Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar ina nafasi nzuri ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kilimo na usarifu wa mwani, uchimbaji mafuta na gesi, utalii, na bandari kwa Indonesia kutokana na uzoefu, mbinu, na teknolojia waliyonayo, hasa katika upande wa Uchumi wa Buluu.Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Jukwaa la Uwekezaji la Zanzibar - Indonesia 2024, ambalo limeandaliwa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), katika hoteli ya Sofitel, Bali, Indonesia, tarehe 1 Septemba 2024.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amebainisha kufurahishwa na muamko wa jukwaa hilo kwa kujitokeza kwa wingi wawekezaji ambao wameonyesha nia ya kuwekeza Tanzania, ikiwemo Zanzibar. Hivyo, tutarajie wawekezaji mbalimbali, hususan katika sekta ya Uchumi wa Buluu kutoka Indonesia.

Jukwaa hilo la kimkakati limewakutanisha viongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Jamhuri ya Indonesia wakiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Sharif Ali Sharif; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury; Waziri wa Madini Tanzania, Mhe. Anthony Mavunde; Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Makocha Tembele pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji. Jukwaa hilo limelenga kukuza ushirikiano wa kiuchumi kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu, ukiwemo utalii, bandari, mafuta na gesi, usafiri wa baharini, uvuvi, na usarifu wa mwani.

Rais Dk. Mwinyi amewasili Bali, Indonesia tarehe 31 Agosti 2024 kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika 2024 unaotarajiwa kuanza kesho tarehe 2 Septemba 2024.