Media » News and Events

Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo Septemba 30, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Mhe. Tony Charles Blair Ikulu Mjini Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Waziri Mkuu Mstaaf wa Uingereza Mhe.Tony Blair, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo Septemba 30, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Mhe. Tony Charles Blair, Ikulu Zanzibar.Mhe. Rais Dk. Mwinyi amemshukuru Mhe. Blair kwa ujio wake wa mara ya pili visiwani Zanzibar katika muendelezo wa ushirikiano baina ya Taasisi ya Mabadiliko Ulimwenguni ya (Tony Blair Institute For Global Change) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi amesema taasisi hiyo itakuwa na jukumu la kuisadia Serikali katika kubadilisha mifumo na kuhakikisha sera na mipango ya Serikali ya Awamu ya Nane inafanyika kwa vitendo, Uwezeshaji kiuchumi pamoja na kuwajengea uwezo watendaji wa Serikalini.Rais Dk. Mwinyi ameongeza kuwa maeneo muhimu ambayo taasisi ya Tony Blair itawekeza nguvu ni pamoja na Sekta za Uchumi wa Buluu ikiwemo Utalii, Mafuta na Gesi baharini, Bandari na Uvuvi. Aidha Wataalamu wa taasisi hiyo wataisaidia Serikali katika Sekta za Kijamii ikiwemo Elimu, Maji, Barabara, Umeme na Uwezeshaji wa Ajira kwa Jamii.

“Hatuna shaka kupitia uzoefu wake tutaweza kufanikiwa ikiwa tutafuata miongozo na maelekezo ya wataalam wao watakavyotuelekeza”. Alisema Rais Dk. Mwinyi.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza. Mhe. Tony Blair amesema, Taasisi yake imefurahishwa na kuridhishwa na kazi inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dk. Mwinyi na iko tayari kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo na kujenga taasisi imara.

Download File: