RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Zanzibar na Oman na kueleza haja ya kuongeza ushirikiano zaidi katika sekta ya biashara.Rais Dk. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Oman Abdalla Abbas Kilima aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha na kusalimiana na Rais.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Zanzibar inahistoria nzuri kati yake na Oman na tayari kumekuwa na mahusiano na mashirikiano mazuri katika nyanja mbali mbali lakini ni vyema mashirikiano hayo pia, yakaimarishwa kwenye sekta ya biashara.Alieleza kuwa Oman ni mdau mkubwa wa maendeleo kwa Zanzibar hivyo, ni vyema uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliopo ukaimarishwa zaidi.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Serikali ya Oman kwa kuonesha utayari wa kusaidia ukarabati wa majengo ya kale yakiwemo Beit al Ajaib pamoja na jumba la wananchi Forodhani ambapo mchakato wake unaendelea.Alisema kuwa tayari kwa upande wa ujenzi wa Bandari, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini Hati ya Maelewano na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman inayohusu mpango mkuu wa ujenzi wa bandari ya Mangwapwani/Bumbwini pamoja na kuigeuza Bandari ya Malindi kuwa ya Kitalii ambapo Serikali iko tayari katika ushirikiano huo na Serikali ya Oman.

Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa utayari wa Kampuni hiyo kwa kufanya upembuzi yakinifu kwa fedha zao wenyewe pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya ndege ya Oman kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Zanzibar kwa azma ya kuja kuekeza katika viwanja vya ndege Unguja na Pemba.Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa Serikali ya Oman kutoa fursa katika kupata soko la bidhaa za Zanzibar nchini humo kwani soko la ‘Gulf’ ambalo limekuwa na uzoefu na historia kubwa ya bidhaa za Zanzibar.

Alieleza haja ya kuwepo kwa soko la uhakika la bidhaa za Zanzibar nchini Oman zikiwemo bidhaa za matunda, mwani, viungo na karafuu hasa ikizingatiwa kwamba bei ya dunia ya karafuu imekua ikishuka hivi sasa.Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua ya mashirikiano yaliopo kati ya Zanzibar na Oman na kueleza jinsi Mamlaka ya Uwekezaji wa Oman ilivyotiliana saini na Zanzibar katika Mpango Mkuu wa Ujenzi wa Bandari ya Magapwani/Bumbwini.

Nae Balozi wa Tanzania nchini Oman alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi sambamba na kazi nzuri ambazo ameanza kuzifanya katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.Balozi Kilima alieleza kwamba Serikali ya Oman imekuwa na uhusiano mwema na wa kihistoria na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar na kueleza hatua ambazo Oman inaendelea kushirikiana na Zanzibar ikiwemo ukarabati wa majengo hayo ya kihistoria.

Hivyo,  ameahidi kulifanyia kazi suala zima la biashara kati ya Zanzibar na Oman hasa ikizingatiwa kwamba tayari kuna Baraza la Biashara ambalo liliundwa kwa ajili ya mashirikiano katika sekta hiyo kati ya Tanzani na Oman.Aidha, alieleza azma ya Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Oman kukutana na kuimarisha mashirikiano na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na uongozi wa Chuo Kikuu Huria chini ya Makamo Mkuu wake Profesa Elifas Tozo Bisanda ambapo katika mazungumzo yao uongozi huo uliumpongeza Dk. Mwinyi pamoja na chama chake cha CCM kwa ushindi uliopata katika uchaguzi mkuu uliopita.Aidha, uongozi huo ulimpa pole Rais Dk. Mwinyi kwa misiba iliyotokea ya Kitaifa ukiwemo msiba wa Hayati Dk. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.

Pia, uongozi huo ulitumia fursa hiyo kumuomba Rais Dk. Mwinyi kuwapelekea salamu zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kupokea vyema majukumu ya Urais sambamba na kuendeleza amani na utulivu nchini.Uongozi huo ulimueleza Rais Dk. Mwinyi mafanikio makubwa yaliopatikana tokea kuanzishwa kwa chuo hicho hapa Zanzibar mnamo mwaka 1994 ambapo hadi mwaka wa masomo uliomalizika Juni mwaka uliopita wameweza kudahili wanafunzi wapatao 4,534 hapa Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Profesa Basinda alieleza kwamba kati ya wanafunzi hao waliohitimu ni 1,855 sawa na asilimia 41 ya waliodahiliwa ambapo hayo ni mafanikio makubwa kwa Zanzibar kwani katika vyuo huria wanafunzi wanaofanikiwa kuhitimu huwa hawazidi asilimia 25.

Nae Rais Dk. Mwinyi kwa upande wake alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi huo pamoja na Chuo hicho kwa juhudi zake kubwa unazozichukuwa katika kutoa elimu kwa wanafunzi wa Zanzibar ambao wamekwua wakifanya vizuri.Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake na chuo hicho ili kizidi kupata mafanikio.