Media » News and Events

Dk. Hussein Mwinyi, leo tarehe 4 Oktoba 2021 amepokea taarifa ya maandalizi ya Tamasha la Vyakula vya Baharini (Zanzibar Seafood Festival)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Wadhamini wa Tamasha la Sea Food Festival linalotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii katika Mkoa wa Kaskazini Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Mwinyi, leo tarehe 4 Oktoba 2021 amepokea taarifa ya maandalizi ya Tamasha la Vyakula vya Baharini (Zanzibar Seafood Festival) lenye kauli mbiu ya Kamata Mshipi Vumba ni Fursa litakalofanyika tarehe 8 na 9 Oktoba, 2021 kwenye pwani ya Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Rais Dk. Hussein Mwinyi amewapongeza waandaji na wadhamini wa tamasha hilo kwa ubunifu mkubwa walioufanya huku akitoa rai kufanyika kwa matamasha zaidi ili kuchochea shughuli za utalii kwani uchumi wa Zanzibar umebebwa na Utalii.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud amemueleza Mhe. Rais kuwa maandalizi ya tamasha hilo ambalo lengo kuu ni kuunganisha mawasiliano baina ya wavuvi, wakulima wa baharini na walaji wa bidhaa mbalimbali za baharini yamekamilika kwa asilimia kubwa.

Ameongeza kuwa, fedha zitakazopatikana katika tamasha hilo zitatumika kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii katika mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, ujenzi na ukarabati wa barabara ya kilometa 2.5, Upandaji wa mikoko baharini pamoja na kuwawezesha wavuvi na wakulima wa mwani.