigeni ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2022 /2023 sekta ya madini Bara ililiingizia taifa kiasi cha shilingi trilioni moja na milioni mia saba kutokana na mauzi ya madini.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Nishati na Madini Joseph Kilangi amesema ripoti hiyo iliyoanza utafiti wake Mwezi Novemba, 2023 na kukamilika tarehe 14 Machi, 2024 itaisadia Zanziabr kupiga hatua kwenye sekta ya madini.Alisema, kwa mujibu wa uchunguzi wa kina wa miamba uliofaywa kwa maeneo mbalimbali Unguja na Pemba ulibaini sampuli 189 za madini nakuonesha kuwepo kwa miamba yenye chokaa kwa matumizi ya viwanda, kiasi kikubwa cha maji kutokana na miamba inayohifadhi maji, mafuta na gesi.