RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaomba wananchi wa Zanzibar wamuunge mkono katika kutekeleza azma yake ya kuiletea maendeleo Zanzibar sambamba na kupambana na ufisadi.Alhaj Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika Msikiti wa Ijumaa Miembeni, Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akitoa salamu kwa Waislamu mara baada ya kukamilisha Sala ya Ijumaa.

Katika salamu zake hizo Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa uungwaji mkono pamoja na dua vinahitajika kutokana na wanaofanya hayo wananufaika na pale panapozuiwa kutofanya na wao watatafuta la kufanya.Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba amegombea nafasi hiyo kwa azma ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar ambapo katika kutekeleza hayo yapo mambo ambayo yatafanywa na kuwaudhi watu kwa hivyo, uungwaji mkono unahitajika kwani yatakayofanywa yatawanufaisha wengi.

Alisema kuwa kwa hatua zinazochukuliwa hivi sasa maendeleo na mafanikio makubwa yatapatikana kwa sababu mambo muhimu ikiwemo amani na umoja yapo nchini licha ya wachache ambao hawajakubali na kueleza kwamba watazidi kuelimishwa.Aliushukuru uongozi wa msikiti huo ambao una historia kubwa katika misikiti ya Mji wa Zanzibar pamoja na kuisifu hutuba ambayo imeeleza mambo mengi huku akiahidi kushirikiana na waumini hao katika kuuendeleza msikiti huo.

Alisema kuwa tokea aingie madarakani viongozi wamekuwa wakiwasisitiza wananchi kuwa wamoja hatua ambayo itapelekea kupatikana maendeleo yanayotarajiwa kwani ili kupata maendeleo ni lazima kuwepo kwa amani, umoja na uwajibikaji.Alisema kuwa viongozi wa siasa wameweza kuhubiri amani na umoja kwa vitendo kwa kuungana na kujenga Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa dhamira ya kuleta umoja katika nchi.Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa dini kwa kuhubiri amani na umoja hapa nchini.

Kwa upande wa uwajibikaji Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa jambo hilo halina mtu maalum bali kwa kila mmoja anatakiwa kuwajibika wakiwemo viongozi na wale wasiokuwa viongozi, waliokuwa nje na ndani ya Serikali wote wanatakiwa wawajibike.Alisema kuwa kukua kwa uchumi kunahitaji kila mmoja kufanya kazi sambamba na uwajibikaji kwa kila mtu kwa azma ya kupata manufaa na maendeleo endelevu.

Katika salamu zake hizo, alisema kuwa kuwepo kwa amani, umoja na kila mtu akiwajibika mafanikio yatapatikana lakini wakitokea wabadhirifu, wazembe, wezi wa fedha za serikali na wala rushwa hapatakuwa na maendeleo.Alisema kuwa kwa makusudi jukumu limechukuliwa katika kuhakikisha hayo yote yanapigwa vita kwa nguvu zote na kuwataka wananchi wote wa Zanzibar kuunga mkono katika jambo hilo pamoja na kuwaombea dua viongozi wanaopambana.

Aliwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kuwepo kwa umoja, amani na mshikamano nchini na kuwaona wananchi wakiwa na muelekeo wa kuwajibika katika nchini yao na kueleza imani yake ya kuona kila mtu anawajibika.

Mapema akisoma hotuba ya Sala ya Ijumaa Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume ambaye pia ni Imamu wa msikiti huo alisema kuwa Mwenyezi Mungu anasema kwamba hakika Waumini wote ni ndugu na vyema ikatafutwa suluhu pale wanapokosana sambamba na kumcha Mwenyezi Mungu ili wapate kurehemewa.Alisema kuwa suluhu ni jambo jema na migongano haina neema kwani Mwenyezi Mungu amekuwa akisisitiza umoja huku akieleza wale waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu wakiwemo walarushwa, wezi na wabadhirifu hivyo akitokea kiongozi wa kupambana na hayo ni vyema akaombewa dua.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi alifika nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Tano Dk. Salmin Amour Juma kwa ajili ya kumjuulia hali na kuzungumza nae.