RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Taasisi ya “The Brenthust Foundation” kwa kufanya kazi nzuri ya utafiti unaohusu upangaji na utekelezaji wa mipango na Sera za kiuchumi kwa maendeleo ya Zanzibar.Rais Dk.Mwinyi alisema kuwa lengo la Taasisi hiyo kufanya utafiti ni kuweza kushirikiana vizuri na Serikiali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala mbali mbali ya utungaji na utekelezaji wa mipango na Sera za kiuchumi.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar mara baada ya kupokea taarifa ya utafiti huo ambao utasaidia katika kutafuta njia bora na zenye ufanisi katika kuinua uchumi wa Zanzibar,taarifa ambayo imetolewa na Taasisi ya “The Brenthust Foundation”.Akitoa shukurani zake kwa timu hiyo ya utafiti, Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi alisema kuwa kuna kila sababu ya kuipongeza timu hiyo ambayo imefanya utafiti huo tena kwa kipindi kifupi ikiwa na lengo la kufanikisha njia bora za kuinua uchumi wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imejikita zaidi katika Sera yake kubwa ya Uchumi wa Buluu kutokana na Zanzibar kubarikiwa na rasilimali nyingi za bahari.Alisisitiza kwamba hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kutambua kuwa licha ya Zanzibar kuzungukwa na bahari lakini inaonekana kwamba bado bahari haijatumiwa ipasavyo katika suala zima la uchumi.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha Sera hiyo ya Uchumi wa Buluu inaimarika kuna sekta muhimu ambavyo zimepewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii,uvuvi, Miundombinu pamoja na sekta ya mafuta na gesi asilia.Aidha,Rais Dk.Mwinyi alieleza kuwa licha ya changamoto zilizokuwepo ikiwemo ya mtaji,lakini bado juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kwamba anafarajika kwa kuwa wapo wanaoijitokeza kuunga mkono juhudi hizo.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Olusegun Obasanjo na timu yake akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya “The Brenthust Foundation” Greg Mills pamoja na Jonathan Oppenheimer ambaye ni Mwanzilishi wa Taasisi hiyo ambao wamekuja Zanzibar kushiriki katika utoaji wa taarifa hiyo pamoja na kushirikiana nao katika uzinduzi wa kitabu cha “Asian Aspiration Book” cha Rais Olusegun Obasanjo na Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn huko katika ukumbi wa Hoteli ya Verde.

Rais Dk. Miwnyi aliwahakikishia kwamba Serikali yake itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa kupitia utafiti huo pamoja na rai mbali mbali zilizotolewa katika utafiti.Pia, Rais Dk. Miwnyi alisema kwamba amefurahishwa kuona kwamba mambo mengi yaliyobainika katika utafiti huo yameonekana kuwa yanakwenda sambamba na mikakakti iliyopangwa kutekelezwa na Serikali jambo ambalo alisema litasaidia sana katika kufikia malengo yaliyowekwa.

Alisema kwamba ni kweli maendeleo yanayohitaji mitaji na rasilimali watu, hata hivyo kazi kubwa inahitajika na taasisi hiyo katika utafutaji wa mitaji ambayo ndiyo kikwazo kikubwa hivi sasa.Kuhusu rasilimali watu, Rais Dk. Mwinyi alifahamisha kwamba, Zanzibar ina wafanyakazi wengi walio somea fani mbali mbali ambapo hata hivyo aliahidi kushirikiana na taasisi hiyo katika kuwajengea uwezo.

Mapema akitoa maelezo yake Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo alisema kuwa ana matumaini makubwa kwamba uchumi wa Zanzibar utaimarika hiyo ni kutokana na mikakati maalum iliyowekwa na Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi.Katika maelezo yake alisema kuwa utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya “The Brenthust Foundation”, utakuwa chachu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuyafikia malengo iliyojiwekea.

Nae Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn alieleza imani yake juu ya utafiti huo uliofanywa hapa Zanzibar ambao utaleta majibu chanya katika kuhakikisha Zanzibar inapata mafanikio kama ilivyopata visiwa vyengine vikubwa ambavyo vimezungukwa na bahari.Akitoa taarifa ya Utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa utafiti huo Ray Hartley alieleza jinsi utafiti huo ulivyofanywa na hatimae kuweza kupata mafanikio makubwa.

Alisema kwamba ili Zanzibar iweze kupata maendeleo zaidi ni vyema Serikali ikaweza kuchukua maamuzi magumu katika kutekeleza mambo yenye maslahi mapana kwa taifa na wananchi kwa ujumla kwa kila pale inapobidi kufanya hivyo.Vile vile, mtafiti huyo alihimiza umuhimu wa kukubali mabadiliko yanayotokezea baadhi ya wakati katika utendaji.

Ray Hartley alitumia fursa hiyo kueleza jinsi ya sekta mbali mbali ambazo iwapo zitafanyiwa kazi ipasavyo zitasaidia kukuza na kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwemo sekta ya utalii, uvuvi, kilimo na nyenginezo.Pia, alitumia fursa hiyo kueleza jinsi ya maradhi ya COVID 19 yalivyopelekea kudhorotesha kuimarika kwa uchumi wa dunia ikiwemo Zanzibar.