Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameshiriki hafla ya uwasilishaji wa Ripoti ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Katika uwasilishaji huo, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman, ameeleza kuwa uchunguzi umebaini kuwa maandamano yaliyofanyika hayakuwa ya amani kama ilivyodaiwa, bali yalilenga kuvuruga mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.
Baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Tume kwa kazi kubwa iliyofanywa kwa uwazi, weledi na uzalendo, na kuwashukuru Watanzania kwa utulivu wao, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza umoja na mshikamano wa kitaifa.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali zote mbili, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wastaafu, mabalozi, wawakilishi wa jumuiya za kimataifa pamoja na wananchi.